Na Waandishi Wetu
WATU sita wamekufa na wengine 41 katika ajali mbili zilizotokea katika mikoa ya Mtwara na Mbeya jana.Ajali ya kwanza ilitokea baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Landrover 110 kupinduka na kushika moto katika Kijiji cha
Kimondo kilichopo wilaya ya Mbeya vijijini mkoani hapa.Chanzo cha moto huo kinadaiwa kilitokana na mafuta ya akiba kumwagika baada ya gari hilo kuanguka majira ya saa 5:00 asubuhi, kutokana na ubovu wa barabara hiyo.
Gari hilo ambalo lilikuwa na abiria zaidi ya 15 lilikuwa likielekea wilayani Makete mkoani Iringa likitoka Uyole, na kwamba kabla ya kuteketea kwa moto lilipinduka baada ya kuyumba mara kadhaa.
Mmoja wa abiria ambaye alinusurika, Abrahamu Sanga (20) alisema kuwa alikuwa ni abiria katika gari hilo akielekea Makete mkoani Iringa wakiwa wamepanda juu ya eneo ambalo linatumika kubebea mizigo na kwamba alipoona gari hilo linayumba aliruka na muda mfupi baadaye gari hilo lilipinduka na kushika moto.
Alisema kuwa wenzie wawili waliangushwa chini na kujeruhiwa wakati gari hilo linaanza kuteketea kwa moto huku yeye akijitahidi kufungua mlango wa nyuma wa gari kwa kuugonga kwa jiwe ili abiria wengine watoke.
Mama mmoja ambaye ni mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo aliyetambulika kwa jina la Hilda Joseph alisikika akilalamika kuwa amepoteza watoto wake wawili wa kiume ambao alikuwa akisafiri nao kwenda Makete.Muuguzi wa zamu katika kitengo cha msaada wa haraka cha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Dkt. Dominick Challo alisema kuwa amepokea majeruhi 11 na wawili kati yao hali zao ni mbaya.
Majeruhi hao ni pamoja na watoto wawili Evans Stephen (miezi saba), Latifa Labison (mwaka mmoja), Bi. Sara Charles (50) na Bw. Bahati Mwavipa (29) ambaye ni dereva wa gari hilo aliyeungua vibaya mgongoni na mbavuni.Wengine ni Victoria Sanga (10), Bw. Okoka Matamsi (20), Bi. Hilda Japhet, Bi. Huruma Israel (38), Bi. Jane Mbalila(21) Bi. Vaileth Stephen (30) na Bw. Juhudi Erick (28).Wakati huo huo watu wanne walikufa jana na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea Masasi, mkoani Mtwara, wakienda harusini.
Akizungumza na majira mmoja wa watu walioshuhudia alisema ajali hiyo alisema ilitokea majira ya saa 2:30 asubuhi katika eneo la darajani wilayani Masasi mkoa wa Mtwara.Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Bw. Steven Buyuya abiria hao walikuwa wanasafiria gari aina ya Canter ambalo lilikuwa limekodiwa kwa jili ya kuwapeleka harusini.
Aliongeza majeruhi wa ajali hiyo wamelazwa katika hospitali za Misheni Ndemba na Nkomaido na maiti zimefadhiwa katika Hospitali ya Ndanda huku dereva wa gari hilo akishikiliwa na polisi.
No comments:
Post a Comment