21 December 2010

Mwaka mpya umeme bei juu

Na Grace Michael

FURAHA ya Watanzania kusherehekea kuanza kwa mwaka mpya wa 2011 imetumbukia nyongo baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuruhusu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupandisha
bei umeme kwa asilimia 18.5.

Kwa uamuzi huo ulitolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa EWURA, Bw. Haruna Masebu, hapana shaka mwaka huo utaanza kwa bidhaa mbalimbali kupanda bei kutokana na gharama za uzalishaji kuwa juu kutokana na kupanda kwa kwa nishati hiyo.

Hata hivyo, kiwango hicho cha asilimia 18.5 kitakachoanza kutozwa Januari Mosi, mwakani ni karibu nusu ya ongezeko lililoombwa na TANESCO la asilimia 34.6.

Bw. Masebu alisema Dar es Salaam jana kuwa wamefikia uamuzi huo bila kupendelea upande wowote na kwa kuzingatia mawazo yaliyotolewa na wadau wakati wa kujadili maombi ya shirika hilo.

"TANESCO waliomba ongezeko la asilimia 34.6 lakini baada ya kuangalia kwa makini gharama zao za uendeshaji na kwa kuzingatia mawazo ya wadau ambao walishirikishwa, tulifikia uamuzi wa kukubali ongezeko la asilimia 18.5 ili shirika liweze kujiendesha na hatimaye kutoa huduma nzuri kwa wananchi," alisema Bw. Masebu.

Alisema kuwa baada ya kupata maombi hayo, waliyaangalia kwa kina na ilionekana kuwepo kwa hoja ya msingi, lakini haikukubaliwa kama ilivyowasilishwa.Kulingana mambo hayo, TANESCO iliomba kuongeza bei ya umeme kwa kipindi cha miaka mitatu kwa maana ya asilimia 34.6 kwa mwaka 2011, asilimia 13.8 kwa mwaka 2012 na asilimia 13.9 mwaka 2013.

Kuhusu mambo hayo ya miaka miwili iliyobaki, Bw. Maseru alisema kuwa wataangalia baada ya suala hilo kufanyiwa utafiti wa kutosha na mtaalamu atakayependekezwa na EWURA hapo kufanyika na kumalizika mwakani.

Hata hivyo, EWURA imeitaka TANESCO kuhakikisha inafungua akaunti maalumu zikiwemo za matengenezo na marekebisho, mpango wa uwekezaji wa mtaji, mpango wa gharama za kukunua umeme unaozalishwa nje.

Masharti haya yanalenga kudhibiti mapato ya TANESCO ili kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa kila mpango zinatumika kama ilivyokusudiwa, na akaunti hiyo itakaguliwa kila baada ya miezi mitatu.

"TANESCO italazimika kuingiza kwenye akaunti hiyo sehemu ya jumla ya gharama zilizoidhinishwa kwenye masharti ya akaunti hiyo kila mwezi," alisema Bw. Masebu.Alisema kuwa sababu zilizoifanya EWURA kukataa mapendekezo ya sasa kutokana na utafiti uliofanywa na TANESCO ni kutoweka wazi gharama za uzalishaji na usambazaji ili kuiridhisha mamlaka hiyo.

"Makadirio, mtazamo, takwimu zilizotumika haziakisi ukweli wa gharama za huduma zinazotolewa na TANESCO. Kutokana na hatua hiyo, ndio maana tulifikia uamuzi wa kuidhinisha nyongeza ya mwaka mmoja," alisema Bw. Masebu.Katika nyongeza hiyo, EWURA imeitaka TANESCO kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaongezeka lakini pia wakiunganisha wateja wapya zaidi ya 100,000 kwa mwaka 2011.

5 comments:

  1. Jamani watanzania, hivi akili zetu kweli zinafanya kazi kweli! Wananchi wengi wanashindwa kuunganishiwa umeme kwa ajili ya rushwa iliyoko Tanesco, mara waseme nguzo ukiwapa chochote ndipo wanakuwekea. Wanasema tupe chochote ili tudanganye kwamba nguzo imeanguka eneo fulani kwa ajili ya mvua nyingi. Hivi kweli nchi hii tutafika kweli. Wananchi wa vijijini hata kupata koloboi kwa ajili ya kuwamulikia usiku ni shida. Sasa ndo watafikiria kuweka umeme kweli. Mimi ninaona ili tuweze kupata huduma bora ni bora shirika hili ligawanywe mara mbili ili washindane kutoa huduma bora. Tena tuwaombe watu wa nje kuja kuwekeza kwenye umeme ushindani ukiongezeka nina hakika Tanesco watabadilika. Ufisadi utakwisha. Uzarishaji utaendelea. La sivyo jamani hata dreva tu anamwibia mwananchi hivi kweli? Kazi yao ni kulipatana posho na masurufu ya ajabu ajabu.

    Mazingira yetu yataendelea kuharibiwa kwa kuwa Tanzania haina watu wenye uchungu na nchi yetu. Tunaingia karne nyingine bado watu wetu hata wa mijini hawana uwezo wa kuweka majiko ya umeme ili kupunguza matumizi ya mkaa. Sasa tena badala ya kuwapunguzia wananchi tena shirika linawaongezea mzigo! Sina hakika kama tutafika mbele ya safari. Wao wasingeozea wananchi gharama za umeme wangeliwabana wale wote wanaokwepa kulipa bili za umeme tunajua mashirika mbalimbali yanayokwepa kulipa ankara za umeme. Wanadaiwa mabilioni ya shillings. Hao wangelibanwa na watu wote walipe kama inavyostahili siamini kama shirika lingeshindwa kujiendesha. Ila kwa kuwa wapo wakubwa na mashirika mbalimbali wanaohonga ili wasidaiwe hata Tanesco iwaongezee maskini ni sawa na bure tu. Na ni dhambi kubwa watu wenye fedha na mashirika mbalimbalil kushindwa kulipa bill zao na kuwatwika mzigo huo maskini wa Tanzania. Ipo siku tu Tanzania itapona CCM itakapoondoka kwenye madaraka kwa nguvu ya umma

    ReplyDelete
  2. ONGEZENI BEI YA UMEME ISAIDIE KULIPIA DENI LA DOWNS

    ReplyDelete
  3. WIZI MTUPU! SHWAINI!!!!!!!!

    ReplyDelete
  4. Mchangiaji wa mwanzo umetoa pointi nzuri. Hawa Tanesco ni wazembe, vichwa maji na wamekosa fikra bora za kuongeza ufanisi katika uendeshaji na uzalishaji wa umeme nchini ingawa wana monopoly karibu nusu karne sasa.

    Dawa ya moto ni moto. Wahenga wamesema vita vya samaki ni furaha ya mvuvi.Tufanye hivi:

    1. Tanesco ipunguziwe madaraka wabaki wazalishaji na wasambazaji wa umeme full stop. Kuundwe chombo cha kusimamia mauzo. Tenda itolewe kwa kampuni binafsi zenye uwezo na ufanisi. Lengo hapa ni kuboresha ukusanyaji wa mauzo ambapo fedha hizi zitasaidia kufanisisha na kuendeleza Tanesco

    2. Kuwe na bodi ya kutoa viwango vya uuzaji wa umeme ambayo itazingatia gharama za uzalishaji, uchumi na ufanisi. Efficiency kiwe ndio kigezo kikubwa

    3. Investors waruhusiwe na wapewe motisha kuweka rasilimali katika sekta hii.

    4. Kuwe na mfuko maalum wa kuwapa motisha wananchi kuanzisha alternative energy production units ambapo umeme wao wa ziada utaingizwa katika National Grid.

    ReplyDelete
  5. Dawa si kuongeza bill za umeme, bali ni sera mbovu za uongozi waliopo madarakani. Hawana ubunifu wowote wana mawazo mgando. HII ni karne ya ngapi tunazungumzia matatizo ya upatikanaji wa umeme, wakati kila kitu kinapatikana kuanzia mito(hydro power),gesi asilia, makaa ya mawe, na uranium.

    ReplyDelete