20 December 2010

Polisi wadaiwa kuua mtuhumiwa

Na Wilhelm Mulinda, Mwanza

ASKARI Polisi wa Kituo Kidogo cha Mirongo jijini hapa wanadaiwa kuua mtuhumiwa kwa kipigo wakati wakimshinikiza aeleze alikokuwa ameficha fedha alizotuhumiwa kuiba dukani kwa tajiri wake, Mtaa wa Uhuru mjini hapa.Tukio hilo
limekuja siku moja baada ya polisi mkoani Arusha kudaiwa kumpiga mbunge wa Arusha mjini, Bw. Godbless Lema wakidai amekaidi amri yao ya kumwondoa katika Kikao cha Baraza la Madiwani.

Mtuhumiwa huyo, Bw. Joseph Godfrey ambaye alikuwa mkazi wa Bugarika jijini hapa, alikamatwa na kufikishwa kituoni hapo Desemba 16 jioni baada ya tajiri yake, Bi. Nura Abrahaman kumtuhumu kwamba alimwibia sh. 700,000 dukani kwake.

Fedha hizo zilikuwa ni sehemu ya mauzo ambayo Bi. Nura alipata baada ya kuuza gari lake na Bw. Godfrey kutuhumiwa kuziiba kwa kushirikiana na watu wengine wawili ambao majina yao hayakufahamika.

Habari kutoka kwa baadhi ya wananchi zinadai kuwa baada ya Godfrey kufikishwa kituoni hapo, polisi walianza kumshushia kipigo sehemu mbalimbali mwilini wakitaka aeleze alikoficha fedha hizo na kuwataja wenzake alioshirikiana nao katika kufanya kitendo hicho.

Inadaiwa kuwa kutokana na kipigo hicho ambacho kilichukua muda mrefu, Bw. Godfrey alisikika akipiga kelele, hali iliyowashtua wapita njia pamoja na wakazi walio jirani na kituo hicho.

Inaelezwa kuwa baada ya polisi kuona kwamba Bw. Godfrey hali yake ni mbaya, walimpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou-Toure kwa ajili ya kutibiwa wakidai kuwa alipigwa na wananchi wenye hasira kali baada ya kuthumiwa kuiba.

Maelezo hayo ya polisi yalionekana kuwachanganya wauguzi wa zamu waliokuwa mapokezi na kukataa kumpokea Bw. Godfrey kwa kile kinachodaiwa kuwa hali aliyokuwa nayo ilionekana kwamba alipigwa na kitu kigumu kwenye maungio ya mikono na miguu na sehemu mbalimbali za mwili.

Kutokana na hali hiyo askari hao waliamua kumpeleka Bw. Godfrey katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mwanza kwa ajili ya kupata msaada zaidi, ili aweze kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini hapa.

Taarifa hizo zinadai kuwa Bw. Godfrey alifariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 17, mwaka huu wakati akiwa mapokezi katika hospitali hiyo ya rufaa akisubiri kupatiwa matibabu.Inasemekana kuwa baada ya Bw. Godfrey kufariki, polisi  walimkamata Bi. Abrahaman wakidai kuwa yeye ndiye alimtuhumu na kupiga yowe iliyofanya wananchi kukusanyika na kuanza kumshambulia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Simon Sirro alisema jana kwa njia ya simu kuwa bado alikuwa akiwasiliana na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Nyamagana jijini hapa ili atoe taarifa kamili kuhusina na tukio hilo.

No comments:

Post a Comment