Na Rashid Mkwinda, Mbeya
NDEGE ndogo ya kukodi iliyokuwa ikimuwahisha mgonjwa mahututi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanguka porini na kusababisha kifo cha mgonjwa huyo na kujeruhi wengine wawili.Bwana Godfrey Mpoli alikuwa amelazwa katika
Hospitali ya Rufaa Mbeya akiwa mahututi, na hali ilipoendelea kuwa mbaya iliamuliwa ahamishiwe MNH kwa matibabu zaidi.
Taarifa za awali zimedai kuwa ndege hiyo ya kukodi ilitakiwa kuondoka katika Uwanja wa Ndege wa Mbeya asubuhi lakini kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya rubani alikataa kuruisha.
Ndege hiyo ilikuwa na abiria watatu na rubani huyo iliruka baadaye baada ya kuona hali imekuwa nzuri, lakini hata hivyo ilianguka karibu na Kituo cha Utafiti wa Kilimo Uyole nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
Wengine waliokuwamo ni Muuguzi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mbeya, Bi. Florence Mapunda na daktari kutoka Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dkt. Jonas Chitemo ambaye amevunjika mkono wa kulia.
Akizungumzia ajali hiyo, Dkt. Chitemo alisema mgonjwa huyo alilazwa katika hospitali hiyo kwa siku tatu katika chumba cha wagonjwa mahututi, kabla ya uamuzi wa kumhamisha baada ya kushindwa kubaini tatizo.Alisema mgonjwa huyo alikuwa akipelekwa MNH jijini Dar es salaam kwa ajili ya vipimo zaidi.
Bi.Mapunda ambaye amepata maumivu ya ndani kwa ndani, alisema kuwa rubani wa ndege hiyo alijitahidi kuepusha madhara zaidi kwa kuielekeza ndege hiyo bondeni badala ya kugonga mlima ilipokuwa inaelekea.
Wakati rubani wa ndege hiyo alichukuliwa wazungu wenzake baada ya kuwasili hospitalini hapo bila kusema chochote kuhusu sababu za ajali hiyo, Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Bw. Advocate Nyombi hakupatikana kuizungumzia.
No comments:
Post a Comment