21 December 2010

Mourinho alia na waamuzi Hispania

MADRID, Hispania 

KOCHA Jose Mourinho, ameitaka timu ya Real Madrid kumsaidia ili kukabiliana na waamuzi baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa baoa 1-0 dhidi ya Sevilla, ikiwa nyumbani licha ya beki wake Ricardo Carvalho, kutolewa nje ya uwanja mapema kipindi cha
pili.

“Kuna makosa makubwa 13 yamefanywa na mwamuzi,” Mourinho aliuambia mkutano wa waandishi wa habari, baada ya mechi hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa  Bernabeu.

“Sijisikii kuwa na presha wakati ninapokuwa nafanya ninachotaka kufanya na ninapenda kuwa kocha. Nimechoshwa na jambo hili, timu yangu inapaswa kulindwa na endapo nitasema ninachokiwaza kesho nitakuwa ukurasa wa mbele kwenye magazeti na nitafungiwa," aliongeza na akasema kuwa kuna klabu na mfumo wake na anataka timu yake ilindwe kuhusu jambo hilo.

Mourinho alisema anaandaa orodha ya waamuzi, hivyo anahitaji msaada mwingine kutoka ndani ya klabu kulivalia njuga suala hilo, ili kukwepa kuadhibiwa huku akisema anahitaji kuwa na kikao binafsi na Rais wa klabu hiyo, Florentino Perez.

“Nina mahusianbo mazuri na klabu, licha ya kuwa tuna mawazo tofauti,” aliongeza.Kocha huyo Mreno tayari ameshafungiwa mechi mbili, baada ya kutolewa nje ya uwanja wakati wa mechi ya Kombe la Mfalme, baada ya kumwakia mwamuzi kabla ya kufungiwa tena wakati wa michuano ya Klabu Bingwa Ulaya.

Mbali na kufungiwa, kocha huyo alilimwa faini baada ya kupatikana na hatia kuhusu kadi mbili nyekundu walizooneshwa wachezaji wake, wakati wa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya iliyofanyika mwezi uliopita dhidi ya Ajax.

Katika mechi ya juzi dhidi ya Sevilla, Carvalho alilimwa kadi ya pili ya njano dakika ya 63, baada ya kugongana vichwa na mchezaji Alvaro Negredo, wakati wakirukia mpira wa juu.

Licha ya timu hiyo kubaki na wachezaji kumi mchezaji, Angel Di Maria alifanikiwa kuipatia timu hiyo bao la ushindi, dakika za mwisho na kuihakikishia Real Madrid kubaki nyuma kwa pointi mbili dhidi ya vinara wa ligi hiyo Barcelona.

No comments:

Post a Comment