21 December 2010

Mahabusu wagoma kushuka ndani ya gari

Na Rehema Maigala

MAHABUSU 20 waliofikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni jana asubuhi waligoma kushuka kutoka kwenye basi la mahabusu ikiwa ni ishara ya kuonesha kuchoshwa na vitendo vya mashahidi wa upande wa mashitaka kutokufika mahakamani
pamoja na kubambikiwa kesi za mauaji  hali inayosababisha kesi zao kuchelewa kusikilizwa.

Gazeti hili lilishuhudia tukio hilo nyakati za saa 2 asubuhi ambapo walikuwa kwenye gari namba STK 5829ambapo kilio chao kilikuwa ni kuchoshwa na kesi na kuchukua muda mrefu.

Mahabusu hao, ambao ni zaidi ya 20 ambao wanatoka katika mahabusu ya Keko, wengi wao wanakabiliwa na kesi za mauaji na wizi wa kutumia silaha.

"Tumechoshwa na sheria ya Tanzania tunaona ni bora kugoma kuliko kuingia Mahakamani ambapo hakuna kitu chochote kinachoendelea kila siku tunaambiwa upelelezi haujakamilika na hata wale ambao kesi zao zipo katika ushahidi, mashahidi hawafiki mahakamani kwa sababu zisizoeleweka," walilalamika mahabusu hao walipokuwa ndani ya basi .Hata hivyo washitakiwa hao walisema kuwa wanahitaji kumuona Waziri wa Sheria na Katiba, Bi. Celina Kombani ili wamueleze shida zao zote juu ya yao .

Naye, Mfawidhi wa Mahakama hiyo Bw. Kwey Lusemwa alisema kuwa mahabusu hao wamegoma kwa sababu wanahitaji sheria ifuate mkondo wake .

Wanadai kuwa wamechoshwa na ucheleweshwaji wa kesi hizo kwani wana miaka mingi kesi zao hazijasikilizwa na pia wanasema kuwa kesi nyingi walizonazo hasa za mauaji ni za kubambikizwa.

No comments:

Post a Comment