21 December 2010

CHADEMA kuchagua 'meya' wao Arusha

Na Glory Mhiliwa, Arusha

MADIWANI wa Manispaa ya Arusha kupitia CHADEMA wanadaiwa kufanya mpango wa kumchagua meya wao huku wakijiandaa kwenda mahakamani kupinga uchaguzi uliofanywa na wenzao wa vyama vya CCM na TLP.Hatua hiyo
inadaiwa inatokana na madiwani hao kudai kuwa uchaguzi wa meya na naibu wake ambao ulishikisha vyama hivyo ulikuwa batili kwa kuwa ulikiuka kanuni.

Mbunge wa Arusha Mjini, Bw. Godbless Lema alikaririwa juzi akisema kuwa watachagua meya wao kwa kuwa hawamtambui yule aliyechaguliwa na madiwani wa CCM peke yao.
  
Kiongozi mmoja wa CHADEMA, Bw. John Bayo, alisema kuwa kukamatwa kwa mbunge huyo wiki iliyopita kuwekwa ndani, kisha jioni kutolewa na kulazwa kwa muda hospitali ya Mkoa Mount Meru, kumewapa nguvu zaidi ya kufuatilia kwa karibu uvunjaji wa sheria.
  
Alisema kuwa wanatambua wazi kuna vitu vingi vilihusika katika kuvunja sheria siku ya uchaguzi, ikiwa na kuita kikao cha siri kwa wanachama wa CCM na baadaye diwani mmoja wa TLP kuungana nao.
  
“Kimsingi, tunasema kuwa hatuna utata na meya, isipokuwa uteuzi huo umefanywa kihuni bila kufuata sheria ya kuwa lazima kuwe na wajumbe theluthi ya mbili ya wapiga kura,” alisema Bayo na kuongeza:
Haiwezekani Meya wa Jiji la Arusha achaguliwe na mbunge viti maalum wa Tanga, kisha uitwe uchaguzi halali wakati ni uchakachuaji wa sheria,alisisitiza Bw. Bayo.
  
Lakini Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha, Bw. Estomiah Changah, alisema kuwa anachokifahamu, kikao hicho kilikuwa halali na kilifuata sheria na taratibu za Halmashauri.
  
Alisema kuwa sheria ilimruhusu kuwa wajumbe wakifika nusu ya wapiga kura ruksa kufanya uchaguzi, ambapo wapiga kura wote ni 31 na wao CCM na mjumbe mmoja wa TLP walikuwa 17 ambao wamepita nusu ya wapiga kura.
  
Kuhusu malalamiko ya mbunge wa kutoka Tanga, Bi. Mary Chatanda, Mkurugenzi alisema ni mbunge halali aliyeidhinishwa kwa barua yenye kumbukumbu namba CEB.77/155/01/79, ambayo ilitoka kwa Naibu Katibu wa Bunge
ambaye ni Eliakim Mrema.
Barua hii ilimruhusu Chatanda kushiriki uchaguzi pamoja na mbunge wa CHADEMA, Bi. Rehema Mngodo ambaye hajaapishwa naye aliruhusiwa kufanya uchaguzi huo,” alisema.

2 comments:

  1. Nyie majira kama mtaacha kuandika habari za kweli zinazohusu jamii na siasa kwa kuegemea chama tawala na kuficha habari zinazoihusu ccm, tutawagomea kusoma magazeti yenu, maana mnaandika habri za upande mmoja....mfuasi wa chadema arusha. acheni habari za upendeleo, mnaharibu aaluma yenu, igeni wenzenu wa mwananchi wanauza sana gazeti lao kwa kuwa wazi.

    ReplyDelete
  2. jamani majira hivi siku hizi mmenunuliwa na mafisadi?
    mbona kama you are defending something since election was over.,ehee.!embu jirekebisheni msije mkawa kama rai na mtanzania.Tanzanian people need journalists who are open .ni hayo tukutoka kwa mwanachama mfu wa ccm arusha.

    ReplyDelete