31 December 2010

Ancelotti adai kupumua

LONDON, England

KOCHA Carlo Ancelotti, amekiri akisema kwamba ni faraja kubwa kwake kurejea tena katika njia ya ushindi, baada ya Chelsea kuondoka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bolton, usiku wa kuamkia jana.Hadi inapata ushindi huo, Blues ilikuwa
tayari imeshindwa mara sita kuondoka na ushindi, hali ambayo iliifanya kujikuta ikishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa nyuma kwa pointi saba kwa vinara wa ligi hiyo, Manchester United.

Kutokana na mwenendo huo mbaya, shinikizo pia lilikuwa limeongezeka kwa  Ancelotti, huku akikiri kuwa ushindi huo ambao timu hiyo iliupata usiku wa kuamkia jana kwenye uwanja wake wa Stamford Bridge, umemfanya apumue.Katika mchezo huo, Chelsea walionekana kuimarika zaidi baada ya kusuasua kwa muda hususan baada ya Florent Malouda, kupachika bao hilo.

Ushindi huo umewafanya warejee tena kwenye kundi la timu nne bora na kocha  Ancelotti, anajivunia kikosi chake kurejea kwenye mstari.
"Tunahitaji kuendelea na ushindi huu," aliiambia Sky Sports."Ni muhimu kupata ushindi ili kusahau kipindi kibaya tulichomo na kwa sasa tunaweza kujiamini zaidi kipindi kijacho," aliongeza.

Alisema kipindi cha kwanza timu yake ilicheza vibaya na walifanya mashambulizi kidogo ya kutisha, lakini walikuwa wakitaka kushinda na kipindi cha pili ndipo wakacheza vizuri na kufanikiwa kupata ushindi huo.

No comments:

Post a Comment