31 December 2010

AC Milan yatangaza dau la Ronaldinho

MILAN, Italia

TIMU ya AC Milan, imetangaza dau la euro milioni 8 ili iweze kumuachia nyota wake Ronaldinho.Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30, raia wa Brazil kwa sasa yupo mwaka wa mwisho katika mkataba wake na vinara hao wa
soka nchini Italia.

Klabu yake ya zamani ya Gremio, tayari imeshaelezea nia ya kumrejesha nyumbani mchezaji huyo, ili aweze kumalizia kazi yake wakati wa usajili wa dirisha dogo litakapofunguliwa kesho na klabu hiyo, inaamini kuwa huenda ikampata bure mchezaji huyo bora wa zamani wa Dunia.

Awali baada ya kukutana na wakala wa mchezaji huyo, AC Milan iliamua kuwa suala hilo halitakuwa na tatizo.Makamu wa Rais wa AC Milan, Adriano Galliani alisema jana kupitia tovuti ya soka nchini Italia akisema kuwa yeyote ambaye atamuhitaji, Ronaldinho lazima awe tayari kutoa euro milioni 8.

Habari hizo pia zinadaiwa kuvishtua vigogo vya soka nchini, Brazil kama Palmeiras na Flamengo, ambavyo vilikuwa vinaangalia uwezekano wa kuingia mkataba na mchezaji huyo kwa kusaidiwa na wafadhili.

Bei hiyo inaelezewa kuwa inaweza kumfanya mchezaji huyo kuendelea kucheza soka Ulaya na timu ya Liverpool, ndiyo inayotajwa kummezea mate nyota huyo huku timu ya Los Angeles Galaxy, ikifuatilia hali hiyo.

No comments:

Post a Comment