30 December 2010

Mzee wa Vijisenti hukumu ya 'furaha'

*Atamba 'pigeni picha mimi Rais wa Afrika'

Na Rehema Maigala
UMATI mkubwa ulifurika jana katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kusikiliza hukumu dhidi ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Bw. Andrew Chenge na kuhitimishwa kwa ndugu na marafiki kufurahia maamuzi.Baada ya hukumu kusomwa na
kumpa unafuu wa kuchagua kati baina ya kifungo na faini, sehemu ya umati huo, wengi wakiwa ndugu, jamaa na marafiki wa mshtakiwa, walionesha dhahiri kuwa wasiwasi ulitoweka kwenye nyuso zao na ghafla wakaonekana wenye furaha na bashasha.

Wakati akiingia mahakamani, Bw. Chenge alisikika akiwaeleza waandishi wa habari waliokuwa wakimpiga picha kuwa, "Nipigeni picha mimi ndiye rais wa Afrika" na wakati akiondoka aliwabeza waandishi hao, akisema nipigeni picha mara ya mwisho, hapa hamtaniona tena".

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kinondoni, Kwey Rusema alianza kusoma hukumu hiyo asubuhi saa 3:30 huku kila mtu akiwa kimya, akisubiri hatma ya Bw. Chenge aliyeshtakiwa kwa kusababisha vifo vya wanawake wawili, kuendesha gari lisilokuwa na bima, na kuendesha bila uangalifu.

Wakati hukumu ikisomwa, Bw. Chenge, mkewe na ndugu zake waliokuwepo mahakamni walionekana sura zao zikiwa na simazi, na hasa baada ya hakimu kutamka kuwa 'mshtakiwa ameingia hatiani kwa makosa yote manne'.Makosa hayo ni kuendesha gari lisilo na bima, kusababisha kifo cha Victoria George, kusababisha kifo cha Beatrice Costantine na kuendesha gari kizembe.

Baadhi ya ndugu hao walionekana kuinama chini na kuanza kusali kwa imani yao, ili mradi tu hakimu asitamke adhabu kubwa kwa ndugu yao.Kabla ya hakimu kutamka adhabu hiyo, Bw. Chenge alitakiwa kujitetea, na kazi hiyo ilifanywa na wakili wake, Bw. Simon Mponda, akiitaka mahakama impunguzie adhabu mteja wake, kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kufanya kosa kama hilo.

"Naomba mahakama impunguzie adhabu mshtakiwa, kwanza ni kiongozi anategemewa na umma wa Watanzania na pia ana majukumu mengi, hivyo tunaiomba mahakama impunguzie adhabu ili aendelee na majukumu yake ya kutetea Taifa la Tanzania," alisema Mponda. Pamoja na maombi hayo, hakimu aliamua kutoa adhabu ya ama kifungo au faini ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia ya kuendesha magari bila uangalifu, na wengine wenye tabia ya kuendesha magari bila ya kuwa na bima.

Katika mashtaka ya kwanza na ya pili, ya kuendesha gari bila uangalifu na la kuendesha gari bila bima, Bw. Chenge alihukumiwa ama kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kila kosa, au kulipa faini ya 250,000 kwa kila moja.Katika mashtaka ya tatu na nne, ya kusababisha kifo cha Victoria George; na jingine la kusababisha kifo cha Beatrice Constantine, mshtakiwa alihukumiwa ama kutumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kila kosa au kulipa faini ya 100,000 kila moja.

Kwa kuwa adhabu zote hizo zinakwenda kwa pamoja, kama Bw. Chenge angeshindwa kulipa faini ya sh 700,000, angepelekwa jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja.Ukiacha kundi la ndugu na marafiki wa mtuhumiwa, watu wengine waliokuwa mahakamani waliondoka wakikosoa sheria zilizohusika katika shauri hilo, na wengine kuhusisha sheria hizo na mabadiliko ya katiba yanayopigiwa kelele.

"Jamani mambo gani haya binadamu wawili wamepoteza maisha yao, leo hii mtu mwenye pesa zake anatakiwa kulipa faini ya 700,000/- huu ni uonevu mtupu kwa nini iwe hivi?" alihoji mwanamume mmoja ambaye jina lake halikupatikana.

"Mbona mimi nilikuwa na kesi ya ndugu yangu tena alimgonga mtu mmoja na kufa, lakini alihukumiwa kifungo cha miaka minne jela au faini ya sh. milioni moja, sasa iweje kiongozi kama huyu apewe adhabu ndogo hiyo," mwingine alidakia.Dakika 15 baada ya hukumu hiyo kusomwa, Bw. Chenge alionekana akipanda gari aina ya Toyota Land Cruser T. 276 AQC huku akipongezwa na mke na ndugu zake kwa furaha.

Katika kesi hiyo mshitakiwa huyo anadaiwa kushindwa kuchukua tahadhari barabarani na kuigonga pipikipiki na magurudumu matatu aina ya bajaji yenye namba za usajili T. 736 AXC na kusababisha vifo vya wanawake hao.

Bw. Chenge alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Machi 30, 2009 akikabiliwa na mashtaka matatu, kabla ya kuongezewa moja na kuwa manne.Ilidaiwa kuwa Machi 27, 2009 katika Barabara ya Haile Selassie Wilaya ya Kinondoni akiwa na gari lenye namba za usajili T. 512 ACE, bila bima wala uangalifu, Bw. Chenge alisababisha vifo vya wanawake hao.

26 comments:

  1. Hukumu ya namna hii niliitegemea. Mbona Deus Mally aliyeendesha gari kwa uzembe na kusababisha kifo cha Chacha Wangwe alifungwa miaka 3? Hii nchi ina uonevu sana, mahakama haitendi haki na kuna double standards. Haki ya nani siku moja tutaingia msituni tuwang'oe mafisadi wote tumechoka atii. Wewe mzee wa Vijisenti Mungu atakuhukumu kama alivyomuhukumu Ditopile na haki ya Mwadamu haipotei.

    ReplyDelete
  2. mie sio mwanasheria ila nilitaka kufahamu, ki ukweli Chenge ni mkosaji na amekutwa na jinai na ametumikia kosa/adhabu na ni bahati yake maana adhabu ya kulipa faini ya shs.700,000 haikuwa ngumu kwake and ndio aliyotekeleza. swali langu .....yes chenge ni mharifu na ana adhabu- je bado anastahili kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo lake?maana anakosa la jinai?

    ReplyDelete
  3. mimi ushauri wangu ni kuwa hukumu ya faini iendane na kipato cha mtu kama nchi zilizoendelea zinavyofanya sio laki 7 kwa mtu mwenye vijisenti kama yeye, na je hawa waliopotezewa maisha yao wamefikiriwa kwa namna yoyote ile?

    ReplyDelete
  4. Mzee wa vijisenti amepatiakana na kosa lajinai je bado anastahili kuendelea kuwa kiongozi wa wananchi? Naomba msaada kwenye tuta!

    ReplyDelete
  5. Anonymous, unataka msaada kwenye tuta? Huu hapa! Kisheria, hastahili. Ana kosa, tena basi la jinai. Ameshahukumiwa jela au faini. Anakosa sifa za kuwa mbunge. Tume, haraka, itisheni uchaguzi mdogo.

    ReplyDelete
  6. Lo wewe hakimu, mimi si mwanasheria lakini kulingana na aibu uliyo itangazia dunia nadhani ujistafishe huwezi kutoa hukumu ya mtu aliye uwa kwa hivi vijisenti, wewe hujuwi kufiwa wala hujawahi kufiwa na wala hutafiwa, kwani hukumu hii ni ya mtu aliye uwa mbuzi tena mbuzi mmoja nasi binadamu wawili. acheni kuidharirisha nnchi kwani kutoa hukumu hii hadharani ni aibu tupu, huu ni mchezo wala si kazi, mtu kauwa unampa faini ya gharama ambayo hikutosha hata uendeshaji wa mazishi kwaninii hapana ajali zisizidi nnchin kama shitaka la kuuwa linalipwa kwabei ya kununulia vifaranga vya kuku? viongozi ndiyomnahamasisha ajali Tanzania kwani mnawatetea kwa kuwatoza faini kidogo. au labda hivyo vijipesa ni kiinimachot chenge katole faini mlangowa nyuma? haiwezekani kwa mtu kuamini kuwa mauwaji ya watu wawili yamemalizika kwa fainiya viisentii wapina wapi. Tusidanganyane. BABA WATAIFA TUONEE HURUMA TUNAZIDI KUANGAMIA WATANZANIA HATUA TENA MTETEZI

    ReplyDelete
  7. SASA NGOJA TENA TUONE TUME ITAFANYAJE KWANIKAMA HUYU HAKIMU KASAPOTI MAUWAJI KWA KUTOA HUKUMU YA KIINI MACHONA TUME JE LITATENDA HAKI, WATANZANIA TUAJUA FIKA KUWA TUME HAITATENDA HAKI KWANI HATA MAHAKAMA HAIKUTENDA HAKI TANZANIA UPUUZI MTUPI

    ReplyDelete
  8. Mahakama za Tanzania zinaubabaishaji sana. Zinapopelekewa kesi za viongozi basi wanatetemeka na kuanza kutafuta namna ya kuwanusuru kwa kutumia mianya ya kisheria.

    Lakini kama ni Kabwela wanatafuta namna ya kukumaliza kabisa ili ukome na usionekane katika uso wa dunia hii.

    Sijui ni kwa sababu mwenye nacho ataongezewa? Lakini mkumbuke kuwa muongo na mlozi wote ni watu wa kuchomwa. Waamuzi na watuhumiwa wa sampuli za Chenge Mungu anawaona, mwisho wenu si miaka 100. Ni wazi kuwa kila nafsi itaionja mauti. Kama mahakama imekupendelea, Mungu atachukua jukumu lake. Poleni wana ndugu, ndio athali za kuzaliwa Tanzania. Hatuna namna ya kufanya zaidi ya kuwashauri mkate rufaa. Mungu awape uvumilivu naye atawalipia.

    ReplyDelete
  9. na mimi nahitaji msaada kwenye tuta......ni advantage amepona kwenda jera, ila amechafuka maana ni mharifu na amevaa vazi la njano kama wengine waliyopo segerea mbalimbali hapa TZ (amenunua vazi kwa 700,000) ni yupo kifungoni tu!sasa mchakato wa kumtoa katika uwakilishi unakuwaje?maana ana jinai ni mharifu na hana sifa ya kuwa mwakilishi - mbuge!si ametoka automatic katika siasa? please na mie nahitaji msaada kwenye tuta

    ReplyDelete
  10. Kweli hukumu hii in utata! Haiwezikani Kosa kama hilo alilifanya Deus Malya, kaichezea jela miaka 3, kwa nini the same should not apply to Chenge! Hivi Jamuhuri imeridhika? hakuna ku-appeal? au ndio hiyo appeal itayeyuka kama ya kina Zombe, maana Kikwete alinadi kuwa Jamuhuri haikuridhi na wata-appeal lakin kimya hadi leo na miuaji inatamba tu mitaani! Kweli sisi ni wadangayika kuna haja kweli ya kubadili Katiba vifungu kama hivi vibadilishwe kabisa

    ReplyDelete
  11. mimi sidhani kama huyu hakimu alikuwa akiifikiria hii kesi kisheria na ki binadamu,kwani maisha ya hawa marehemu wawili yanaweza kuwa sawa na dollar us 1000 hii popote dunia hakuna atakae kuwa na imani na huyu hakimu wetu.Isipokuwa tayari tanzania imetawaliwa na ufisadi basi tuchunge hatua zetu,kwani tanzania uhai wako ni laki 350,000 Tsh,Je mtoto wa huyo chenge pia uhai wake ni 350,000???????
    Mungu ibariki tanzania na uwalaaani wote wale wanao hukumu uhai wa wenzao bila kujali kuwa watakufa.

    Inshaallah,
    Eimeeen.

    ReplyDelete
  12. Mimi ni mtanzania ninayeishi U.S.A.Kila ninaposikia mambo ya kipuuzi kama haya uwa naongeza miaka 10 mbele ya mimi kuwepo hapa.
    Hivi waliogonwa wangekuwa dada wa Kikwete au Shein hukumu ingekuwa hivyo hivyo.
    Sioni sababu ya Kikwete kuwa mswaliina au Sheini kuwa hivyo ,wana mwaswali mazito kwa mola wao.
    Hiyo inchi inatisha!!!!

    ReplyDelete
  13. Nadhani hapa tulaumu sheria zetu na wala tusimulaumu chenge wala hakimu. Hakimu ametoa hukumu kwa mjibu wa sheria kama alimpa adhabu ya chini au ya juu zaidi hiyo ni juu ya hakimu mhusika kulingana na uzito wa ushahidi. Mie nadhani maoni yanayotolewa ni ya kiushabiki zaidi kuliko uhalisia. Kwani Chenge ametiwa hatiani kwa traffic offense na si jinai (criminal offense). Kwa hiyo hii haimwathiri katika nafasi za uongozi alizonazo. Pia maoni mengine yamelinganisha kosa la Mallya aliyesababisha kifo cha marehemu Wangwe, huyu Mallya hakuwa na leseni ni tofauti na Chenge ambaye alikuwa hana bima. Bima na leseni ni vitu viwili tofauti, na kwa vyovyote vile uzito wa adhabu yake nao ni tofauti. Kisheria ndivyo ilivyo. Mbona watu hawaongelei kosa kama hilo la Jaji Rugazia aliyesababisha kisho cha mtu pale victoria/mikocheni lakini polisi hawajaipeleka hiyo kesi hata mahakamani? Haya ni mambo ambayo inabidi yarekebishwe kisheria lakini kumbuka watu wa kawaida pia wataumia zaidi iwapo watapatwa na kosa kama hili na adhabu ikawa beyond their reach.

    ReplyDelete
  14. Kwa makosa hayo nategemea vyeo vyote ataachia. Ingekuwa ulaya angesha lazimika jiuzulu siku nyiiiingi.

    ReplyDelete
  15. Tusilete ujinga wa siasa kwenye kesi,ya Malya hamuyajui ni MAFIASM ya wachaga alikuwa naye aondoke. turudi kwenye kesi,mimi nasema hata siku moja sitamshauri mwanangu aingie kwenye taaluma ya sheria ili awe hakimu,jaji au wakili hawa hawana dini,na bila shaka wengi wataenda motoni,labda kwa wale wenzetu wanaoungama kwa padri au askofu watasamehewa,lakini kwa dini zingine hawa ni wa motoni moja kwa moja,wanadhulumu haki za watu sana kwa ajili ya pesa,hiyo ya Chenge ni trela tu. Hawa mawakili kwa kushirikiana na makarani ndio wavurugaji wakubwa wa kesi hapo mahakamani. hata Mungu huwaadhibu hapahapa duniani na wanakufa vifo vya mateso sana kutokana dhuluma zao.Wanapata advantage ya uoza wa usimamizi katika nchi yetu ndio wanajifanyia wanavyotaka NYIE DHULUMUNI HAKI ZA WANYONGE LAKINI HUKO MBELE YA HAKI MTAKIONA

    ReplyDelete
  16. Sizifahamu sheria vizuri lakini nadhani jamaa wa marehemu wana uwezo wa kufungua civil case na kutaka kulipwa fidia ya damu iliopotea. Msingi wa mahakama huru zote duniani unakwenda na balance of evidence.

    Kwa wale waliohukumiwa kabla, nadhani mahakama pamoja na mambo mengine hufuata 'precedent judgement' katika kuhukumu kesi zinazofanana.

    Kwa vile ushahidi wa vifo na uzembe upo katika kesi hii, mawakili wa wafiwa wanaweza wakadai kiwango kikubwa, lets say Shs 200 million per deceased.

    Lengo hapa sio fedha bali ni kuweka msingi madhubuti wa sheria na kuheshimu thamani ya roho ya mwanadamu. Hii pia itapelekea madereva nao kuwa waangalifu na kutii mali na roho za raia.

    ReplyDelete
  17. Wananchi msilalamike sana. Hata nyie hamtendi haki barabarani. Kijana akizomewa sokoni kaiba simu ya shilingi 30000,- mko tayari kumpiga mpaka afe.Huku mkifurahia kutenda haki!! Au kuua Albino mkitafuta utajiri!!Acheni unafiki. Nchi nzima ni mbovu. Kuanzia juu mpaka chini.

    ReplyDelete
  18. kwanini asipewe adhabu ya community service kama masaa mia mbili, hapa jeuri ingemtoka kwani angepigwa picha kuzidi rais wa Africa, na kama hangefanya hivyo ndo angehukumiwa kifungo.

    ReplyDelete
  19. Wewe uliye USA kama kweli unavyosema tunakuambia Tanzania itajengwa na Watanzania walio ndani na walio wazalendo kwa nchi yao,usitufanye sisi ni wajinga,huna sababu ya kumtaja mtoto wa Kikwete wala Shein kwenye masuala kama haya,huo ni ujinga. Hapa Tz mwenye pesa ndio mwenye haki,au uwe mwanasiasa maarufu. hivi hujui kuna mtoto wa Mzee Mtei alikamatwa Babati na magari ya wizi? yaliishia wapi? licha ya kupelekwa mahakamani? hivi hujui mgombea urais wa Chadema Dr Slaa alipora mke wa mtu na juu ya kwamba ushahidi wote ulipelekwa mahakamani lakini bado aliendelea kutesa naye kwenye viwanja? ingekuwa mlalahoi kama mimi saa hizi ningeozea jela,hapa bongo haki ni kwa mwenyenacho. Lakini hata huko ulipo usidhani haki imekuja hivihivi kwa muda mfupi,soma historia ya Wamerakani weusi uone nao walianza lini mapambano ya kudai haki,haya mambo hayaji kwa mara moja,wenzetu waliweza kwa karne nyingi tu,wewe angalia hapa kwetu wanaharakati wengi wa haki za binaadamu na makanisa na misikiti walipanua midomo sana kuropoka wakati wa uchaguzi mkuu kila mmoja kwa interest zake lakini kwa suala kama hili wapo kimya.

    ReplyDelete
  20. huku ukiendesha gari bila bima ukikamwata hata kama hujafanya kosa ni faini isiyopungua$500.ukigonga mtu hata hakimu hakuangalii usoni unamiaka 25 jela then utaangalia jinsi ya kukata rufaa kivyako.hayo ndio maajabu ya tanzania ni oonezi mtupu.hata huruma hawana.

    ReplyDelete
  21. Kweli hakimu kakosea. Mwanzo, ajali haina kinga lakini ni sharti mwenye gari awe na bima ili ajali ikitokea wanaoathirika wapewe ridhaa. Na kiwango cha ridhaa inategemea mambo mengi kama umri,mapato, ujuzi n.k. ya walioathirika. Hoja kwamba mshtakiwa ni kiongozi badala ya kumtetea Chenge iko dhidi yake: kwani ikiwa ni kiongozi lazima aonyeshe mfano mzuri kwa kutii sheria - kwa kuwa na bima. Hilo ndilo kosa kubwa lakini mtu yeyote anaweza kuingia katika ajali.Kila siku twasikia habari kwamba baba na jamii yake wamefariki kwenye ajali ambapo baba ndiye dereva. Sielewi huyu hakimu alitumia sheria gani kwa kutompiga faini kubwa huyo mshatikiwa na kushindwa kuwapa ridhaa nzito jamii ya wanawake wawili walio kufa.Pana haja ya mawakili watanzania kukata rufaa hasa kwa upande wa ridhaa.

    ReplyDelete
  22. Kwa vyevyote vile Chenge achengeshwe. Alipe raia aliowaua Haki kamili. Kama hana Bima, basi kiwango maximum cha coverage ya Bima kwa kupoteza maisha ya abiria alipe hicho kiwango kamili kwa kila mmoja.

    Chenge mwenyewe, iwapo hutolipa hawa wazee wanafmilia, nakuhakikishia UTAANGAMIA, Kama huamini subiri basi! Unadhani unachezea maisha ya mwanadamu kama sungura??

    Chenge Kalipe hela kamili, usijibabaishe hapa, ebo!

    ReplyDelete
  23. sheria kwa nchi zetu za dunia ya tano ni kwa wale WASIO NA MAJINA , WASIO NA HELA , NA WASIO NA NDUGU WA KUWASAIDIA, hapo ni lazima ukumbane na sheria, lini hapa kwetu ulisikia mtu mwenye sifa hizo juu anapamabana na sheria na akashindwa.? WACHA WATUONEE TU HAKI YETU IKO KWA MUNGU

    ReplyDelete
  24. Kwani si tunajua kuzindikwa ni nini jamani?? Baba yetu, Baba wa taifa, Mungu wa Waafrika - katuachia wanafunzi wake ambao wamehitimu kabisa. Aliwasomesha Uongo, Ujanja, wizi, kamata kamata, tisha tisha tia jela n.k. Kwa hio unapoona ofisi imewekwa picha ya "Baba wa Taifa", na unapoona mtu anajinasibu na "baba wa Taifa" jua apo ipo kazi. Maana mtu hata ile luga inabadilika kukulaza wewe - unazindikwa tena apo! Wache watumalize na dhuluma zao. Mungu yupo tu.

    ReplyDelete
  25. Kweli Tanzania ni nchi masikini mno,maana tunaumasikini mpaka wa wanasheria.mi nafikiri aliye hukumu kesi ya chenge hana taaluma ya sheria haiwezekani mtu amepatikana na kosa tena la mauaji halafu anapewa hukumu ya kipuuzi hivyo.ila mwenyezi mungu huwa anahukumu hapa hapa mlimwona DITOPILE? tumsubiri na chenge

    ReplyDelete
  26. Watz wametoa comments zao, hisia kutoka mioyoni mwao. Hii inaonesha jinsi walivyo na uchungu na watanzania wenzao waliopoteza maisha kwa ajali ya kizembe iliyosababishwa na Mkubwa fulani.

    Ni haki yenu au yetu sote kuonesha hisia hizo. Ni kweli sheria imetoa haki yake katika kosa hilo, lakini tukumbuke hakimu amefuata miongozo ya sheria na Chenge kama Binadamu mwingine naye atakuwa amejitetea alivyoweza mpaka kufikia hapo.

    Mi nakubaliana kuwa yapo mapungufu ya kisheria katika kosa kama la Chenge kwa sababu kama fidia ambayo marehemu walitakiwa kupata, dereva wa Bajaj, na mmliki wake toka kwa Msababishaji ajali kama angekuwa na Bima imekosekana.

    Haki ya Compersation yao imekosekana na kwa sababu marehemu hao hawawezi tena kuongea ndiyo kabisaa!! Haki yao imenyang'anywa kisheria. Sheria hii ina mapungufu na si kwa utendaji wa hakimu, mahakama wala mtuhumiwa mwenyewe bali ksiheria, hivyo inastahili marekebisho ili siku nyingine isije ikatokea kama hivi iivyotokea.

    Sasa kama suala la haki hiyo kukosekana na hakuna sheria inayotuongoza katika hilo ni vizuri tuyatazae mapungufu hayo na turekebishe sheria hii kama tulivyosema, lakini pia Chenge kibinadamu hatuwezi kumhukumu mara mbili kwamba awalipe marehemu wakati tayari keshahukumiwa.

    Kibinadamu namwomba Chenge asome alama hizi za nyakati akawaombe radhi wafiwa na hata ikibidi asikie kilio cha Watanzania awapatie kifuta machozi hata kama ndugu wa marehemu hawaatahitaji kifuta machozi hicho. Ila awabembeleze wakipokee kiweze kuwasaidia japo kidogo wategemezi wote wa marehemu hao.

    Tanzania kwa hekima tutafika!

    ReplyDelete