Na Mwajuma Juma, Zanzibar
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imefanya uteuzi wa wajumbe 20 wa Baraza la Wawakilishi kupitia viti maalumu, ambao wataingia katika baraza hilo linalotarajiwa kuanza
kesho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Afisa Uhusiano wa ZEC, Bw. Idrissa Haji Jecha wajumbe 11 walituliwa
kutoka CCM na tisa kutoka Chama Cha Wananchi (CUF).
"Uteuzi wa wajumbe hao umefanyika kutokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 31, mwaka huu ambapo CCM ilishinda majimbo 28 na CUF majimbo 22, hivyo kuzingatia uwiano huo wajumbe hao wameteuliwa.
Wajumbe hao walioteuliwa kwa upande wa CCM Bi. Salma Mussa Bilali, Bi. Wanu Hafidh Ameir, Bi. Mwanaidi Kassim Mussa, Bi. Amina Iddi Mbarouk, Bi, Absha
Bakar Makame, Bi. Mgeni Hassan Juma, Bi. Shadya Mohammed Suleiman, na Bi. Bihindi Hamad Khamis.
Wengine ni, Bi. Raya Suleiman Hamad, Bi. Viwe Khamis Abdallah na Bi. Panya Ali Abdallah.
Kwa upande wa chama cha Wananchi CUF ni Bi. Zahra Ali Hamad, Bi. Ashura Sharif Ali, Bi. Asha Abdu Haji, Bi. Mtumwa Kheri Mbarak, Bi. Kazija Khamis Kona, Bi.
Mwajuma Faki Mdachi, Bi. Farida Amour Mohammed, Bi. Salama Mohammed Ali, Bi. Farida Amour Mohammed na Bi. Bimke Yussuf Hamad.
Uteuzi wa wajumbe hao umefanyika kufuatia masharti ya ibara ya 67 (1) ya katiba ya Zanzibar, ambayo inaeleza kuwa kutakuwa na wajumbe wa viti maalumu wa Baraza la Wawakilishi wanawake, sawa na asilimia 40 ya wajumbe wote wa kuchaguliwa katika majimbo.
Aidha katika ibara ndogo ya (2), inaeleza kuwa kila chama cha siasa kitakachoshinda zaidi ya asilimia kumi ya viti vya majimbo katika baraza hilo kitapendekeza majina ya wanachama wanawake kwa kuzingatia masharti ya
uwiano wa uwakilishi baina ya vyama vitakavyoshinda katika uchaguzi mkuu katika majimbo.
Hivyo baada ya tume kuridhika kuwa mwanamke aliyependekezwa ana sifa za kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi itamtangaza kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Wakati huo huo Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein amemteua Jaji Omar Othman Makungu kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee, uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa kifungu 55 (1) cha Katiba ya Zanzibar, ambacho kimempa rais mamlaka ya kufanya hivyo. Uteuzi huo ulianza jana.
No comments:
Post a Comment