08 November 2010

Kikwete atakiwa kuwatosa waliomwangusha.

Na Gladness Mboma

RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kuangalia uwezekano wa kupunguza ukubwa wa Serikali yake kwa kuweka watu makini, wazalendo na wachapa kazi na
wenye kusimamia haki ili aweze kutekeleza ahadi alizoahidi Watanzania na kufikia malengo.

Akizungumza na Majira kwa njia ya simu jana akiwa Unguja Zanzibar Mchungaji wa Kanisa la Pentekoste Evangelical  Church-PEC la Mjini Mbeya, Bw. William Mwamalanga alisema, Rais anatakiwa kutambua na kuwa na tahadhari kubwa na kundi lililojitokeza kutafuta vyeo badala ya kuwatumikia Watanzania na kuwaondoa katika umaskini.

Mchungaji Mwamalanga alisema kuwa kundi hilo halina upendo na Tanzania, bali linatafuta vyeo kwa gharama yoyote hata kwa kumwaga damu.

"Kundi hili linazuia watu wazuri wasipate madaraka, na linafanya juu chini kuhakikisha linakuwa na nguvu na kufanikisha malengo yake na kundi hili liko ndani ya CCM hivyo wakati wa kuteua anatakiwa kuwa makini," alisema na kuongeza.

"Ninapenda Rais atambue kwamba watu hao wako kinyume kabisa na yeye na ndio maana CCM katika kipindi cha kampeni walikuwa na hali ngumu ya kuwanadi viongozi wake, kama serikali inayokuja itakuwa kama ile iliyopita kwa kweli hakutakuwa na miujiza itakayofanyika kutekeleza ahadi,"alisema.

Alimtaka Rais Kikwete kutosita kuchagua watu kutoka vyama vya upinzani ambao wana sifa na uwezo wa uongozi ili waweze kumsaidia.

Mchungaji Mwamalanga alimsisitiza Rais Kikwete kufukia mashimo kwa kupunguza ukubwa wa serikali na asichague watu wanaolala usingizi ikiwa ni pamoja na kuepukana na watu wanafiki katika siasa waliomdanganya hasa kipindi kilichopita.

Alisema kuwa mwaka 2005 Watanzania walikuwa na matumaini makubwa sana kwake, lakini baadaye alikosa vitendea kazi, akaweka wanafiki wengi waliobaki kula tu bila kufanya kazi.

"Niliona uchungu sana wakati wa kampeni kwani watu  walikuwa na hasira na yote hayo yalikuwa yakielekezwa kwa Rais Kikwete hayo yote yanatokana na watendaji wake wote kutotekeleza majukumu aliyokuwa amewapa,"alisema.

Alisema kuwa baadhi ya Mawaziri wake hakuna kitu walichokuwa wakikifanya na badala yake walikuwa wanajipangia safari za kwenda Ulaya na kumtaka kutowarejesha tena madarakani mawaziri ambao walikataliwa na wananchi katika kura za maoni na hata kwenye ubunge.

Mbali na hayo alimtaka Rais Kikwete kutokubali watu kumwingilia na wala kupokea ushauri utakaompotosha  kama kipindi cha awamu iliyopita.

Alisema kwa upande wa sekta ya madini,Wizara ya Maliasili na Utalii inahitaji Waziri na Katibu Mkuu mwadilifu na mtu makini na mchapakazi atakayeweza kusimamia vyema wizara hiyo iliyokumbwa na majangili ambao wamegeuza wizara hiyo kama benki yao isiyokuwa na riba kwao.

Alisema kuwa kwa upande wa uwekezaji, umefika wakati Rais Kikwete kuangalia eneo la ardhi, kwani kuna watu wanatumia uwekezaji kwa manufaa yao wenyewe.

Alisema kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kugeuza sura ya uwekezaji iwe na tija na kuondokana na uwekezaji wa unyonyaji ambao hauna manufaa kwa Watanzania.

Mchungaji Mwamalanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Haki za Jamii Nchini na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuhifadhi Misitu na Mazingira Tanzania (MRECA) Mbeya amewataka viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi wakati wote.

3 comments:

  1. UMAKINI WA KUPATA WATENDA KAZI WAZURI UNAHITAJI HEKIMA, UJASIRI, NA KUJUA UNATAKA KUWAFANYIA WAPIGA KURA. KIKWETA LAZIME IFIKE MAHALI ATAFAKARI KWANZA KAMA ANATAKA KAFANYA KAZI AU ANATAKA USANII. KUWAPA NAFASI WASEMWAO NI MAFISADI. NI KUJILETEA SHIDA TU. SISI HATUTASEMA MAFISADI WAMESHINDWA KAZI BALI RAISI KIKWETE HAJUI KAZI. NAMUOMBEA KIPINDI KIJACHO MUNGU AMPE UJASIRI NA HEKIMA WA KUAMUA MAMBO MAGUMU. ISIJE IKAFIKA WAKATI AMBAPO YEYE NA FAMILIA YAKE WATANYANYAPALIWA:

    ReplyDelete
  2. ajisafishe kwanz yeye

    ReplyDelete
  3. Hakuna lolote Kikwete atazidi kuteua washikaji zake tu mfano mzuri ni kuwa Rais atajuaje kuna mtu anafaa kuwa mkuu wa mkoa au wilaya?

    ReplyDelete