08 November 2010

Wanandoa wauawa kinyama Kahama.

Na Patrick Mabula, Kahama

WANANDOA wawili wameuawa kinyama kwa kucharangwa mapanga na watu wasiojulikana katika kijiji cha Segese, Kata ya Segese wilayani Kahama.
Walifikwa na mauaji hayo juzi saa mbili usiku wakiwa nyumbani kwao mara baada ya kumaliza kula chakula cha usiku.

Baada ya kumaliza kula chakula hicho, ghafla walivamiwa na watu wasiojulikana na kuwakata mapanga na kusababisha kufikwa na umaiti.

Wanandoa hao walitajwa kwa majina ya Bw. Mabula Kufinga (45) na mkewe Bi. Roda Cherehani (35).

Taarifa za awali zilizodhibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Daud Siasi zinatibitisha kuvamiwa kwa wanandoa hayo na watu wasiojulikana.

Kamanda Siasi alieleza kuwa, wauaji hao baada ya kufika nyumbani kwa wanandoa hao, waliwakuta wamemaliza kula
ndipo walipowaweka chini ya ulinzi na kuanza kuwashabulia kwa kuwakata mapanga hadi kufa.

Mashuhuda ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao walilieleza Majira kuwa, mauaji hao yalihusishwa na imani za kishirikina na kwamba walizoea kusikia mauaji hayo yametekelezwa kwa vikongwe pekee.

Polisi wilayani Kahama inawashikilia ndugu na jamaa wa marehemu na watu kadhaa kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.

1 comment:

  1. Hivi kwanini mtu anapouawa polisi wanawahi kuwakamata watu wasiohusika na kuwasumbua?

    Imefikia wakati sasa jeshi hilo wapate mafunzo ikiwezekana hata waende shule maana hana taaluma ya kutosha.

    ReplyDelete