08 November 2010

Watano wafa ajali ya boti.

Na Sammy Kisika, Sumbawanga

WATU watano wakiwemo watoto wanne wamekufa na wengine zaidi ya kumi wakihofiwa kufa maji ya baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama katika
Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa.

Habari za uhakika zilizothibitishwa na polisi mkoani
hapa, zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni katika maeneo ya kijiji cha Mkombe wakati Boti hiyo ilipokuwa ikitoka kijiji cha Kabwe kuelekea kijiji cha Kalila kilichopo Mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Bw. Isuto Mantage aliwataja waliokufa maji katika ajali hiyo kuwa ni  mtoto Emmanuel Makasi (1) mkazi wa Tunduma, mtoto Helena White (1) Mkazi wa kabwe, mtoto Korodina Tende (1), mtoto Modesta Mengo (6) na Apolinali Roman, maarufu kama Sungura (36) wote wakazi wa Kijiji cha Kalila.

Alisema boti hiyo ilikuwa imebeba watu wengi ambao walikuwa ni wafanyabiashara wa dagaa waliokuwa wakielekea katika kijiji hicho kwa lengo la kununua dagaa na samaki.

Kamanda huyo alisema kuwa watu 21 waliokolewa kutokana na jitihada za wavuvi waliokuwepo maeneo ya karibu  ambapo wanne hawajulikani walipo na wanahofiwa kufa
maji baada ya kuzama kwa boti hiyo. 

Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo Bw. Ramadhani alisema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya boti hiyo kupasuka na kuzama ikiwa safarini.

Aliongeza kuwa wakati wakiwa safarini ghafla boti hiyo inayokadiriwa kuwa na watu zaidi ya 36 ikiwa na mizigo ilipasuka na kuanza kuzama ambapo baadhi ya watu
walifanikiwa kuogelea hadi ufukweni na kuokoa maisha yao.

“Ilikuwa ajali mbaya Mwenyezi Mungu ametusadia sana wengine…mimi nilishikilia mbao za ile boti mpaka nilipopata msaada toka kwa wavuvi waliokuwa maeneo ya jirani na kutuokoa baadhi yetu hadi nchi kavu, tulikuwa wengi hivyo wengine wanahofiwa kufa,” alisema Bw. Ramadhani.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kabwe Bw. Asante Edward alisema kuwa ajali hiyo imesababisha simanzi kubwa katika kijiji cha Kabwe ambapo tangu jana shughuli zote za uvuvi zilisimama kijijini hapo na kuongeza  kuwa kazi ya kutafuta miili ya watu waliopoteza maisha ilifanywa hadi saa 2.00 usiku.

Kwa mijibu wa Kamanda Mantage, polisi wilaya Nkasi kwa kushirikiana wananchi wanaendelea kutafuta miili mingine ya watu wanaohofiwa kufa maji kwenye ajali hiyo, huku akitoa rai kwa wavuvi na wananchi wengine wa vijiji vya jirani kutoa taarifa iwapo miili ya watu hao itaonekana ikielea majini.

No comments:

Post a Comment