08 November 2010

Chenge amvaa Spika Sitta.

*Adai amejenga bunge la chuki, husuda, uzushi, kutoaminiana
*Adai aliliongoza bunge kwa nia ya kujitafutia umaarufu
*Asema bunge lililopita lilijaa majeruhi, yeye anakwenda kutibu
*Sitta asema hana cha kusema, wananchi wanajua ukweli wataamua


Na Tumaini Makene
MBUNGE mteule wa Jimbo la Bariadi Magharibi kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Andrew Chenge amemshambulia
spika wa zamani Samuel Sitta, akiweka wazi sababu zake za kuwania kiti cha uspika, ikiwamo wa kwenda kuondoa husuda, chuki, hasira, uzushi na kutibu majeraha na kutoaminiana miongoni mwa jamii, alivyodai vilivyojitokeza katika bunge lililopita.

"Ninawania kiti cha uspika nikiamini kwamba nina uwezo wa kutibu majeraha makubwa yaliyoliumiza bunge na taifa, wananchi na chama changu kwa sababu tu ya kuwa na kiongozi aliye tayari kujitafutia na kujitwalia umaarufu au ushujaa wake binafsi kwa njia ya kuwahujumu, kuwaumiza na kuwachafua wengine kwa kutengeneza tuhuma za kashfa za kila namna...tiba ya uongozi wa aina hii ni kuchagua kiongozi bora wa bunge...kiongozi mbadala mwenye uwezo na nia njema.

"Ni hatari kuendelea kuliacha bunge likiongozwa na mtu ambaye ubora wake unapimwa kwa umahiri wake wa kuwapaka matope wengine, kuwazushia wengine huku yeye akijitwalia ushujaa ambao gharama zake ni chuki, husuda na kutoaminiana, matokeo yake wananchi ambao siku zote wamekuwa na imani kubwa na viongozi wao, wamelishwa sumu mbaya, hilo limechochea chuki, hasira na kutoaminiana miongoni mwa jamii," alisema Bw. Chenge na kuongeza.

"Mimi kama walivyo wengi wengine, ni miongoni mwa majeruhi wa aina hiyo. Kama bunge, hatuna budi kukabiliana nalo kwa nguvu kubwa...bunge letu limekuwa na changamoto kubwa ya uongozi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, viongozi ambao wajibu wetu wa msingi ni kuonesha njia, badala yake tumekuwa vinara wa uzushi, uongo, fitina na majungu.

Bw. Chenge ambaye kwa muda mrefu amekuwa katikati ya shutuma kali, akituhumiwa katika kashfa kadhaa za ufisadi, amesema kuwa anaamini kuwa kutokana na uzoefu alionao katika utumishi wa muda mrefu serikalini na ndani ya CCM, ana uwezo wa kutibu majeraha makubwa, aliyodai yaliliumiza bunge, taifa, wananchi na chama chake, kwa miaka mitano iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam juu ya nia yake ya kuwania uspika, Bw. Chenge alisema kuwa moja ya sababu iliyomfanya agombee ni kuwa anazo sifa na uzoefu wa kuongoza, akisema kuwa atakuwa daraja imara la kuunganisha shughuli za bunge na serikali, kusaidia chombo hicho kuisimamia serikali, wala si kutoa maagizo.

Akilazimika kujibu maswali mengi kutoka kwa waandishi wa habari walioonesha shauku ya kumtaka aeleze kwa kina tafsiri ya maneno yake hayo ya 'chuki, husuda, hisia, kutoaminiana, kutibu majeraha' iwapo hayatokani na hisia zake, pia yakionesha kuwa anawania nafasi hiyo kwa nia ya kulipiza kisasi akiwakilisha kundi la wabunge watuhumiwa wa ufisadi, Bw. Chenge alitumia nafasi hiyo kukanusha tuhuma za ufisadi ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kwa muda mrefu sasa.

"Nimeomba kukutana na ninyi baada ya kuendelea kusumbuliwa na baadhi yenu mkiniuliza nia yangu ya kuamua kuchukua fomu ya kugombea kiti cha uspika...madhumuni ya kugombea uspika ni kuwa kwa mujibu wa katiba ya nchi, kiti hicho kiko wazi mara rais anapoitisha mkutano wa kwanza wa bunge jipya...lakini pia sifa za kugombea nafasi hiyo ninazo...pia uzoefu wa kuongoza bunge ninao kwa sababu nimeshikilia nafasi mbalimbali serikalini na ndani ya bunge kwa muda mrefu.

Huku akiziita jina la 'makandokando' tuhuma za ufisadi ambazo amekuwa akituhumiwa kwazo, Bw. Chenge alizungumzia suala la kashfa ya kumiliki akaunti ya bilioni 1 nje ya nchi, ambayo ndiyo ilimsababisha akajiuzulu uwaziri mwaka jana baada ya kuziita kuwa ni vijisenti, alisema kuwa fedha hizo ni mali ya mfuko wa kusaidia watoto yatima, ambao hata hivyo hakuutaja jina wala uongozi unaousimamia, ingawa alisema wadhamini wake ni yeye na mke wake, Tina Chenge.

"Kumekuwepo na makandokando yaani maneno au hisia dhidi yangu kuwa nimelisababishia taifa hasara kubwa kupitia mikataba mibovu, hasa kwenye sekta ya madini, ubinafsishaji wa mashirika ya umma, IPTL na kadhalika...kuwa nachunguzwa na makachero wa SFO (Taasisi ya Kuchunguza Ufisadi ya Uingereza), kuhusiana na ununuzi wa rada...jameni napenda kuwaambia kuwa kuhusu mikataba mikubwa...mkataba wowote una aspect (nyanja) mbalimbali kwa kutegemea na subject matter (suala husika) yenyewe.

"Inaweza kuwa commercial (biashara), financial (masuala ya fedha), technical and legal (na kisheria), role (jukumu) ya mwanasheria mkuu ni kuhakikisha mikataba hiyo inakidhi sheria na kanuni za nchi basi. Si masuala ya nchi inapata kiasi gani au fedha kiasi gani, lakini pia mjue waziri mwenye dhamana husika hawezi kutia sahihi mkataba bila ruksa ya rais kwa kuufikisha katika Baraza la Mawaziri na kuidhinishwa...kuhusu suala la rada, kwa ufahamu wangu mimi, SFO walishamaliza uchunguzi na kufunga jalada lao. Hapa nyumbani TAKUKURU na DPP (mkurugenzi wa mashtaka) walishafanya uchunguzi na kufunga majalada yao."

Akijivunia rekodi yake ya kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (1991-1993), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG, 1993-2005), na uzoefu wa kuwa mbunge kwa miaka takribani 20, huku akiwa ameshikilia pia nafasi za uwaziri katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, kabla hajalazimika kujiuzulu kutokana na msukumo wa vyombo vya habari, Bw. Chenge alisema kuwa bunge atakalolisimia iwapo atachaguliwa, litazingatia dhana ya wengi wape, akisisitiza nidhamu na utii kwa chama.

Aliongeza kuwa atasimamia kwa mujibu wa utawala wa mfumo wa demokrasia ya kibunge, akisema kuna pande mbili za bunge, upande wa serikali na wabunge wa chama tawala na upande wa wabunge wa upinzani, huku wale wa chama tawala wakikosoa serikali kwa kuzingatia kauni zilizowekwa na wabunge wa chama hicho, hivyo wanapaswa kujitofautisha na wale wa upinzani ambao wanaikosoa kwa nia ya kuidhoofisha ikiwezekana kuiondoa. Alikataa dhana ya wabunge wote bila kujali vyama kuungana kuwa kitu kimoja, dhidi ya serikali.

Akizungumzia madai hao jana, Spika Sitta alisema, "sina la kusema, nawaachia wananchi, maana ndio wanaoujua mambo haya, wanaujua ukweli, wanatujua sote wawili na ushindi wangu uko mikononi mwa wabunge. Utasema nini juu ya mtu anayeamua kukutuhumu mambo mengi namna hiyo."

     

16 comments:

  1. Huyu Jamaa nadhani ana matatizo na anatakiwa apatiwe ushauri nasaha ili azeeke na busara. Kwa maoni yangu, Chenge hana sifa hata punje ya kuwa Spika wa taasisi nyeti kama Bunge.
    Ni Matuasi kwa Watanzania kuwa na Spika wa aina ya Chenge ambaye anaonesha wazi kuwa safari yake ya Uspika ni kwenda kulinda Mafisadi wenzie. Kwa kweli kwa Chenge kuwa spika heshma ya bunge letu itatoweka machoni pa wananchi na jamii ya kimataifa. Chenge kuwa Spika, Nooooooooooooooo.

    ReplyDelete
  2. Haikubaliki na wala hatudanganyiki. Chenge hana uadilifu wa kuongoza chombo nyeti kama bunge

    ReplyDelete
  3. Chenge hafai hata kidogo kuwa spika wa Bunge letu,Chenge ni mtu wa dharau,na amelionyesha ili kwa kuutaka uspika wa bunge letu wakati wote tunajua ya kuwa si muadilifu,hajaaelezea kuhusu account ya fedha nje alipata tokana na nini,na kama issue ya rada anayodai imeisha iliishaje.Kamwe hafai na hatafaa.apumzike afiche aibu yake asije akafanya ikawa aibu ya bunge na baadaye ya watanzania,nasema CHENGE HAFAI.

    ReplyDelete
  4. Nikweli Chenge hafai kabisa kuwa spika, lakini ninachojua mimi nikwamba atachaguliwa na mafisadi wenzake kulinda masilahi yao.Tena atapita kwa kishindo na atapigiwa debe na baba mwenye nyumba kama ilivyotokea kwenye kampeni za ubunge. Wakuwalaumu ni wananchi wa Bariadi na umaskini wao. Bravo wananchi wa Rombo!!

    ReplyDelete
  5. .......mi nadhani mzee Chenge anazeeka vibaya na hasomi alama za nyakati....kama akili ake inafanya kazi vizuri ni muda muafaka wa yeye kukaa pembeni na laiti mimi ningekua yeye kutokana na yale yalotokea hata ubunge mwaka huu nisingegombea.....Chenge hana jipya la kutuambia watanzania na ni mtu asiye na busara...inatakiwa aende japo kozi fupi ya lugha ili angalau awezepata maneno ya kuongea.....aache uchu wa madaraka.....!!!!
    Mtossah

    ReplyDelete
  6. Mathias Mathias,

    Darubini ni watu, vyombo ni msaada; kama watu ambao ni darubini unaweza ukawagonga na gari wakafa, halafu unakataa kosa, si ataharibu bungeni halafu akatae kosa?. mimi nadhani laana ya Mungu juu ya yale aliyoyafanya yanayoambatana na mikosi, yanamshauri vibaya.

    kwenye mjengo tumeshaomba waingie watu wenye utii, uadilifu na uaminifu. kuna watu anataka kuwakingia kifua, lakini wadau naomba mfahamu, Damu ya mtu lazima ilie. ndiyo hivyo, Damu za aliowagonga na kukataa kufanya hivyo zinalia.

    ReplyDelete
  7. F. Mlay,

    Acheni presha wachangiaji, anguko kuu la ccm linaanza kuonekana.. akiingia Chenge au fisadi mwingine yeyote au yeyote atakayebebwa na mafisadi basi ujue hilo ni anguko kuu 2015..

    Viva waTZ, ukombozi uko karibu

    ReplyDelete
  8. Jamani hawa viongozi hawaoni?jinsi gani watanzania wengi kama sio wote tumechoka kudanganywa? ANGUKO KUU LINAKUJA MWAKA 2015.



    VIVA WATz

    ReplyDelete
  9. Uspika si kucheza disco, muda huo wa kuwasaidia watanzania ataupata wapi na DISCO ataenda saa ngap, laana ya kuua roho za watu wasio na hatia inamchanga, na kama mafisadi wenzake watamchagua basi ndio mwisho wa chama chetu tawala maana watakomba mpaka tone la mwisho na kutuachia nchi yetu ilijaa kila aina ya neema na madeni yasiyolipika.....e mola nautuepushie balaa hili...Chenge hafai kuwa hata mkuu wa familia achilia uspika.

    ReplyDelete
  10. KWA UKWELI NIA YAKE KUJIFICHA KTK KICHAKA CHA BUNGE ILI ASIZIDI KUUMBUKA, LAKINI KWA STAILI HII KAINGIA CHOO CHA KIKE, KWANZA HATUJAJUWA HATMA YA VIJISENTI VYAKE,PILI KUHUSU KESI YAKE YA RADA, TATU KAUA WATU 2 KWA UZEMBE NA ULEVI, TATU KULE KTK KAMPENI TENA KAGONGA, NI MAMBO MENGI SANA NA BADO ANAONGEZA MAJERAHA BADALA YA KUTIBU MAJERAHA WALIOKUWA NAYO!!KUHUSU ANGUKO KUU 2015 HIYO LINABIDI MUTAFAKARI UPYA SI LELEMAMA MAANA CCM WAMESHAJUWA WAPI WALIPO JIKWAA WANATAFAKARI NA PIA KUSEMA KUWA UKOMBOZI UKO KARIBU TZ UNA HAKIKA NA UNALOSEMA? AU NDIO KUTAKA KUONGEZA CHUKI BAINA YA WATU NA CCM!? UKOMBOZI UNATAKA KUJIKOMBOA KUTOKA KTK MIKONO SALAMA? UINGIE KTK MIKONO YA MFANO WA AL-SHABBAB?POLE KWA FIKRA POTOFU TUKO KTK AMANI NA SALAMA KAMA UKO MBALI NJOO UONE MAMBO WACHA FITNA NA MAJUNGU.FIKIRI KABLA YA KUTAMKA!!TUKO HURU NA MAKINI

    ReplyDelete
  11. Watanzania tuwe makini ni wapi tunakwenda na tunaipeleka nchi yetu.

    Mtu kama huyu akiwa spika kwa kweli tunaelekea kubaya. Wabunge inabidi kuwa makini wanamchagua nani. na wajue wanawakilisha wananchi sio mafisadi.

    ReplyDelete
  12. Kimsingi anachofanya Chenge ni kutaka kulinajisi bunge kwa kuwapa mafisadi wenzake sehemu ya kujisafishia na kupanga dili nyingine kubwa zitakazoliacha taifa msambweni kama si kaburini. Anasifika kwa kuwahonga na kuwapofua wapiga kura wake. Anaiba sana ili awahonge sana nao wamchague sana. Je kipi muihimu-kutatua matatizo ya mtu mmoja mmoja au jamii kwa ujumla? Kwanini kuiba pesa ya nchi ili kuwahonga watu wa eneo lake?
    Hakuna kimenishangaza kama alivyoonyesha jeuri ya kifisadi hadi kufikia kugombea hata uspika. Ili iweje? Tujalie mbunge wa upinzani aje na hoja ya kutaka kujadili wizi wa rada, Chenge kama spika kweli ataruhusu hiki kitanzi kivikwe shingoni mwake? Je wabunge wetu nao watakuwa wameishiwa kiasi gani kumchagua mtuhumiwa wa uhujumu hivi? Yetu macho na nani ajuaye iwapo ufisadi nchini mwetu umehalalishwa huku uadilifu ukiharamishwa?
    Na kwa kumsafisha, kama NEC, TAKUKURU imethibitisha dhana kuwa ni Taasisi ya Kudumisha na Kutetea Rushwa basi.
    Chenge hafai hata kuwa spika wa kijiwe cha kahawa achilia mbali bunge letu tukufu.

    ReplyDelete
  13. HAYA NI MATUSI KWA WATANZANIA, NA IKO SIKU WATACHOKA,HIVI KWELI CCM INAWEZA KUDIRIKI KUMPATIA FOMU ZA KUGOMBEA USPIKA MTU ALIYE SUBUTU KUITA MAMILIONI ALIYO WEKA NJE KUWA VISENTI WAKATI WATANZANIA HATA MLO MMOJA NI KWA TABU. MTUKUFU RAISI AMEWATAKA WATANZANIA KUPONYESHA VIDONDA VYETU.AMESAHAU KUWA VIDONDA VIKUBWA VILIVYO WAKERA WATANZANIA NI PAMOJA NA FEDHA ALIZO ZIITA VISENTI ?. MIMI NI MWANACHAMA WA CCM NA NIKIONGOZI HATA KAMA SI WA NGAZI YA JUU.UKWELI NI HUU: TUMEPOTEZA VITI VINGI KWA SABABU YA VISENTI,RICHMOND, NA CCM KUTO CHUKUA HATUA KALI NDANI YA CHAMA KWA VIONGOZI WANAONYOSHEWA VIDOLE NA WANANCHI AMBAO NI WAPIGA KURA WETU.LEO UNAKUJA KUZOMEA WATANZANIA HIVI UNAWAFANYA MBUMBU AU NI KEBEHI YA AINA GANI?.NAKUOMBA MHESHIMIWA RAIS HILI USILIFUMBIE MACHO, KUZOENA KANDO, URAFIKI KANDO. TAIFA LINAHITAJI WATANZANIA WATAKAONA UCHUNGU JUU YA HALI MBAYA, NA VIONGOZI WANAOCHUKIA UFISADI KWA VITENDO NA WANANCHI WASEME NDIYO: NINAMKUMBUKA SANA BABA WA TAIFA NINA UHAKIKA ANGEKEMEA NA KUSEMA TUPISHE UNAKICHAFUA CHAMA!.KWA MPANGO HUU NAOMBA CHAMA KINIKOPESHE FOMU NIGOMBEE USPIKA MAANA NAONA WANA CCM WENYE HURUMA NA NCHI WAMEKWISHA NA WATU WAADIRIFU HATUNA FEDHA ZA KUCHUKULIA FOMU.MH: RAIS PUNGUZA UPOLE HATA KAMA NI UTAWALA WA SHERIA UNAOTUTIA AIBU TUKATAE IKO SIKU MH: RAIS UTAKUJA KUKUTA UMECHAGULIWA WEWE NA UNA BUNGE LA UPINZANI LOTE HEBU TAFAKARI BWANA VISENTI NDO SPIKA WA BUNGE UNADHANI 2015 WANANCHI WATATUFANYAJE? NAKUSIHI MWENYEKITI WETU WA CCM TUMIA HEKIMA YAKO KUHAKIKISHA KUWA TUNAKUWA NA SPIKA WA BUNGE AMBAYE NI WAZI WATANZANI WANAMTARAJIA NA NI DHAHILI HATA WEWE UNAJUA WATANZANIA WANAMTAKA NANI KWA SASA NA HII ITAONGEZA IMANI KWA CHAMA CHETU CCM.KUPITA UBUNGE NI MCHEZA KWAO, MTOTO WA MTU NI WA MTU!.MAANA MZAZI NDIYE ANAYE FAIDI VISENTI VYA MAMILIONI WAKATI TUNALALA NJAA.

    ReplyDelete
  14. Chenge asijigambe Kuwa FSO wamemuona hahusiki na rushwa ya kashifa ya rada. Kwa mujibu wa kifungu cha 2 cha Criminal Justice Act 1987, mkurugenzi wa FSO ana mamlaka ya kumuita mtuhumiwa kufika mbele yake kujibu maswali na kutoa vielelezo kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.Kwa mujibu wa kifungu hicho SFO haiwezi kumshitakiwa kwa kutumia maelezo au vielelezo alivyotoa mbele yake. Hata hivyo anaweza kushitakiwa tu iwapo itangundulika kuwa maelezo au vielelezo vyake vilikuwa vya uongo. Hii maana yake ni kwamba Chenge inawezekana alikiri ( au alieleza ukweli wa mambo) ndiyo maana hawezi kushitakiwa kwa kosa hilo.Kifupi ni kwamba amesaidiwa na udhaifu wa sheria hiyo ya makosa ya jinai ya hapa UK. Ashukuru mungu ingekuwa ni USA kule hawana mchezo. PATRIOT Act 2001 ingemsurubu. Namalizia kwa kusema kuwa Chenge hafai kushika nafasi hiyo ya uspika. Kwa jinsi nilivyomuelewa baada ya kusoma habari hii, anagombea nafasi hiyo ili kulipiza kisasi (kutibu majeraha).
    Tanzanian law student in UK

    ReplyDelete
  15. Jamani watanzania ikiwezekana vyombo vya Haki za binadamu na mashhirika ya binafsi ,na vyama vya siasa viandae maandamano makubwa kupinga kupititishwa jina la Chenge kuwa spika.

    ReplyDelete
  16. hawezi kuchaguliwa msihofu

    ReplyDelete