05 November 2010

Watano wachukua fomu kuwania uspika.

Na John Daniel

KINYANG'ANYIRO cha kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania kimeshika kasi baada ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
Waziri wa Miundombinu, Bw. Endrew Chenge kujitokeza kuchukua fomu kumvaa spika anayetetea nafasi yake, Bw. Samwel Sitta.

Mbali na Bw. Chenge pia aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge, Bw. Job Ndugai na Mbunge wa Afrika Mashariki, Bi. Kate Kamba nao walijitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo jana.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuchukua fomu hiyo jana, Bw. Chenge alisema anaamini kuwa anao uwezo na uzoefu wa kutosha kuendesha bunge.

"Mimi nina uzoefu mkubwa wa mfumo wa kuendesha serikali, kazi kubwa ya spika ni kuunganisha wananchi na serikali. Spika ni daraja na anatakiwa aunganishe wabunge wote bila kuwa na kundi wala upendeleo.

"Lakini ni lazima uhakikishe chama kilichochaguliwa kuongoza serikali kinapata nafasi kubwa zaidi kutekeleza mipango yake," alisema Bw. Chenge.

Akijibu swali la wana habari kuhusu ongezeko la wabunge wa kambi ya upinznai bungeni tofauti na bunge lililopita, Bw. Chenge alisema hilo halimpi wasiwasi iwapo atachaguliwa.

"Mwaka 1995 hali ilikuwa sawa na hii, mwaka huu imezidi kidogo tu, lakini mimi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali tulihimili vizuri sana, hilo halinipi wasiwasi," alisema Bw. Chenge.

Kwa upande wake Bi. Kamba alisema anamini kuwa iwapo atachaguliwa ataimarisha bunge zaidi kwa kuwa anao uzoefu wa Bunge la Afrika na uongozi ndani ya serikali na CCM.

Kuhusu kuongezeka kwa wabunge wa upinzani alisema hilo ndilo furaha yake kwa kuwa kuwepo kwao kutaichangamsha serikali na kuongeza utendaji.

"Bunge lenye wapinzani ndilo ninalopenda mimi, hata kama wangefika asilimia 30 bado ingefaa tu maana wanasaidia serikali kuwa macho zaidi, mimi hilo halinipi wasiwasi," alisema.

Akizungumza na Majira, Bw. Sitta, alisema amefurahishwa na demokrasia ya wengi kujitokeza kuwania nafasi hiyo na kwamba hana wasiwasi hata kama wangejitokeza zaidi ya 20.

 "Kwanza sina wasiwasi hata kama angejitokeza nani, hata wakiwa 20 hakuna tatizo, mimi nina rekodi ya kuendesha bunge vizuri na viwango, kama nisingejitokeza kutetea nafasi yangu Watanzania wangenishangaa sana.

Alipoulizwa kama ahofii watu wanaodaiwa kupandikizwa kupambana naye, alisema, "Mimi sijui kama kuna mtu au watu wametumwa kupambana na mimi, lakini hata kama wapo hilo halinipi shida, ninajiamini," alisema Bw. Sitta.

Kumekwepo na uvumi kwamba wapo wagombea waliotumwa na mojawapo ya kundi hasimu dhidi ya Sitta ili kuhakikisha anashindwa kurejea katika nafasi yake ya uspika.

Kundi hilo linadaiwa kuongozwa na watu wanaochukizwa na msimamo wa kiongozi huyo katika masuala nyeti yenye maslahi kwa Taifa, hasa mapambano dhidi ya ufisadi.

Kwa upande wake Bw. Ndugai alisema kutokana na uzoefu wake ndani kwa vipindi vitatu mfululizo anao uzoefu na uwezo mkubwa wa kuhimili nafasi ya uspika.

"Kwanza nimekuwa Mwenyekiti wa Bunge, nimekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Mali Asili na Mazingira, nitasimamia sheria zilizopitishwa kwa maslahi ya taifa," alisema.

Mtu mwingine aliyejitokeza jana kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo ni Luteni Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Benedict Lukwembe.

Hadi Majira inaondoka katika Ofisi za CCM jana jumla ya wana CCM watano walikuwa walichukua fomu kupambana na Bw. Sitta.

Wakati huohio Katibu Mkuu wa CCM Bw. Yusuf Makamba, ametangaza kuongezwa kwa muda wa kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya nafafsi ya uspika kutoka leo hadi Novemba 8 saa 10 jioni muda ili kutoa nafsi zaidi kwa wanachama wake kupata nafasi ya kutosha kujiandaa.

6 comments:

  1. JAMANI CHONDE CHONDE WABUNGE WETU KUWENI MAKINI NA MTAKAYEMCHAGUA,KWA MAANA TULITARAJIA KUWA NA BUNGE IMARA LAKINI???? KUNA WATU WAMEINGIA AMBAO HAWANA SIFA NJEMA TENA WANATAKA WAWE SPIKA,HAWAFAI HATA KIDOGO,WATAWAVURUGA NA KUTETEA YALE TULIYOKUWA TUNAPINGANA NAYO,HWAFAI HATA.........KIDOGO SIYO WADILIFU NA WOTE MNA MACHO.MWENYE MACHO AAMBIWI TAZAMA

    ReplyDelete
  2. Napata wasiwasi kwa baadhi yenu, kama mliweza kuona ni sawa kuhodhi vya uma na kuona si kitu hivi kweli mtatetea maslahi yetu mkiwa spika? Kumbukeni kuna watu wanaishi chini ya dola moja wakati wenzetu bilioni moja kwenu ni visenti. Kweli tutaimba na kucheza ngoma inayofanana?

    ReplyDelete
  3. CCM MARA ZOTE HUANGALIA MASLAHI YA WACHACHE YAANI MAFISADI. USPIKA UNAENDA KIULAINI KWA UPINZANI. WAPINZANI CHONDE CHONDE MKAO WA KUIMALIZA CCM HUO UNAKUJA BUNGENI. HUKO HAKUNA TUME YA MAKAME. WAPINZANI UNGANENI KUKIONDOA CHAMA CHA MAFISADI.

    ReplyDelete
  4. Ewe mola tusaidie wanao watanzania kupitia bunge letu tukufu kumpata spika imara,nawe mzee wa vijisenti una jipya gani?Nchi uliiingiza hapa tulipo kwa mikataba yako yenye maslahi binafsi, halafu tena unataka tukukabidhi uspika siutawauza hadi wabunge sasa upate vijishilingi? Waheshimiwa kuweni macho na hao wajanja msijikute mnauzwa kwa percentage.

    ReplyDelete
  5. Ewe Mola mwenye fadhila nyingi, tunakushukuru kwa taifa letu la Tanzania.Tunaomba uwajalie wabunge wetu busara katika kumchagua spika wa bunge.Tanzania bila umaskini inawezekana.Ndugu wabunge wetu bila kujali chama wala itikadi zenu,tuliweke taifa letu mbele.Hatutaki kuwa kicheko eti "luggards of development" kisa hatujaamua kusimamia rasilimali zetu.Tuna uwezo, basi tuwe na nia ya kulijenga taifa letu lisonge mbele, watoto wake waishi kwa amani na sote tuseme ASANTE MUNGU KWA KUTUWEKA TANZANIA.Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

    ReplyDelete
  6. I have a very big question to all Tanzanians, WHEN will we wake up and rise to the occasion, to know that its our right and not a priviledge to get what we deserve? poor or no roads, lack of water, lack of adequate education and unimaginable poverty are not our rights but the opposite is our rights.We therefore urge our politicians to stop playing around with peoples lives and get down to work.lets create a working nation and fight poverty with all our might.Together, we can.Mr president, if it happens that you also read this comment, KNOW that the lives of all Tanzanians entirely depends on the decisions you make in your office, so act wisely and aspire for greater change, kuona Tanzania yenye mafanikio.I wish all our leaders an ample time in their endeavors of making Tanzania a prosperous nation.Please this time, make us proud, at least show that you can in these five years of service.
    Call me Mzalendo.

    ReplyDelete