05 November 2010

TACCEO yataja kasoro uchaguzi mkuu.

Na Tumaini Makene

KASORO mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu, ikiwemo muundo mbaya wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na matumizi ya
teknolojia mpya, zimedaiwa kusababisha kutokuwa wa haki.

Mbali na kasoro hizo, zingine ni uwezo mdogo wa wasimamizi wa uchaguzi juu ya baadhi ya taratibu za uchaguzi, daftari la wapiga kura kutopatikana kiurahisi ili watu wahakiki majina yao, majina ya wapiga kura kutokuonekana vituoni na kukosewa kwa namba za kitambulisho cha mpiga kura, ambazo ziliwafanya wananchi kushindwa kutumia haki yao ya kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Hayo yamo katika taarifa ya awali ya Mtandao wa Mashirika 17 ya Asasi za Kiraia (TACCEO) yakiongozwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambayo yalikuwa na waangalizi wa uchaguzi katika majimbo kadhaa ya nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, kwa niaba ya TACCEO, mmoja wa wajumbe wa mtandao wa mashirika hayo, Bi. Martina Kabisama alisema kuwa kasoro hizo zimeufanya uchaguzi huo uwe huru lakini si wa haki.

"Ingawa tunakiri kuna baadhi ya maeneo NEC imefanya vizuri na inaweza kusifiwa, lakini leo tunajielekeza katika mapungufu zaidi. Daftari la wapiga kura halikupatikana kwa urahisi pamoja na kuwa liliwekwa mtandaoni, lakini si wananachi wengi wanaweza ku-access (kupata) taarifa za mtandaoni...lakini pia hata huko lilikuwa halipatikani kwa urahisi.

"Watu wengi hawakuona majina yao kwenye daftari, lakini hata vituoni yalipobandikwa wengi walipata taabu kuyaona au hawakuyaona kabisa...bado hata namba yenyewe ya watu waliosajiliwa inatia shaka maana inaonesha kuwa karibu nusu ya Watanzania wote nchini wana sifa za kupiga kura, kitu ambacho kinatia wasiwasi," alisema Bi. Kabisama.

1 comment:

  1. Kikwete kasema "Yaliyopita si ndwele tugange yajayo", lakini kwa kasoro hizi zilizotajwa na TACCEO, tusijikusanyie kazi, tutibu kasoro hizi ikiwa chama tawala na NEC vinataka viaminiwe na kuheshimiwa na Watanzania. Mheshimiwa Kikwete asijiridhishe kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani na kitaendelea kuwa hivyo daima. Ikiwa CCM na NEC vitaendelea kuwaona Watanzania kuwa ni mazezeta, iko siku mambo yanaweza kuwatoka mikononi. Kwa hiyo, kabla ya kufikiria kuganga yajayo, iponye vidonda vya uchaguzi alivyovitaja kwa kuondoa (sio kupunguza) kasoro za NEC zilizofanywa ama kwa makusudi au uzembe.

    ReplyDelete