05 November 2010

Usalama wa Taifa wamjibu Dkt. Slaa.

* Wasema madai yake ya uongo, yanalenga kuvuruga amani
* Rostam ajitetea tuhuma za kupanga uchakachuaji kura
* Yeye ataka wasijibu kisiasa bali wafanyie kazi madai

Grace Michael na Tumaini Makene

IDARA ya Usalama wa Taifa imejitokeza kujibu tuhuma mbalimbali zinazotolewa na mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),
Dkt. Willibrod Slaa na kusema kuwa taarifa anazotoa kwa wananchi ni za uongo zenye lengo la kuvuruga amani ya nchi.

Hivi karibuni, mwanasiasa huyo alikaririwa akiihusisha Idara hiyo na uchakachuaji matokeo ya kura za urais kwa nia ya kumsaidia mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete.

Hatua ya kujitokeza hadharani viongozi waandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa kujibu hoja za wanasiasa, ni ya kwanza katika historia ya mfumo wa vyama vingi nchini na zaidi tangu nchi ipate uhuru.

Akijibu tuhuma hizo, Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama, Bw. Jacky Zoka aliwataka wananchi kupuuza kauli hizo na kueleza kuwa Dkt. Slaa anatumia taarifa za uongo kuwachochea. Alisisitiza kwamba idara hiyo haiwezi na wala haiko kwa ajili ya kukisaidia chama chochote kwa maslahi ya nchi.

“Tangu kampeni za Uchaguzi Mkuu zilipoanza, kumekuwa na tuhuma mbalimbali kuwa Idara imekuwa ikiwasaidia baadhi ya wagombea,  hususan  CCM na tuhuma hizo zimekuwa zikitolewa na  Dkt. Slaa, tuhuma hizo zimekuwa hazijibiwi kwa sababu si utaratibu wa idara kujibu mambo ya namna hiyo lakini imefika mahala idara imeona itoe tamko,” alisema Bw. Zoka.

Alisema kuwa Idara imefikia hatua ya kujibu kutokana na kuona kwamba kimya chake kinachukuliwa kama sababu ya kumfanya Dkt. Slaa azidi kutoa tuhuma za uongo hasa anapoona matokeo yanayoendelea kutolewa, hayamwendei vizuri.

“Kwa mfano jana (juzi), alizungumza na vyombo vya habari na kudai kuwa matokeo yanayotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni yaliyotengenezwa na Idara ya Usalama hivyo hatayakubali...tuhuma hizi ni nzito na zisipojibiwa wananchi wanaweza kuamini kuwa viongozi watakaopatikana si wale waliowachagua bali ni wale ambao idara ilitaka wawe,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuwa Idara inachukulia tuhuma hizi kama jitihada zilizopangwa makusudi kwa nia ya kuichonganisha na wananchi na kuwahakikishia kuwa tuhuma hizo ni za kuzua zenye lengo maalum la kuchochea au kutaka aonewe huruma na wananchi.

Alisema kuwa utaratibu wa kupiga kura ni wa wazi unaoendeshwa kwa kanuni ambazo hazihusishi Idara ya Usalama na kura zinapopigwa na kuhesabiwa, hakuna ofisa usalama anayekuwepo hivyo idara haihusiki kwa namna yoyote ile katika mchakato mzima.

Bw. Zoka alisema kwa utaratibu huo haiingia akilini ni sehemu gani ambapo ofisa usalama anaweza kupata nafasi ya kuchakachua kura hizo hivyo tuhuma hizo zina lengo pia la kuipaka matope idara hiyo.

“Lengo la Idara ni kuhakikisha nchi inakuwa na amani na sikuwa chanzo cha kuhatarisha usalama kwani ina jukumu la kufanya kazi kwa maslahi ya Taifa hivyo hawana sababu ya kuchakachua kura kwa kuwa suala hilo halina maslahi kwa taifa,” alisema.

Akizungumzia utendaji  kazi ya Idara hiyo, alisema ni chombo kinachofanya kazi kwa misingi ya maadili yaliyoainishwa kisheria na misingi hiyo haina sehemu ya kupendelea chama chochote na utaratibu wa kufanya kazi zake kwa siri usiwe chanzo cha watu kama Dkt. Slaa kuituhumu kwa mambo ya uongo yasiyo na nia njema kwa Taifa.

“Kama ana ushahidi kuwa Idara inahusika na anayoyasema atoe autoe na kila mtu athibitishe bila shaka yoyote ...tunasisitiza kwamba kwa makusudi au kwa kudanganywa na wanaojiita maofisa wa usalama, Slaa mejikuta akitumia taarifa za uongo kutoa matamshi ya kuwadanganya Watanzania ili kuwachochea kuvunja amani kwa lugha ya kawaida, ameingizwa mjini na yeye akaingia kichwa kichwa,” alisema Bw. Zoka.

Alisisitiza kuwa  Idara haihusiki kwa njia yoyote kuingiza taifa kwenye mgogoro wa kisiasa kama anavyotaka wananchi waamini.

Wakati huo huo Dkt. Willibrod Slaa ameeleza kushangazwa kwake na hatua ya Idara ya Usalama wa Taifa kuamua kujibu hoja kama wanasiasa badala ya kufanyia kazi taarifa na kuliokoa taifa katika ufisadi unaolitafuna taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari juu ya tamko la Usalama wa Taifa, lililotolewa mapema jana na Naibu Mkurugenzi wa Idara Bw. Zoka,  Dkt. Slaa alisema kwa kawaida Idara hiyo ilipaswa kufanyia kazi taarifa za ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi kwa maslahi ya nchi na wananchi ambao ndiyo waajiri wao, si kukanusha kuwa hawakuhusika na uchakachuaji wa matokeo.

"Nimeshasema mimi sitishiki...katika principle (masuala ya msingi) mimi sitishiki na mtu yeyote...nimeshasema kuchakachua kura ni ufisadi kama ufisadi mwingine na nitauita hivyo hivyo, Usalama wa Taifa walipaswa kufanyia kazi taarifa nilizozitoa jana si kujibu kama wanasiasa, kama wanataka basi nao waingie kwenye siasa ili wajue maana ya kile ninachokizungumza juu ya wizi wa kura.

"Mimi nina uzoefu nao tangu wakati wa ufisadi wa EPA nilipata barua yao wakizuia hoja za ufisadi wa EPA, isiende bungeni, wanamweleza Waziri Mkuu kuwa serikali haina majibu ya hoja ya ufisadi huo...nilitegemea wafanyie kazi taarifa si kukana kuwa hawahusiki nilichokisema," alisema Dkt. Slaa na kuongeza;

"Nafurahi kwa mara ya kwanza Usalama wamejibu tuhuma, tena wameandika, maana mtu akiandika unamjua vizuri...nilitegemea kwa mfano Dkt. Slaa anasema kura zake zilizoko vituoni ni elfu ishirini lakini zimetangazwa elfu tatu, wazitafute hizi wajue zimeenda wapi, ndiyo kazi yao walipaswa kuwa wa kwanza kujua...wajue kuwa Usalama wa Taifa si Usalama wa CCM, wala chama chochote kingine, bali taifa."

Alisema kuwa Idara hiyo imeajiriwa kwa kodi ya Watanzania wote hivyo wanapaswa kulinda maslahi ya nchi na kudai kuwa kwa sasa haifai, kwani imeshindwa mara kadhaa kulinda maslahi ya na haki za watu."

Kuna mahali huyu Naibu Mkurugenzi ameandika juu ya Sheria ya Uchaguzi, hii haina haja, anazungumzia nadharia, sisi tunataka vitendo, tuko kwenye siasa haya ya Sheria za Uchaguzi tunayajua vizuri...kwa mfano ninazo taarifa kuwa walikwenda Karatu wakaingia vituoni wakitoa maelekezo, msimamizi akawakatalia akisema hawaruhusiwi kuwa vituoni, wala hakuna taarifa ya uwepo wao.

Mapema, mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni, Bw. Philip Mugendi alidai kuwa yeye na wagombea wengine wa vyama vya upinzani walikamata masanduku 25 ya kura katika nafasi ya urais na ubunge, ambayo yalikuwa hayajahesabiwa lakini yalikuwa katika eneo la kujumlishia matokeo.

Akitoa namba ya masanduku hayo 25, alidai kuwa yalikuwa mengi zaidi lakini wakanakiri idadi hiyo wakiamini ni ushahidi wa kutosha, Bw. Mugendi alisema kuwa matokeo ya Jimbo la Kinondoni katika nafasi zote za udiwani, ubunge na urais, yamechakachuliwa kwa kiasi kikubwa ambacho yanatia shaka kuaminika, kwani kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.

Wakati huo huo, Mbunge mteule wa Jimbo la Igunga, Bw. Rostam Aziz amekanusha tuhuma zilizotolewa na Dkt. Slaa kuwa alishiriki kikao cha kupanga kuhujumu uchaguzi huko Mwanza.

Katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, Bw. Rostam alisema taarifa hizo ni za uongo kwani tarehe iliyotajwa alikuwa safarini Afrika Kusini na alirejea, Oktoba 19 mwaka huu.

"Tarehe anazotaja Dkt. Slaa,mimi nilikuwa Afrika Kusini na nimerejea nchini usiku wa Oktoba 19, 2010. Kwa maana hito nisingeweza kuwa Mwanza , Napenda kuambatanisha nakala ya pasipoti yangu na nakala ya tiketi  ikionesha siku nilipoondoka kwenda afrika Kusini na siku niliporejea,"  alisema Bw. Rostam na kuongeza ;

Hata kama ningekuwepo nchini  kwa mfumo wetu wa uchaguzi  uwezekano wa mtu , kikundi au taasisi kuiba kura haupo. Wasimamizi wa Uchaguzi wa Kimataifa wamesifia mfumo wetu  na wameeleza utaratibu mzima ulivyokwenda  vizuri na wameeleza kuwa uchaguzi huu ulikuwa huru na wa haki"

Alimshambulia Bw. Slaa na kumwelezea kuwa ni mwongo na mkurupukaji na kwamba anazusha jambo hilo kwa lengo la kuwapotosha Watanzania.

" Dkt. Slaa ni mtu mzushi, mwongo na mkurupukaji, hata historia yake inathibitisha kuwa si mtu mkweli. Watanzania ni vizuri wamemfahamu Dkt. Slaa kuwa amekuwa mtu asiyeaminika  katika maisha yake yote  na kwa ajili hiyo wamemnyima fursa ya kuongoza taifa letu. Amedanganya katika kampeni  na kabla ya kampeni ana historia ya kumdanganya hata Mungu, hivyo haiwezi kuwa kazi ngumu kwake kumzushia mtu yeyote na kuwapotosha Watanzania" alisema Bw. Rostam na kuongeza;

"Slaa na CHADEMA tangu mwanzo wa kampeni walijua watashindwa  na wamejiandaa kukataa matokeo na kusababisha vurugu kutishia nyau  waingizwe serikalini  kama ilivyotokea Zanzibar . Uongo huu umethibitisha nia yao hiyo. Watanzania tukatae hila zao , uchaguzi umekwisha, wananchi wameamua."

14 comments:

  1. Kwani Rostam anafanya kazi ktk ofisi ya Mungu? kama sivyo anajuaje kwamba Dk Slaa amemdanganya Mungu?Yeye Rostam na Mungu nani zaidi? anawezaje kuwa msemaji wa Mungu? Kwani Mungu hujui kwamba Rostam ni mwizi kupitia Kampuni yake ya Kagoda?

    ReplyDelete
  2. Hivi huyu Rostam ni nani hasa?? ametumwa na nani?? amekaa bungeni miaka 5,bila kuchangia hoja ye yote kwa kusema au maandishi,hivi hata huko bungeni anaenda kufanya nini,au ni kwa nini anaenda Bungeni na hana mchango wo wote,ina maana jimbo la IGUNGA HAWANA JAMBO LA KUSEMA KUHUSU HOJA ZOTE ZILIZOWAHI KUPELEKWA BUNGENI???

    ReplyDelete
  3. Slaa ni Padre lakini amediriki kutembea na mke wa mtu hakuridhika akaamua kumtangaza km mchumba wake yeye akiwa km kiongozi wa dini kioo cha jamii sasa hapo ni kwamba amemdanganya MUNGU huu ndio ukweli si kila asemayo ni kweli na ipo siku atakosa ushahidi ataingia matatizo punguza speed kaka itakuponza hutoona mpambe hata mmja.mdau japan

    ReplyDelete
  4. Wanausalama fanyeni kazi zenu sio kuja kuwa wanasiasa, inaonyesha wazi kwamba yote aliyotamka Dr. Slaa ni ya kweli kabisa ingekuwa sio ya kweli msingejitokeza kupinga. Kwanza jana Kiravu alikiri, pili kucheleweshwa matokeo, tatu sehemu ambayo chama tawala kilikuwa na uhakika wa kushinda matokeo yake yalitangazwa haraka nne Mgombea wa jimbo la Segerea pamoja na kukamatwa na masanduku ya kura bila ya usalama kuchukua hatua inaonyesha wazi kabisa kwamba mmeshiriki katika kuchakachua matokeo yote ya uchaguzi wala sio kwa uraisi peke yake. Kiongozi wa juu namna hiyo wa usalama hapo umebugi step jisahihishe fanyakazi uliyotumwa watananzania wa sasa sio kama wale wa zamani kujitokeza kwako kwenye vyombo vya habari kunaashiria wazi kwamba maneno yote ya Dr. Slaa ni ya kweli. Tafadhali kuweni macho Watanzania wana hasira mbaya kwa sasa hasahasa Vijana.Umakini wa kusema uwepo wa tu wanasikiliza sana maneno yanayotolewa na wanasoma habari.

    ReplyDelete
  5. wewe tuanzungumza hoja ya slaa na usalama wa taifa na hasa habari hii iliyo hapa sasa,kama mtu mwingine hana la kuchangia katika ilo asubiri hoja anayoweza kuchangia achangie,atusemi sifa ya mtu hapa kwani kama hivyo hata huyo ambaye mnaona anafaa afai mambo yake mengi tu yanafahamika na wala magazeti yote yasingetosha kama tungeyaandika.kwa hiyo tuseme HOJA iliyoandikwa hapa.

    ReplyDelete
  6. Imani ni nzuri na uchunguzi ni mzuri. Lakin Dr amezidi. Hana ujuzi wowote ktk masuala ya usalama na ktk maisha yake atategemea usalama. sasa leo anawafundisha kazi usalama. hebu jiulize hivi leo slaa angepewa nchi ni nani angemfanyia shughuli za ulinzi kama sio hao usalama? nina wasiwasi na tena ni hakika kuwa kamwe slaa hatapewa nchi since Ikulu hufanya kazi na usalama, jeshi, polisi na hata magereza. na leo ni maadui wake wakubwa, inakuingia akilini kweli kwa mtu kama huyo kukabidhiwa nchi. je atawafukuza majeshi wote na kuanza kuajiri wapya au ndio watu wa kufanya nae kazi. Hebu jiulize mara 2 na zaidi. ktk vitu muhimu ktk nchi ndio hivyo tena jeshi, usalama na polisi. so ajifunze kudili na watu na si kuwafanya maadui wake
    thank, by

    ReplyDelete
  7. Wafanyakazi wa Usalama wa Taifa/CCM ni watu kama wengine na wanatoka jamii hii hii ya Kitanzania. Kama TAKUKURU imeweza kushiriki kwenye Richmond, je, Usalama wa CCM wana tofauti gani nao. Hawa ni wachumia tumboni. Hawahurumii wananchi wanaoshindwa kuwasomesha watoto wao na wagonjwa kufa kwa kukosa matibabu. Vyama vya Uzalendo/upinzani vinapokuja na sera za kuwanufaisha watanzania, vyombo vya dola vinakandamiza. Je, ni mtanzania gani anayependa watoto wake wasome bure kama wanavyosomeshwa Wanausalama wa CCM na kutibiwa bure, asiichague CHADEMA au CUF; bali aichague CCM inayowanyonya watanzania? KAZIKAZI.

    ReplyDelete
  8. Kumbe hata usalama wa taifa wamekiri walituma usalama wa taifa nzima kipindi cha uchaguzi eti kwa ajili ya usalama? hapa nimeshapata jibu moja kwa moja walihusika, no dought

    ReplyDelete
  9. Kama Usalama wa CCM unasema Dkt. Slaa ameingizwa mjini kwa kumpatiwa taarifa za uongo na wanaojifanya usalama wa taifa, kwanini basi msiwatafute na kuwakamata watu hao kwa kujifanya watu wa usalama wa taifa kumbe watu wa usalama wa CCM? Kwahiyo ninyi ni usalama wa ccm na wala si usalama wa taifa, mnashindwaje kuwakamata!.

    ReplyDelete
  10. USALAMA WA TAIFA TUWASIFU KWA LIPI?. MNAANGAMIZA TAIFA KWA KUWALINDA MAFISADI? KWANI SLAA KASEMA UONGO? KAMA KWELI USALAMA WA TAIFA MNAFANYA KAZI, ILIKUWAJE RICHMOND WAKALIINGIZA TAIFA MKENGE, ILIKUWAJE EPA IKAIBIWA? MLIKUWA WAPI? MSITAKE KUTUTIBUA, TUNAWAVUMILIA TU LAKINI NYIE NDIO MNAOFANIKISHA WIZI. ETI BAJETI ZENU NI SIRI! JIFUNZENI KWA WENZENU WA MAREKANI, URUSI, CHINA, INDIA, IRAN, ISRAEL, NK. WANALINDA NCHI ZAO. NYIE HAMUONI AIBU TAIFA LETU KUIBIWA? WALINZI GANI NYIE! AU NYIE SIO WENZETU. MMEAJIRIWA NA ROSTAM AU WANANCHI WA TANZANIA?

    ReplyDelete
  11. CCM wasituhadae na amani. Amani haiwezi kuwapo bila kutenda haki. Kwanini amani ya Tanzania itegemee ukondoo na si kutenda haki? Hata Kikwete na waramba viatu wake wanajua hakushinda kihalali bali kwa kutegemea uchakachuaji na upuuzi mwingine utokanao na jinai ya kuiba. Ni ushindi wa aibu na pigo kwa taifa hasa wale wanaochukia ufisadi ambao Kikwete anaulinda kwa vile ulimuingiza madarakani. Slaa shikilia msimamo maana hakuna wa kukufanya kitu. Wanaogopa kunyea debe The Hague.

    ReplyDelete
  12. Huyu Rostam Azizi ni mtu wa kuogopwa sana! Kwa wasiofahamu Mzee Aziz (baba yake Rostam) alikimbilia Uganda wakati wa vita ya wahujumu uchumi ilyoongozwa na Sokoine. Walikaa huko kama wakimbizi hadi panga la Mmasai lilipokwisha makali. Waliporejea hapa nchini wakaja na jazba na kuanza uhujumu upya lakini safari hii wakaamua kupata kinga ya kisiasa na wakuu wa nchi. Akahonga mpaka CCM wakampa uweka hazina wa chama cha Mwalimu! Matusi makubwa kwa mzee wa Kizanaki! Akaanzisha uswahiba na viongozi wa kisiasa, majeshi na usalama wa Taifa. Dili lilipokamilika wakaanza uhujumu uchumi upyaaaa! Huyu anapaswa kuwekewa alama ya X kama nyumba iliyojengwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara ili siku ikifika awajibishwe!

    ReplyDelete
  13. huyo rosta anaonekana ni mtu asiyependa amani, ni mtu wa malumbano tuu, tokea nimeanza kumsikia, sijawahi kusikia zuri kutoka kwake.

    samahani mimi siyo nahukumu, ila mwanadamu anapoingia kwenye ulingo wa siasa angalao lisikike hata jambo moja zuri. mimi nafikiri hata kushinda kwake jimboni ni uchakachuaji,pia kutumia kipato alicho nacho ili kuwahadaa wananchi.
    safari hii tetea hoja za wanachi kwenye bunge kwa bidii acha kukaa kimya (bADILIKA) pia penda kuwa mtu wa kuwapenda wengine, acha malumbano na UFISADI, wananchi wengi tumekuchoka.

    ReplyDelete
  14. ndugu rostam, nadhani kuwa sasa wewe ni mheshimiwa lazina uwe mtu wa kulingana na status ya uheshimiwa, usiwe kiongozi wa kushambulia wengine kwa mambo yasiyokuhusu(chuki nichukie moyo wangu niachie) ,kwani unaonyesha usivyokoma kisiasa,cha msingi jenga hoja za kutatua matatizo ya wananchi yaani kuondokana na umaskini uliokithiri, ujinga na maradhi, pia hoja za kudumisha umoja, upendo, na amani kwa wananchi kama ilani ya chama cha TANU

    ReplyDelete