07 November 2010

Waislam walalamikia mabucha ya 'kitimoto'.

Na Joseph Mwambije, Songea

WAISLAM wanaofanya biashara zao kwenye soko la Mazao Songea (SODECO)  Mkoani Ruvuma wamelalamikia kuwepo kwa mabucha ya kuuza
  nyama ya nguruwe kwenye soko hilo
na kuziomba ngazi zinazohusika kuyaondoa mabucha hayo na kuyapelaka nje ya mji.
 
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema kitendo hicho ni sawa unyanyasaji wa kidini na kwamba kinaweza kuzusha vurugu siku za usoni na kuhatarisha amani iliyopo na kuondoa ushirikiano uliopo baina  ya waislamu na Wakristo.
 
Katika barua yao iliyoandikwa Januari 7 mwaka huu kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Songea wanasema kitendo cha kuweka mabucha ya nguruwe  kwenye soko hilo ni
unyanyasaji dhidi yao kiimani na kinyume cha katiba.
 
Wamesema kuwa wageni wa ngazi mbalimbali wanapofika Songea ni lazima wafike mjini na wanapofika kwenye vibanda vya kuuzia chakula vya Mama  lishe vya hapo SODECO wamejikuta wamekula kwa kuwa iko sokoni hapo na hakuna  tahadhari ya kujulisha kuwa hiyo ni nguruwe hivyo wanabaki wamechukia kwa hasira.
 
“Hapa ni katikati ya mji, tujiulize mji gani Tanzania wanauza nguruwe sokoni, kwa kweli hatutendewi haki kabisa na ni aibu kwa Mkoa wanahoji katika barua yao hiyo kwenda kwa Mkuu wa Wilaya.
 
Katika barua yao nyingine waliyoiandika Januari 4  2010 kwenda Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Songea Mjini na Vijijini wameeleza  kuwa uwepo wa mabucha hayo
umekuwa kero kubwa kwao kwa muda mrefu na kufafanua kuwa mabucha hayo yako matano na Mama Lishe wako baraza hilo wanauza ugali pamoja na  nyamahiyo ambayo ni haramu kwa waumini wa dini ya kiislamu.
 
Barua hiyo inaeleza kuwa katika Mabucha hayo kuwa eneo la kukaangia nyama hiyo kwa kutumia kuni ambazo husambaza husambaza moshi soko  zima na kuwa kero nyingine na
kusababisha uchafu wa Mazingira. Pia katika barua hiyo wanasema walimwandikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Aprili 1 mwaka huu  lakini hakukuwa na majibu na
wakamuandikia Mkuu wa Wilaya naye hakutoa majibu.
 
Wanasema baada ya kuona hali hiyo wakakaa na Mzee Mustapha Songambele ambaye alizungumza na viongozi wa mkoa wakakubaliana pasiwepo  na mabucha ya aina hiyo
katikati ya mji pamoja na SODECO, lakini wanasema wanashangaa hakuna utekelezaji wa makubaliano hayo.
 
Katika Barua iliyoandikwa na BAKWATA Songea Mjini Oktoba 22 mwaka huu yenye Kumbukumbu namba BKT/WS/U,10/Vo11 kwenda kwa  Mwakilishi wa Waislamu hao wanaoomba kuondolewa kwa Mabucha sokoni hapo Bw. Shabani Gawaza  wameeleza kuwa katika uchuguzi
wao wamebaini Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wameshindwa kulipatia ufumbuzi suala hilo na kamwe hawawezi kulishughulikia kwa mazingira yaliyopo.
 
Barua hiyohiyo iliyosainiwa na Katibu wa BAKWATA Songea Mjini D. Y. Mikunga inaeleza kuwa Oktoba 21 mwaka huu waliazimia kulipeleka  suala hilo BAKWATA Taifa
kutokana na sababu wanazozijua na wamewaomba waislamu wawe na subira wakisubiri hatua zinazochukuliwa.
 
Naye Mwakilishi wa waislamu katika kushughulikia suala hilo ambaye anafanyia biashara zake kwenye soko hilo Bw, Shaban Gawaza alisema  kuwa wakati waislamu walipanga wote kuswali Msikiti wa Mkoa na wakitoka hapo kuvunja mabucha hao lakini walichukua hatua za kuwatuliza.
 
Alisema licha ya kuwatuliza lakini hadi sasa hakuna hatua madhubuti za kushughulikia suala hilo ambalo anasema lisiposhughulikiwa  linaweza kuzusha Mapigano ya kidini.
 
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambaye pia ni Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo  Dkt. Zuberi Kivo alisema kama mabucha  hayo yako kwenye soko hilo yapo kimakosa na afisa biashara ametoa leseni ya mabucha hayo kimakosa.
 
'Mimi nilidhani mabucha hayo ni ya ng'ombe ngoja niwasiliane na Afisa Afya nimwambie akakague ili tuweze kushulghulikia, lakini  uninukuu kama Mganga Mkuu wa Wilaya na umtafute Mkurugenzi mwenyewe aweze kukutolea  ufafafanuzi", alisema.
 
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na Afisa biashara wake walipotafutwa kwenye ofisi zao hawakuweza kupatikana kuzungumzia Sakata hilo.
 
Kwa upande wake Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kupitia Katibu tawala wake Dkt Anselm Tarimo amekiri kuyapokea malalamiko hayo na  kusema  mabucha hayo yako hapo kwa muda mrefu na hawawezi kuyahamisha na kwamba soko  hilo la mazao liliyakuta yakiwa yamejengwa kienyeji na sasa yamejengwa kisasa. 

2 comments:

  1. Walikuwa wamejificha wakati wa uchaguzi sasa wameshinda UDINI unaendelea kwa kari na ari mpya

    ReplyDelete
  2. sisi waislamu tumezidi kulalamika, kila jambo ni sisi tu. Hata kama nguruwe ni halamu kwetu lakini uhalamu huo usiwanyanyase wenzetu! Kama hatuli nguruwe si tusinunue,yaani hadi watu wote wajue kuwa hatuli nguruwe. Jamani dunia itatuchoka!

    ReplyDelete