07 November 2010

Mkakati waundwa kummaliza Sitta.

Na John Daniel  

KUNDI la watu wanaodaiwa kuwa ni mahasimu wa kisiasa linadaiwa kuanza mikakati mizito kuhakikisha linamwangusha Spika wa Bunge anayetea nafasi yake
Bw. Samwel Sitta.

Vyanzo vyetu ndani ya CCM makao Makuu vilieleza Majira Jumapili kwamba kundi hilo tayari limeanza kutekeleza mkakati wake wa kwanza wa kutuma watu wake kuwania nafasi hiyo ili kupambana  na Bw. Sitta.

Mkakati wa pili wa kundi hilo wa kumwangusha Bw. Sitta ulitajwa kuwa ni kushawishi wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho (CC) itakayokutana kati ya Novemba 10 au 11 mjini Dodoma kukataa jina Mbunge huyo wa Urambo Mashariki.

"Tayari watu wao wawili wamechukua fomu kupambana na Mhe. Sitta, lengo ni kuhakikisha wanapata watu hata 10 kuchuana naye ili wakifika kwenye Kamati Kuu waseme kwamba hafai na ili wananchi wasipate nafasi ya kuhoji kama ameonewa wataachwa wengi.

"Wameanza kuwazungukia wajumbe wa Kamati Kuu na wapo wazee wachache wanawaunga mkono akiwemo kigogo mmoja wa chama,"kilisema chanzo chetu ndani ya CCM.

Hadi sasa waliokwishachukua famu ya kupambana na Bw. Sitta katika nafasi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Naibu wake Bi. Anna Makinda, Bw. Andrew  Chenge, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Bw. Job Ndugai, Mbunge wa Afrika Mashariki Bi. Kate Kamba pamoja na Bi. Anna Abdallah.
 
Pia yumo Luteni mstaafu wa Jeshi la Wananchi Bw. Benedict Lukwembe pamoja na Mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari. Ilielezwa kwamba jambo kubwa linalomfanya Mbunge huyo machachari kuwa na upinzani mkali katika kiti hicho ni msimamo wake hasa katika mapambano dhidi ya ufisadi pamoja na kuwa upande wa wananchi katika masuala ya msingi.

Moja ya vitu vilivyotoa sura halisi ya msimamo wa Bw. Sitta kuhusu vita vya ufisadi ni mkataba wa Richmond uliosababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa, kujiuzulu.

Vita ya uspika dhidi ya Bw. Sitta vinadaiwa kuwa ni moja kati ya mikakati ya urais wa mwaka 2015 ndani ya CCM ambapo kundi linalompinga linaamini kwamba kuwepo kwake katika nafasi hiyo itawapa ugumu wa kufikia lengo hilo.

"Hao jamaa wanataka mtu wao wa kwenda kulinda maslahi yao na kuwasafisha, chini ya Mheshimiwa. Sitta hilo haliwezekani, wanazunguka na kutumia hela nyingi sana, juzi kwenye uchaguzi wametumia milioni 420 ili kumwangusha wakashindwa," kilisema chanzo chetu.

Majira Jumapili ilipomtafuta Bw. Sitta ili kujua ukweli wa madai hayo dhidi yake alikiri kuzisikia na kuweka wazi kuwa ni dalili mbaya kwa nchi kufikia hatua hiyo. "Hata mimi nimesikia taarifa hizo na nimepigiwa simu sana kuulizwa, lakini ninachoamini ni kwamba Mungu amekuwa akinisaidia sana katika mambo makubwa magumu,hata hilo atanisaidia,"alisema Bw. Sitta.

Alisema anawaamini wajumbe wa CC kuwa ni watu wenye busara na wanaopima alama za nyakati na kubaini mbinu chafu na kuweka wazi kuwa yeye bado ana imani kuwa watatenda haki bila kurubuniwa.

"Mimi naendelea na maandalizi yangu ya kawaida tu kusubiri kujadiliwa na kutolewa maamuzi, ila ninajihami, nimepita katika mambo magumu ndio maana wananchi wa jimbo langu wamenibatiza jina la chuma cha pua, hata hilo nitashinda tu, acha wajisumbue Watanzania si wajinga wanawaona na kuwasikia.

"Hivi sasa wameanza kutumia magazeti yao na mengine kunichafua kwa tuhuma za uwongo na kibaya zaidi wanasubiri tu ikifika muda wa uchaguzi muhimu kwangu ndio watunge uwongo wananchi wanawaona na Mungu anawaona,"alisema Bw. Sitta.

Uvumi wa kundi hilo kupambana na Bw. Sitta kwenye uspika ulianza tangu mwaka jana ambapo awali jimbo lake lilidaiwa kuandaliwa sh. milioni 400, huku Jimbo la Mbunge mteule wa Kyela Dkt. Harrison Mwakyembe ulitengewa bilioni 600 kuhakikisha wanaanguka katika kinyang'anyiro cha ubunge.

Kundi la Sitta iliyokuwa ikiwindwa na kundi hilo yumo pia Mbunge mteule wa Same Mashariki Bi. Anne Kilango Malecela, Mbunge wa mteule wa Simanjiro Bw. Christopher Ole Sendeka, aliyekuwa Mbunge wa Nzega Bw. Lucas Selelii pamoja na aliyekuwa mbunge wa Sikonge Bw. Said Nkumba.

2 comments:

  1. ukitaka kwenda mbinguni lazima ufe; hivyo kwa kuwa Uspika kwa Sitta si kifo, wanaotaka kumchaua lazima waharibike wao.

    mimi namfagilia Sitta

    ReplyDelete
  2. gazeti la halionekani kwenye mtandao kwa wakati; kwa kuwa watu wanalipenda sana, inawakera wanapofungua mtandao na kulikosa hewani;

    ReplyDelete