Na Elizabeth Mayemba
WACHEZAJI wa Yanga, wamempongeza Mdhamini Mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji kwa hatua yake ya kuwaita na kuwauliza matatizo yanayowakabili ikiwa
na kupewa nafasi ya kila mmoja kutoa ushauri wa nini kifanyike ili timu hiyo iwe tishio.
Hivi karibuni Manji alikuwa na kikao na wachezaji hao, kwa lengo la kutaka kujua ni nini kinachosababisha wacheze chini ya kiwango na kutaka kujua matatizo yanayowakabili.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, wachezaji hao walisema kitendo cha mdhamini huyo kuwaita na kuwauliza matatizo yanayowakabili, imewatia moyo na kuona wana kazi kubwa mbele ya safari, ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika michuano inayoakabili.
"Kwa upande wetu hatukutegemea hata kidogo kama mdhamini wetu anaweza kutuita ili aweze kujua matatizo yetu, ni kitu nadra sana katika soka letu la Tanzania," alisema mmoja wa wachezaji hao ambaye hakupenda kuandikwa gazetini.
Alisema kuitwa kwao na Manji kila mmoja ameweza kumaliza dukuduku lake, na ameahidi kufanyia kazi maoni ya kila mchezaji kwa lengo la kujenga timu bora itakayoleta upinzani katika ligi na michuano ya kimataifa.
Mchezaji huyo nyota katika kikosi hicho cha Jangwani, alisema kutokana na Manji kuwajali wana uhakika mzunguko wa pili watafanya vyema na hata kunyakua ubingwa.
Alisema ni maswali mengi waliyoulizwa ikiwa na kupewa nafasi ya kumshauri mdhamini huyo nini anatakiwa kufanya ili wachezaji wasiwe na manung'uniko tena.
Naye mchezaji mwingine wa timu hiyo, alisema Manji ni mtu mwelewa ambaye ameahidi kuyafanyia kazi maoni ya kila mchezaji bila kujali anacheza au la.
Alisema wito huo umekuwa na kubwa kwa Yanga, kwani kuna uhakika hata akikutana na viongozi ambao amepanga kukutana nao watajenga kitu cha msingi.
No comments:
Post a Comment