12 November 2010

AC Milan yakamata usukani Italia.

ROME, Italia

KLABU ya AC Milan, imepanda kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Italia, Serie A baada ya juzi kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Palermo, katika
Uwanja wa San Siro huku waliokuwa vinara Lazio, wakipata kichapo cha bao 1-0 ugenini dhidi ya timu iliyopanda daraja ya Cesena.

Pato alifunga goli la kuongoza kwa Milan kabla ya Armin Bacinovic, Kuwazisha kwa timu hiyo ya Sicili lakini, Zlatan Ibrahimovic alifunga bao lingine kwa penalti na Robinho akafunga la tatu katika dakika za mwisho.

Dakika ya 77, Milan ilizawadiwa panalti baada ya Massimo Ambrosini kuangushwa katika eneo la hatari.

Kocha wa Milan, Massimiliano Allegri  akikiri kuwa timu yake ilikuwa na bahati kwa kupewa penati kwa kuwa mshambuliaji huyo, aliguswa kidogo na kuanguka.

"Kuona tena kwenye televisheni ilionesha Ambrosini alijiachia kuanguka, lakini ninaweza kusema haikustahili kutolewa penalti," alisema na kuongeza kuwa mbalia na tukio hilo, lakini kila timu ilistahili kupewa panati mbili na mwamuzi ila hakufanya hivyo.

Lazio ilipoteza mechi ya pili mfululizo baada ya kufungwa Jumapili mabao 2-0 na Roma.

Marco Parolo alifunga bao pekee ikiwa zimesalia dakika tano, kabla ya mechi kuisha.

Mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Inter Milan wameshushwa kwenye msimao hadi nafasi ya nne baada ya kutoka sare kwa mara ya tano, katika mechi zao 11, ambapo Lecce ilitoka nyuma na kusawazisha goli walilotanguliwa kufungwa.

Diego Milito alifunga goli lake la tatu katika msimu huu dakika ya 76, lakini lilisawazishwa na Ruben Oliver.

Napoli, ilipanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo ,baada ya kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya Cagliari, balo lake likiwekwa kimiani na Ezequiel Lavezzi.

Juventus imeporomoka hadi nafasi ya tano, baada ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Brescia, ambapo Alessandro Diamant alisawazisha bao la
Fabio Quagliarella.

Licha ya kuanza vibaya katika msimu, Roma iliyo katika nafasi ya sita inazidiwa pointi tano tu na vinara wa ligi hiyo, baada ya kushinda mechi ya tatu mfululizo.

Simplicio alianza kufunga goli la kwanza katika mechi hiyo iliyoishia kwa matokeo ya ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Fiorentina katika Uwanja wa Stadio Olimpico huku, Marco Borriello akifunga magoli mawili. Alberto Gilardino alifunga goli moja.

No comments:

Post a Comment