11 November 2010

Samuel Sitta atemwa rasmi.

Anna Makinda, Anna Abdallah, Kate Kamba wapeta
Makamba asema lengo ni mwanamke aongoze bunge


Emmanuel Kwitema na Tumaini Makene
ULE mkakati uliokuwa ukisemwa muda mrefu wa kutaka kumng'oa Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta umepata baraka za
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumuweka kando na kuwapitisha wanawake watatu kuwania nafasi hiyo.

Wanawake waliopitishwa ni aliyekuwa Naibu Spika katika bunge lililopita, Bi. Anna Makinda, mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Bi. Anna Abdallah na mbunge mstaafu wa Afrika Mashariki, Bi. Kate Kamba.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kamati kuu ya CCM mjini Dodoma jana, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusuf Makamba alisema lengo la uamuzi huo ni kutoa fursa kwa mhimili huo kuongozwa na mwanamke kwa mara ya kwanza tangu uhuru.

Kwa uamuzi huo, waliotemwa na Spika Sitta, Mbunge mteule wa Bariadi Magharibi, Bw. Andrew Chenge, Bw. Job Ndugai,  John Maurice, Bw. Salim Kungulilo, Bw. Samuel Sitta, Bw. Benedict Lukwembe na Bw. Kazimbaya Makwega.

Awali, habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kuwa  mpambano wa kuwania kugombea nafasi za uspika na unaibu spika ndani ya CCM ulikuwa umesukiwa mikakati mikali ikitawaliwa na maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wa chama huku sifa kama vile uzoefu, utendaji kazi kwa maslahi ya nchi na wananchi vikiwekwa kando.

Ilielezwa kuwa kwa makusudi ya mikakati hiyo ni kuhakikisha wagombea wote katika nafasi hizo wanapatikana kwa maelekezo ya kundi fulani, ili kuweka watu wanaowataka kulinda maslahi yao na yale ya chama na serikali, hasa wakati wa mijadala mikali inayoihenyesha serikali, mara bunge likapoanza kukutana.

Kutokana na mikakati hiyo inayosemwa kuwa ni ya hali ya juu, ikiwa imepata baraka za uongozi wa juu ndani ya CCM, lengo likiwa ni kupata spika atakayeweza kulinda maslahi ya CCM zaidi, hususan kundi husika na kufanya nafasi ya Bw. Sitta kuwa ndogo kukosekana kabisa.

Habari zilizolifikia Majira jana wakati vikao vya ndani vya CCM vikiendelea na mchakato wa kuchuja majina hatimaye kupata matatu yatakayowasilishwa kwenye kamati wa wabunge wa CCM ili kupata moja litakalochuana na wagombea wa upinzani bungeni, zilihabarisha kuwa kuna kundi lilikuwa limejipanga kuhakikisha jina la Bw. Sitta halipenyi katika vikao vya chama na badala yake anachaguliwa mgombea mwingine.

Vyanzo mbalimbali vya habari kutoka ndani ya CCM vimelijuza Majira kuwa mkakati unaosukwa kwa uratibu wa baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM, umeshafanikiwa kujenga ushawishi kuwa mgombea uspika wa chama hicho anapaswa kuwa mwanamke, ambaye ameandaliwa (jina tunalo).

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo mikakati iliyokuwepo ilikuwa kuhakikisha Bw. Sitta hapitishwi na CCM kugombea uspika, bali nafasi hiyo ama iende kwa Bw. Andrew Chenge au mmoja wa wagombea wanawake ambao walikuwa wameandaliwa tayari, ikiwa ni pamoja na kushawishiwa kuchukua fomu, kisingizio kikiwa ni kupata mtu ambaye atarejesha utulivu ndani ya chombo hicho na zaidi kujali nafasi ya mwanamke.

Lakini kwa upande mwingine, mkakati wa kundi hilo ulikuwa umepata sababu ya kusema kuwa upande wa Sitta na Chenge zina mvutano, hivyo kutoa sababu ya kutafuta mtu wa tatu wa kusawazisha hali hiyo.

Vyanzo vya habari vya Majira vilizidi kuongeza kuwa mwangwi wa kutokubalika kwa Bw. Chenge ulisababisha wapanga mikakati waamue kujipanga upya kwani matazamio ya kupeleka wagombea wawili, mgombea wa mwanamke na mwanaume yalikuwa yameshindikana kwani uwezekano wa mwanamke kuchaguliwa ungelikuwa mkubwa kuliko mwanaume waliyemtaka, ambaye tayari ilishaonekana hakubaliki na umma ungeshangaa iwapo angechaguliwa kuwa spika.

"Isingekuwa tatizo, lakini mambo yamegongana...imetokea kuwa katika nafasi ya unaibu spika kwa CCM amejitokeza mgombea mmoja pekee, Bi. Jenista Mhagama, hivyo wakapiga mahesabu kuna uwezekano wa kupoteza moja ya nafasi hizo au zote kabisa, kwa sababu ingekuwa vigumu vikao vya CCM kuchagua spika na naibu wake, wote wawe jinsia moja, hasa kwa nyakati kama hizi za masuala ya usawa wa kijinsia.

"Sasa ukapangwa mkakati mwingine wa kuhakikisha mmoja wa wagombea mwanaume kati ya waliojitokeza kuwania uspika ambaye anaonekana kuwa ni tishio kwa yule mwanamke waliyemuandaa, ashuke chini na achukue fomu ya unaibu spika apambane na Jenista Mhagama, huko watampitisha huyo mwanaume, hivyo yule mwanamke anayewania uspika apita bila mgogoro," kilisema moja ya vyanzo vyetu vilivyo karibu na kinachoendelea ndani ya CCM.

Wakati hayo yakielezwa, taarifa kwa vyombo vya habari kutoka Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, iliyotumwa jana kwa vyombo vya habari ilisema kuwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho iliyokutana Novemba 9, mwaka huu chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu, Bw. Yussuf Makamba, imeongeza muda wa wanachama wa CCM kuchukua fomu za kuwania nafasi ya unaibu spika.

Taarifa hiyo ilisema kuwa muda wa mwisho sasa utakuwa ni Novemba 13 saa 10.00 jioni ambazo zitapatikana katika ofisi ya wabunge wa CCM iliyopo katika Ofisi ya Bunge mjini Dodoma.

"Awali muda wa mwisho ulikuwa tarehe 8/11/2010 saa 10.00 jioni. Majina ya walioteuliwa na vyama vya kugombea nafasi hiyo yanatakiwa kuwasilishwa Ofisi ya Katibu wa Bunge tarehe 15/11/2010. Kamati ya Wabunge wote wa CCM itakutana tarehe 14/11/2010 kuchagua jina moja la mgombea wa nafasi hiyo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya CCM.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Mrema aliliambia Majira kuwa chama hicho kimempitisha mmoja wa waasisi wa siasa za mageuzi na wakili maarufu, Bw. Mabere Marando kuwania uspika.

Bw. Marando ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, akiwa amejiunga na chama hicho mwaka huu, akisema kuwa aliamua kuahirisha kustaafu siasa za jukwaani na kuamua kurudi baada ya kufurahishwa na uamuzi wa Dkt. Willibrod Slaa kugombea urais wa Tanzania, kwa tiketi ya CHADEMA.

Amewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Rorya kwa miaka mitano, mwaka 1995 hadi 2000, kisha akawa mmoja wa wabunge wa mwanzo katika baraza la kwanza la kutunga sheria, Afrika Mashariki.

Jitihada za kupata jina la nani atasimama kuwania kiti hicho kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF) hazikufanikiwa baada ya kuwasiliana na mmoja wa viongozi walioko Dodoma, lakini akasema hawezi kuzungumza na akaomba apewe muda mpaka atakapomaliza kikao alichokuwa akihudhuria.

18 comments:

  1. Umechambua vizuri sana ndugu mwandishi uko makini sana. Nashukuru sana na wanachosahau ni kwamba nafasi hizo zinatakiwa zipate baraka za wananchi na si tu wabunge kwa kupitia uchama. Kumbuka kinachotakiwa ni maendeleo ya wananchi na si maendeleo ya vitambi fulani fulani.

    ReplyDelete
  2. Pole Sitta, tulikupenda, lakini Mungu kakupangia jingine, kumbuka likuepukalo lina kheri nawe, usijali! hata hivyo wakina mama nao wapewe nafasi, kura yangu kwa Makinda! wabunge nitilieni huko!

    ReplyDelete
  3. wabunge msfanye unafiki pigeni kura toka mioyoni mwenu, tunajua maslahi yapo lkn hata shetani uonea huruma wafusi wake wanapoadhibiwa na MUNGU, so nanyi lioneeni huruma taifa letu japo kwa kuchagua spika mwenye kufaa, kisha muendelee kutunyonya kama mlivyozoea.

    MUNGU AWALAANI WALE WOTE WATAKAOPIGA KURA KINAFIKI.

    ReplyDelete
  4. Pole Sitta, tulikupenda, lakini Mungu kakupangia jingine, kwa kweli hapo umeongea Sitta Baba yangu umshukuru Mungu kwani kuna alilokuepushiaa na Munngu atakuzidishia Aso hili ana lile, waache hao akina makamba wawatetee mafisadi mwisho wao ni 2015.

    ReplyDelete
  5. Hayo yote yasingempata Samwel Sita kama angekuwa na msimamo, unafiki wake umemponza. Angalia alivyokuja kuwasaliti wapambanaji waufisadi wakati wa kuhitimisha swala la Richmond. Alitakiwa afahamu nguvu ya mafisadi na kukomaa kwelikweli,lakini akaamua kuwa popo. Anastahili kuangushwa ili ajifunze ubaya wa unafiki.

    ReplyDelete
  6. Kwa hili na sisi wananchi tunanafasi ya kulonga kwani cc ni nani bwana!!Waheshimiwa wabunge fanyeni kweli kuthibitisha kuwa kitendo kilichofanywa na cc hakikuupenza uma wa watanzania kwa kumwacha sitta.Wabunge mpeni marando sasa uspika ili mambo yaende vyema lakini kama mtawapa hao waliopendekezwa na cc ninauhakika bunge lijalo halitakuwa nalolote bali kuleana tu.Pole sana sita mafisadi wamefanikiwa hatimaye kukuondoa.GOD IS GREAT!!!

    ReplyDelete
  7. siamini kama hoja iliyotolewa ya kuwapa wanawake nafasi ni ya kweli, hapa kuna kitu wanaficha, mbona nafasi ya urais hawakusema jinsia, waacha kuchezea watanzania, 2015 tutawaonesha tulikuwa tunamuhitaji sita, hao watakaowapitsha kwa masilahi ya ccm na mafisadi watakuwa wao, nilidhani uchaguzi huu umewafunza...

    ReplyDelete
  8. Pole sana Mh. sitta hiyo ishu ilipangwa toka muda wewe kuenguliwa uspika 2010, usijali huenda Mungu kakupangia nafasi nyingine,waache hao Mama tuone wataongozaje bunge la 2010? ila kura yangu ni kwa Makinda, wabunge nawaomba mlioene hilo sio mnachagua mwanamama anayejali maslahi ya ccm,na mafisadi, Sitta tulikupenda zaidi NAKUTAKIA MAISHA MAREFU NA YENYE BARAKA

    ReplyDelete
  9. Hongereni wanaCCM kwa ubinafsi katika kutetea chama chenu kuliko masilahi ya nchi na wananchi kama agenda ilikuwa wanawake mbona mliruhusu wanaume kuchukua fomu? Mmemtema Sitta kwasababu aliruhusu bunge kujadili mambo maovu ya serikali ya CCM. CCM msiwaamshe waliolala, wananachi wamelala ndo mana wameendelea kuwachagua ole wenu karibu usingizi wao unakwisha.

    ReplyDelete
  10. pole sana sita. hao ndo mafisadi wenye nchi yao.lakini mungu yuko upande wako.umetimiza wajibu wako.watanzania tuko pamoja na wewe.kazi tumeiona.

    ReplyDelete
  11. Nimezoea CCM wanajali sana aliepo madarakani amelize kazi alioinza.imekuaje Sitta hakufanya cha maana kwa akina makamba?

    Kafara zipo nyingi lakini ya binadamu inagharama kubwa sana! CCM kweli wapo tayari kubeba gharama ya kumwacha Sitta kwa maslahi ya taifa?

    Mkasa mwingine unaotonesha kutokuwepo uhuru wa siasa Tanzania; Jamaa angeamua kuomba Spika bila kupitia chama na ANGEPATA TU!

    Demokrasia inanyongwa hapo Tanzania.

    Hawa watatu watuweke wazi mikakati yao kutetea demokrasia hasa ya uhuru wa kuomba uongozi pasipo kulazimika kupata ridhaa ya watu wanaojiita CHAMA.

    ReplyDelete
  12. Matatizo yote ya nchi hii tunajitakia wenyewe. siku zote tunawaambia dawa ya kumaliza unafiki huu ni kuiondoa ccm madarakani.

    ReplyDelete
  13. Wabunge timizeni wajibu wenu taifa linaangamia kwa ufisadi kumbukeni mko bungeni kutuwakilisha wananchi wote watanzania na sio vyama vyenu.CCM wanajifanyia wanavyotaka wameshatuona sisi wote ni wajinga. Hakikisheni hamumchagui yoyote kati ya hao wanaowania uspika waliopendekezwa na CCM. Kwani Sitta ndiyo lilikuwa chaguo la Watanzania. Chagueni spika toka upinzani ili wasiendelee kutuchezea nchi hii ni yetu sote sio waopeke yao MUNGU NA AWALAANI WOTE WANAOTETEA NA KUSHABIKIA UFISADI

    ReplyDelete
  14. huyo mwanamke anayepewa hiyo nafasi nikwamba kunakitu sanasana maslahi ya chama cha familia na sio maslahi ya nchi,na huyo sita kwanini yeye jamani na wengine tupewe nafasi

    ReplyDelete
  15. Wabunge kuweni na msimamo mmoja,Anna Makinda ameshapita kupitia tiketi ya chama cha ccm, na Mabere Nyaucho Malando kupitia kambiya vyama pinzani,hivyo wabunge mkitaka nchi iendelee kiuchumi na kufichua mafisadi Mchague MABERE japokuwa Anna Makinda ananafasi kubwa ya kushinda kwa kutegemea chama chake kuwa na viti vingi vya bunge.

    Wana ccm na wabunge wapinzani nawaomba mchagueni Mabere ili tuweze kutokomeza mafisadi wanaoendelea kuliangamiza Taifa letu na kudai Sitta alikuwa akiwapa nafasi ya upendeleo wabunge pinzani kufiwachua Mafisadi ndio maana nafasi yake ipewa na mtu Mwanamke huyo. SITTA UNASIFA ZOTE ZA KUWA SPIKA POLE SANA WAMEAMUA WAKUFISADI TU.

    ReplyDelete
  16. Makinda anaweza akashindwa vile vile coz kuna wana CCM ambao hawapendi UFISADI wanaweza wakageuka kwa MABERE. Anna Makinda amepewa Bilion 1 ili asiwe anakubali hoja binafsi we unazani kachukua FOMU makusudi? Mafisad walishapanga kila kitu na kumpa bilioni.

    kwanza hafai hata bunge lililopita alikuwa nabore kishenziiiiiiiiiiii

    MUNGU TUNAOMBA UKASIMAME LENGO LA MAFISADI LISHINDWE KWA JINA LA YESU

    ReplyDelete
  17. Ni kweli Sitta angegombea uspika bila kupitia chama chochote angepita, maana anakubalika na wabunge wote pamoja na Watanzania kwa Wabunge na siku ya uchaguzi mtafakari nani anafaa kuwa spika wa bunge Makinda au Mabere? jibu lipo kwenu, ila ingefaa zaidi huyo mabere awe spika ili kuleta changamoto bungeni na kuwafichua mafisadi.

    ReplyDelete
  18. Kikwete anaanza kuonyesha sura yake hali ya kulipiza visasi. Na bado. Msishangae kwa jeuri yake akamteua tena Lowassa kuwa waziri au waziri mkuu licha ya kupigwa teke kwa ufisadi wake. Msishangae akina Chenge wakarejeshwa kwa mlango wa nyuma.
    Kilichofanyika Dodoma ni kuonyesha serikali ya kichakachuaji ilivyo madarakani kutetea maslahi ya wale walioiwezesha kuchakachua na Kikwete kushinda na si wananchi. Yetu macho.

    ReplyDelete