Na Elizabeth Mayemba
MCHEZAJI raia wa Ghana ambaye alikuja nchini kuichezea Yanga, Keneth Asamoah usajili wake bado umetanda giza kutokana na uongozi wa Yanga, hadi jana ulikuwa
bado haujajua hatima yake.
Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga, zilieleza Dar es Salaam jana kuwa tatizo lililojitokeza katika mzunguko wa kwanza huenda likajirudia kutokana na kasoro zinazojionesha kwamba huenda wakashindwa kumsajili kama awali.
"Kwa kweli suala la Asamoah, kuichezea timu yetu kwenye mzunguko wa pili bado ni tatizo, kuna vitu ambavyo tumevigundua vinavyoweza kuleta kasoro Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na tukanyimwa tena kibali chake," zilieleza habari hizo.
Habari hizo zilidai kuwa pamoja na dirisha dogo la usajili kufunguliwa, bado hakuna utaratibu wowote uliofanywa kuhakikisha mchezaji huyo anaichezea Yanga, kutokana na kasoro zilizojitokeza.
Zilidai hata hivyo kuanzia leo au kesho, uongozi wa klabu hiyo utajaribu kushughulikia tena suala hilo ili kupata ufumbuzi wa suala la mchezaji huyo anayecheza nafasi ya ushambuliaji.
Awali Yanga ilishindwa kumtumia mchezaji huyo, kutokana na kukosea usajili wake likiwemo jina la lake sababu iliyoifanya FIFA kushindwa kutoa kibali.
Kutokana na kushindwa kusajiliwa katika timu hiyo, mchezaji huyo ameendelea kuwepo nchini akisubiri mambo yake kukaa sawa na amekuwa akienda na Yanga kwenye mechi zake za mzunguko wa kwanza ambao umemalizika Jumapili na yeye kuondoka kurudi kwao Ghana kwa mapumziko.
No comments:
Post a Comment