11 November 2010

Njia za Vodacom Cycle zatangazwa.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Vodacom ambao ni waandaaji wa 'Vodacom Mwanza Cycle Challenge' jana wametangaza njia zitakazotumika kwenye
mashindano ya baiskeli ambayo yatakayofanyika Jijini Mwanza kesho na keshokutwa.

Akizungumza Jijini Mwanza jana, Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom, Rukia Mtingwa alisema mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na kuwaomba washiriki kujitokeza kwa wingi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), Godfrey Mhagama alizitaja njia hizo na kusema kwamba mbio za walemavu wanawake ambazo ni za kilometa 10, zitaanzia kiwanda cha soda cha Pepsi (SBC) na watageuzia eneo la Nyamanoro.

Alisema kwa upande wa mbio za kilometa 16 za walemavu wanaume pia zitaanzia SBC na watageuza eneo la Kisesa karibu na mashine ya mchele ya Ndakila.

Mhagama alisema kwa upande wa mbio za kilometa 80 kwa wanawake zitaanzia eneo la Nata na kwenda Bihayabyaga umbali wa kilometa 25.

Mwenyekiti huyo alisema kwa upande wa mbio za kilometa 196 wanaume  zitaanzia eneo la Nata, kwenda Bihayabyaga kupitia Bundilya.

Aliyataja maeneo ya tahadhari kwa wakimbiaji kuwa ni Mabatini, Igoma na Kituo cha basi cha Buzuruga kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watu.

Mashindano pia yamedhaminiwa na Alphatel, Knight Support, SBC kupitia kinywaji chake cha Pepsi.

No comments:

Post a Comment