10 November 2010

Shibuba ataka polisi kuharakisha upelelezi.

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MBUNGE mteule katika Jimbo la Maswa Magharibi mkoani Shinyanga kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. John Shibuda amelitaka
Jeshi la Polisi
wilayani Maswa kuharakisha upelelezi wa kifo cha mfuasi wa CCM Bw. Steven Kwilasa (26) ili ukweli uweze kufahamika.

Mbali ya kufahamika kwa ukweli juu ya kifo hicho, alisema hatua hiyo itaharakisha haki iweze kutendeka kwa watuhumiwa 11 wanaoshikiliwa na polisi hivi sasa wakituhumiwa kuhusika na kifo hicho kilichotokea Oktoba 21, mwaka huu katika kijiji cha Kizungu wilayani Maswa mkoani Shinyanga.

Bw. Shibuda alitoa rai hiyo juzi alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Mji wa Malampaka wilayani Maswa ambapo alisema pamoja na kutokea kwa tukio la kuuawa kwa
mwanachama huyo wa CCM, bado wahusika wakuu hawajafahamika waliokamatwa hawakuwepo katika eneo la tukio.

Alisema watu waliokamatwa ni wanachama wa CHADEMA peke yao licha ya kwamba vurugu hizo zinadaiwa zilihusisha wafuasi wa vyama viwili,CCM na CHADEMA.

“Kwa kweli binafsi naliomba jeshi la polisi liharakishe upelelezi wake juu ya kifo cha ndugu yetu Bw. Kwilasa, kifo hiki kina utata, watuhumiwa waliokamatwa kuhusiana na kifo hicho hawakuwepo eneo la tukio, lakini wamekamatwa na kuwekwa mahabusu.

“Lakini maelezo ya awali yanadai kuwa hawa ndiyo waliohusika na mauaji ya Bw. Kwilasa, lakini jambo la kusikitisha inadaiwa siku hiyo ya tukio pande mbili
zilikuwa zikipigana na wafuasi wanne wa CCM walijeruhiwa akiwemo marehemu Kwilasa, sasa iweje upande wa pili usiwe na majeruhi?” alihoji Bw. Shibuda.

Alisema mara baada ya kukamilika kwa shughuli za uchaguzi mkuu, kuna muhimu mkubwa kwa jeshi la polisi kuharakisha upelelezi wake wa kina juu ya tukio hilo na kama kuna
watu wa kupelekwa mahakamani wapelekwe ili haki iweze kutendeka bila upendeleo.

Oktoba 21, mwaka huu mwanachama mmoja wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Bw. Steven Kwilasa alikufa kutokana na kupigwa mawe katika vurugu zilizotokea katika Kijiji cha Kizungu wilayani Maswa baada ya kutokea vurugu kati ya wafuasi wa CCM na wale wa CHADEMA ambapo watu 12 akiwemo Bw. Shibuda walikamatwa.

Hata hivyo kufuatia uchunguzi wa awali uliofanyika ukiongozwa na Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, Bw. Shibuda aliachiwa huru baada ya kubainika hakuhusika katika vurugu hizo.

1 comment:

  1. Mimi hili la mauaji halinisumbui sana, naamini uchunguzi wa kina ambao ni wa kitaalamu zaidi ukitumika, watatiwa mbaroni wauaji na haki kutendeka.

    Kinachonisumbua mimi ni kujua ni adhabu gani anayopewa mtu anayemrukia OCD akiwa kazini na kumpiga mateke. Kama Kisena hatafunguliwa mashtaka au kama hatapatikana na hatia yoyote, itabidi kesi ya kikatiba ifunguliwe juu ya upendeleo kwa mafisadi.

    ReplyDelete