10 November 2010

Kificho arejeshwa uspika Zanzibar.

Na Mwajuma Juma, Zanzibar

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, jana walimrejesha tena Bw. Pandu Ameir Kificho (CCM), kuwa Spika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, katika uchaguzi
uliofanyika ndani ya baraza hilo.

Katika uchaguzi huo ambao ulisimamiwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Bw. Ibrahim Mzee Ibrahim, Bw. Kificho alijinyakulia wadhifa huo kwa kupata kura 45 na kumpita mpizani wake, Bw. Abass Juma Muhunzi (CUF) aliyepata kura 32. Kura moja iliharibika.

“Kutokana na matokeo haya sasa namtangaza rasmi Bw. Pandu Ameir Kificho kuwa Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa kipindi cha miaka mitano,” alisema.

Akitoa shukrani zake mara baada ya kuchaguliwa, Spika Kificho aliwashukuru wajumbe hao kwa kumrejesha tena kuwa mtumishi wao, na kuwaahidi kuwa atafanya kazi ya ziada ili aweze kuwatumikia.

“Ninawashukuruni nyote kwa moyo wenu wa kunichagua kuwa mtumishi wenu na ninatoa ahadi kuwa nitafanya kazi ya ziada ili kuweza kuwatumikia wote,” alisema.

Hata hivyo, akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Spika huyo aliwataka wajumbe hao kuulinda mfumo huo hasa kwa vile baadhi yao walishiriki kikamilifu katika marekebisho ya kumi ya katiba yaliyofanywa na baraza hilo katika kikao cha saba cha baraza hilo.

Alisema kuwa kitendo cha wananchi kupiga kura ya ndio na kukubali kuwepo kwa mfumo huo, kunapaswa kulindwa na kutekelezwa na kila mmoja wao.

“Kwa maana hiyo tujue kwamba hivyo ndivyo wananchi walivyotaka na tunapaswa kutekeleza,” alisema Bw. Kificho.

Mara baada ya kufanyika uchaguzi huo wajumbe hao wa baraza la wawakilishi wapatao 79 walikula kiapo cha uaminifu cha kuitumikia Zanzibar ndani ya baraza hilo kwa kipindi cha miaka mitano, katiba za Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuchaguliwa kwa Spika Kificho kunamfanya kuliongoza baraza hilo kwa vipindi vinne mfulululizo tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi Tanzania mwaka 1992.

No comments:

Post a Comment