10 November 2010

Maalim seif, Balozi Idd makamu wa Rais Zanzibar.

Na Ali Suleiman na Tumaini Makene.

RAIS wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amefanya uteuzi wa makamu wake wawili, ambapo amemteua Bw. Seif Sharif Hamad kuwa makamu wa kwanza wa Rais na
Balozi Seif Ali Iddi kuwa makamu wa pili wa rais.

Uteuzi huo ambao umemwacha nje ya uongozi wa juu, aliyekuwa Waziri Kiongozi wa serikali iliyopita, Bw. Shamsi Vuai Nahodha, unakamilisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo ilipata baraka zake katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Wawakilishi, ulioitishwa katikati ya mwaka huu kubadili Katiba ya Zanzibar ili kuwezesha uundwaji wa serikali hiyo na utaratibu wa utekelezaji wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu Zanzibar, Rais Shein amefanya uteuzi wa makamu wa kwanza wa rais, kutokana na mamlaka ya kikatiba aliyonayo kama yalivyoainishwa katika kifungu 39 (1),(2) na (3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Rais Shein pia ametumia mamlaka yake katika Katiba ya Zanzibar, kifungu cha 39(1),(2) na (6) kumteua Balozi Idd kuwa Makamu wa Pili wa Rais, huku uteuzi huo ukianza rasmi Novemba 9, mwaka huu. 

Serikali hiyo ya Umoja wa Kitaifa ambayo sasa itaongozwa na Rais Shein, Makamu wa Kwanza Bw. Hamad na Makamu wa Pili , Balosi Iddi ambaye ndiye mtendaji na msimamizi wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi, ni matokeo ya maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa kati ya vyama vya siasa vya CCM pamoja na CUF kwa lengo la kumaliza siasa za chuki na uhasama Tanzania Visiwani.

Bw. Hamad alikuwa mgombea wa Chama cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliomalizika mwezi jana ambapo alishika nafasi ya pili baada ya kuangushwa na mpinzani wake Dkt. Shein kwa tofauti ya asilimia 0.2 ya kura zilizopigwa. Dkt. Shein alipata asilimia 50.1 na Maalim alibuka na asilimia 49.9.

Bw. Hamad anayo historia ya kushiriki katika chaguzi zote kuu tangu kuanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, akiwa pia amewahi kushiriki uchaguzi enzi za chama kimoja, ambapo alishindwa kwa taabu na aliyekuja kuwa rais wa nne wa Zanzibar, Hayati Idrisa Abdulwakil Nombe katika uchaguzi wa mwaka 1985.

Aliwahi kutumikia nafasi ya Waziri Kiongozi Zanzibar wakati akingali CCM, wakati wa Serikali ya Rais wa tatu, Mzee Ali Hassan Mwinyi na pia wakati wa Hayati Abdulwakil, kabla hajafukuzwa ndani ya chama hicho mwaka 1987.

Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, makamu wa pili wa rais atakuwa ndiye mtendaji mkuu wa shunguli za Serikali na pia katika Baraza la Wawakilishi. Kabla ya uteuzi mpya, Balozi Seif alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete lililopita.

Katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni, Balozi Seif aliibuka na ushindi mkubwa katika jimbo la uchaguzi la Kitope, akiwa mwakilishi wake tangu mwaka 2005.

Balozi Iddi alipata kuwa balozi wa Tanzania nchini China kwa muda mrefu. Mara baada ya kurudi nyumbani mwaka 2000  aliteuliwa kuongoza idara ya mambo ya nchi za nje ya Zanzibar na kuwa mkurugenzi katika kipindi kifupi.

Aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ofisi ndogo Zanzibar Kisiwandui Juni, mwaka 2000 hadi mwaka 2002.

No comments:

Post a Comment