11 November 2010

Uingereza sasa yairuka Takukuru kuhusu Chenge.

Yasema kashfa ya rada haijafika mwisho
*Kesi yake kuanza kunguruma Novemba 23


Na Tumaini Makene
SAKATA la tuhuma za mlungula linazomkabili aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Andrew Chenge juu ya ununuzi wa rada linaonekana
bado bichi, baada ya Serikali ya Uingereza kuweka bayana kuwa kwa sasa haiwezekani kuhitimisha suala hilo na kutoa uamuzi kuwa mtu yeyote kuwa ana makosa au la.

Taarifa hiyo ambayo inaonekana kuwa ni sawa na kukanusha taarifa nyingine ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) juu ya kashfa ya ununuzi wa rada, iliyotolewa juzi ikimsafisha Bw. Chenge, imeweka wazi kuwa katika hatua iliyofikiwa sasa katika uchunguzi, suala hilo halijafikishwa mahakamani kwa uamuzi.

Taarifa ya TAKUKURU iliyotolewa hivi karibuni ilimsafisha Bw. Chenge ambaye pia ni mbunge mteule wa Bariadi Magharibi ikisema kuwa uchunguzi uliofanywa na wao pamoja na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO), umegundua kuwa mwanasheria mkuu huyo wa serikali ya awamu ya tatu, hakuhusika.

Lakini Ubalozi wa Uingereza jijini Dar es Salaam ulikata mzizi wa fitna na kusema, "Serikali ya Uingereza inatambua taarifa ya TAKUKURU iliyotolewa Novemba 8, mwaka huu juu ya kesi inayohusu kampuni ya BAe (British Aerospace Systems) ya suala la rada. Suala hilo bado halijafikiwa uamuzi mahakamani, hivyo haiwezekani kutoa uamuzi wa aina yoyote kwa wale wote waliohojiwa wakihusishwa na tuhuma hizo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Serikali ya Uingereza

Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Februari 5 mwaka huu, SFO  ilitoa taarifa ya kufikia makubaliano na kampuni ya BAE, baada ya uchunguzi katika mkataba na serikali ya Tanzana.

Ilisema katika makubaliano hayo, kampuni ya BAe ilikiri kufanya makosa katika taarifa sahihi za hesabu zake hapa nchini, na iko tayari kukiri kosa hilo na kulipa kiasi cha paundi ya Uingereza milioni 30 (sh bilioni 72) kama adhabu na fidia kwa Tanzania.

"Makubaliano hayo, baina ya SFO na BA yalihitimisha shughuli za uchunguzi zilizokuwa zinafanywa na taasisi ya SFO. Hata hivyo, kwa kuwa makubaliano hayo hayajathibitishwa na mahakama si sahihi kwa sasa kusema kuwa uamuzi huo umepitishwa," ilisema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa usikilizwaji wa kesi hiyo utaanza Novemba 23 mwaka huu ambapo uamuzi wa kuthibitisha makubaliano hayo utatolewa.

Hivi karibuni, Bw. Chenge akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, kuhusu hatua yake ya kuwania uspika wa bunge, kupitia CCM, alisema kuwa hahusiki na tuhuma za rushwa katika ununuzi wa rada unaohusishwa na umiliki wa akaunti nje ya nchi yenye kiasi cha sh. bilioni 1, akisema kuwa kwa ufahamu wake jalada hilo lilishafungwa ndani na nje ya nchi.

Badala yake Bw. Chenge alisema akaunti hiyo ni ya asasi isiyo ya kiserikali inayohusika na misaada kwa watoto yatima na kujigamba kuwa taasisi za uchunguzi zikiwamo TAKUKURU na SFO, zilibaini kwamba haina harufu ya rushwa kama ambavyo amekuwa akituhumiwa kwa muda mrefu sasa, hata kupekelea kujiuzuru uwaziri wa miundombinu mwaka jana.

Lakini hata hivyo Bw. Chenge aligoma kutaja jina la asasi hyo wala uongozi wake, zaidi ya kusema kuwa wadhamini wa taasisi hiyo ni yeye na mkewe, aliyemtaja kwa jina la Tina Chenge.

7 comments:

  1. TULIJUWA KUWA TAKUKURU WAMEMBEBA HUYU CHENGE, MAANA DUNIA YA LEO IKO WAZI IWEJE KESI IISHE, AU IFUNGWE TUSIJUWE AJUWE HOSEA TU NA CHENGE? KWA HILI NA HAYO MENGINE YALIYOFUMBIWA MACHO NA SERIKALI,NI WAZI HOSEA HANA USAFI NA SI MWADILIFU INABIDI AJIUZULU AU RAISI AMWAJIBISHE KUNA KUBEBANA KWA MANUFAA YA WACHACHE.HATA HIYO ASASI ISIYO RASMI ANAYODAI NI YAKE NA MKEWE ICHUNGUZWE NA IFATILIWE NA KAMPUNI YA NJE AU ISIWE HII TAKUKURU MAANA IMEKUWA KWA CHENGE HAINA UAMINIFU

    ReplyDelete
  2. Wakati umefika kwa Hosea kujiuzuru! tumesubiri sana hilo halikutokea, lakini sasa bora akae pembeni kusafisha hicho chombo, la sivyo hatuna imani nacho tena! kipo kwa maslahi ya mafisadi tu!

    ReplyDelete
  3. Hosea inabidi hawajibishwe kwani ana hudumu ktk sehemu muhimu sana ya nchi yetu ili kuondoa doa kubwa la nchi yetu yeye anakuwa muongo na si muwazi!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  4. Maelezo ya Hosea yanakwenda sambamba na Chenge.Hosea amemsafisha Chenge ili apite kwenye kugombea uspika.Kikwete amfute kazi Hosea au asimamishwe na ufanywe uchunguzi uhusiano wa Hosea na Chenge.
    Uingereza imemruka Hosea kwa kutoa taarifa ya uongo.
    Hosea asipojiuzulu au kfutwa kazi wananchi watakosa imani na TUKURURU.

    ReplyDelete
  5. TAKUKURU HAINA LOLOTE NI KIINI MACHO TU,HAITUSAIDII CHOCHOTE NA HAIKO KWA MANUFAA YA MTANZANIA WA HALI YA CHINI.TAKUKURU IMEKUWA KIJIWE CHA KUGAWANA RUSHWA NA KUWALINDA MAFISADI.MMEKOSA HESHIMA KWA UMMA NA SIJUI NI NANI HATAWASAFISHA.

    ReplyDelete
  6. HOSEA TUTAMLAUMU BURE NDUGU ZANGU KAKALIA KUTI KAVU HASIPO UNGA MKONO ...... NAYE ATAKUWA MBUZI WA KAFALA KAMA SITA ALIVYOTOSWA.

    TUELEWE SIASA ZA NCHI YETU NI ZA MIZENGWE NA FITINA.UKITUNGIWA FITINA HUTOKI.

    ReplyDelete
  7. TAKUKURU IMETIA AIBU TENA,
    TAKUKURU IVUNJWE HARAKA IWEZEKANAVYO.
    TAKUKURU INASABABISHA KINYAA!
    POLISI IIMARISHWE ILI IFANYE KAZI ZINAZOFANYWA NA TAKUKURU.

    ReplyDelete