* Awatema Mgosi na Tegete
Na Elizabeth Mayemba.
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' Jan Paulsen ameteua kikosi cha wachezaji 22 kwa ajili ya michuano ya Kombe la
Chalenji akiwemo, Gaudence Mwaikimba huku Mussa Hassan 'Mgosi' akitemwa.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 27 mwaka huu, ambapo Kilimanjaro Stars iliyopangwa kundi A watafungua dimba na timu ya Zambia 'Chipolopolo.
Akitangaza kikosi hicho Dar es Salaam jana, Poulsen alisema amezingatia vigezo vyote katika kuteua kikosi hicho, ikiwemo uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Aliwataja wachezaji aliowaita kuwa ni Juma Kaseja, Shaaban Kado na Said Mohammed, mabeki Shadrack Nsajigwa, Erasto Nyoni, Stephano Mwasika, Shamte Haruna, Idrissa Rajab na Juma Nyosso.
Viungo ni Henry Joseph, Shaaban Nditi, Nurdin Bakari, Jabir Aziz, Nizar Khalfan, Mohammed Banka, Kigi Makassy na Salum Machaku, washambuliaji ni Dan Mrwanda, John Boko, Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngassa na Mwaikimba.
Poulsen alisema katika kikosi chake cha Stars atawakumbuka sana wachezaji wake, Nadir Haroub 'Cannavaro', Agrey Morris, Selemani Kassim na Abdi Kassim ambao wameitwa kuunda kikosi cha Zanzibar Heroes.
"Ni wachezaji wazuri ambao wataleta upinzani mkubwa katika kikosi chao, lakini kutokana na tofauti kubwa iliyopo kwenye michuano hii, sina budi kukubali matokeo," alisema Poulsen.
Kocha huyo alisema si kama kikosi hicho amekiteua moja kwa moja, isipokuwa atafanya hivyo tena mara baada ya mechi ya kirafiki ya kimataifa inayotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kuchezwa, kwani ataweza kugundua kasoro.
"Mechi hiyo ya kirafiki ndiyo itakayonipa mwanga zaidi katika kuchagua tena kikosi kwa ajili ya michuano hiyo, kuna wachezaji wageni ambao natakiwa kuwajaribu," alisema
Wachezaji ambao wameachwa katika kikosi hicho ni Mgosi, Kelvin Yondani na Jerson Tegete.
Wakati huo huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Sunday Kayuni alisema awali walikuwa wacheze mechi hiyo ya kirafiki ya kimatifa na Burundi, lakini wamekataa dakika za mwisho.
"Mwanzo walitukubalia vizuri kwa masharti kwamba tugharamie kila kitu, lakini jana kabla ya mkutano na waandishi wa habari, walileta taarifa kamba hawawezi kucheza kwa sababu wachezaji wao wa kimataifa hawapo, hivyo tumetuma maombi tena Kenya na Ethiopia," alisema Kayuni.
No comments:
Post a Comment