10 November 2010

Kayuni ajichanganya kwa Kaseja.

Na Mwandishi Wetu

SAKATA la kipa wa timu ya Simba, Juma Kaseja limezidi kuchukua sura mpya baada ya kubainika kwamba Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Sunday Kayuni kutoa taarifa tofauti na aliyoisaini kwenda kwa timu hiyo.

Kayuni, Ijumaa iliyopita, alikaririwa alieleza kwamba Kaseja amefungiwa michezo mitatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 baada ya kubainika kwamba hakusalimiana na Mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro wakati timu yake ilipoumana na Yanga jijini Mwanza wakati si kweli.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kayuni alikiri kutoa taarifa kimakosa kwani taarifa aliyoisaini kwenda Simba ilieleza kwamba Kaseja hakusalimiana na wachezaji wa Yanga na si mgeni rasmi.

''Najua watu wana kiu kubwa ya kujua suala la Kaseja, adhabu itabaki palepale ila maelezo yaliyotolewa ndiyo yatakayobadilika, nilitoa maelezo kimakosa tofauti na yale niliyoyasaini katika barua niliyoipeleka Simba," alisema Kayuni.

Alisema Kaseja akiwa nahodha baada ya kumkaribisha mgeni rasmi alipaswa awaongoze kwa wachezaji, lakini hakufanya hivyo badala yake alikwenda moja kwa moja kwenye benchi la wachezaji wa akiba la timu yake.

Akizungumzia kuhusu suala la mchezaji kupewa adhabu kwa kukataa kusalimiana na mgeni rasmi, Kayuni alisema si lazima lakini kama atakuwepo uwanjani na akaamua kushuka ili kusalimiana na wachezaji, kanuni za mashindano husika zitafuatwa na ndiyo maana adhabu ya Kaseja ipo pale pale.

No comments:

Post a Comment