Na Addolph Bruno
TIMU ya taifa ya pool imeondoka jana kwenda nchini Ufaransa kushiriki mashindano ya dunia ya mchezo huo yatakayoanza kuchezwa kesho mpaka Novemba 13
, mwaka huu.
Timu hiyo imeondoka ikiwa na wachezaji saba ambao ni Vailet Mrema, Ali Akbal, Mohamed Ibu, Felix Atanas, Goffrey Mhando, Omari Akida na Issa Mkindi.
Msafara huo utaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Pool Tanzania (TAPA), Fred Mushi.
Akizungumza kabla ya kuwakabidhi bendera wachezaji hao, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana, aliwataka wachezaji hao kurudi na ushindi.
Rugimbana alisema ushindi watakaoleta utamsaidia Rais Jakaya Kikwete, kusherekea kuchaguliwa kuiongoza tena nchi kwa kipindi cha miaka mitano.
"Ushindi wenu ni muhimu kwa taifa, hasa kwa rais wetu mpenda michezo, mkifanikiwa mtakuwa mmemwongezea furaha sana," alisema.
Rugimbana aliwataka wachezaji hao kuzingatia nidhamu na kudumisha utamaduni wa Tanzania katika mashindano hayo.
Kwa upande wake Meneja wa Bia ya Safari Lager, Fimbo Butallah, ambao ni wadhamini wakuu wa timu hiyo, alisema wamekamilisha taratibu zote za safari, hivyo wanatarajia wachezaji watajituma katika mashindano hayo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Mzambia Denis Lungu, alisema ana imani kubwa kwa timu yake kurejea nyumbani na ushindi kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya.
"Watanzania wategemee ushindi, maandalizi tuliyofanya ni mazuri, nina imani tutafanya vizuri," alise.
Timu hiyo itaanza kutupa karata yake ya kwanza kesho dhidi ya wenyeji Ufaransa ikiwa imepangwa Kundi A, lenye timu za Wailes, Scotland, Uganda, Morocco, Gibrita, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na wenyeji Ufaransa.
No comments:
Post a Comment