Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa klabu ya Yanga umeshangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kushindwa kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi wa
Kagera Sugar aliyemfanyia vurugu Kocha Kostadin Papic.
Yanga wameshangazwa na TFF kuwaadhibu kwa makosa waliyofanya, lakini waliyofanyiwa, yameachwa kabisa.
Hatua ya Yanga kutoa kauli hiyo, imetokana na kupigwa faini ya sh.500,000 na Kamati ya Mashindanbo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), na kumfungia kipa wao Mserbia Ivan Knezevic, kwa kosa la kumtolea lugha chafu mwamuzi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu ya Yanga, Louis Sendeu, alisema TFF macho yao yote yameelekezwa Yanga kuangalia makosa wanayofanya.
Alisema mara nyingi wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya utovu wa nidhamu, lakini Kamati hiyo imeshindwa kuwaadhibu wahusika.
"Hakuna hatua ambayo TFF wameichukua dhidi ya kiongozi wa Kagera Sugar ya kumfanyia vurugu kocha wetu, pia mechi dhidi ya Simba, mashabiki wanaosadikiwa kuwa wa Simba, walivunja kioo cha gari la wachezaji wetu, lakini yote haya hawayaoni," alisema Sendeu.
Alisema kwa kuwa wanajua klabu yao ina fedha, ndio maana wanapenda kuwatoza faini.
Sendeu alisema kuna matukio mengi ambayo klabu yao imekuwa ikifanyiwa, hawaoni maamuzi yoyote yanayochukuliwa.
Alisema wao hawakatai mchezaji wao kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu, wanashangaa ni kwanini wanapofanyiwa vitendo vya utovu wa nidhamu, hakuna hatua zinazochukuliwa.
No comments:
Post a Comment