09 November 2010

Njoolay atuma rambirambi kwa waliokufa maji.

Na Juddy Ngonyani, Sumbawanga

MKUU wa Mkoa  wa Rukwa, Bw. Daniel ole Njoolay ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu waliokufa na wale zaidi ya kumi wanaohofiwa kufa
maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama katika Ziwa Tanganyika.

Bw. Njoolay alitoa rambirambi hizo wakati alipozungumza Majira njia ya simu jana kutoka Dar es Salaam ambapo alisema kuwa alipokea taarifa za ajali hiyo kwa mshtuko na simanzi kubwa.

Kutokana na ajali hiyo ameagiza mamlaka husika kufanya uchunguzi wa kina ili sheria ichukue mkondo wake.

Katika ajali hiyo watu watano wakiwemo watoto wanne na wengine zaidi ya kumi wanahofiwa kufa maji baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kupasuka na kuzama katika Ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani hapa.

Watoto hao waliokufa maji wanakadiriwa kuwa na umri kati ya  miezi kumi na moja na miaka sita.

Habari za uhakika zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Polisi mkoani hapa,zimeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 11 jioni katika maeneo ya Kijiji cha ikitokea  Kijiji cha Kabwe kwenda Kijiji cha Kalila kilichopo mwambao wa Ziwa Tanganyika.
 
Watu 21 waliokolewa kutokana na jitihada za wavuvi waliokuwepo maeneo ya karibu na wengine  zaidi ya kumi hawajulikani walipo na wanahofiwa kufariki  kwa  maji  baada ya kupasuka na kuzama kwa boti hiyo.

Wakati huo huo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Bw. Isuto Mantage, aliseama kuwa jitihada za kusaka watu hao zaidi ya kumi ambao wanahofiwa kufariki kwa maji inaendelea ambapo Jeshi la Polisi wilayani Nkasi kwa kushirikiana na wananchi wanaendelea kutafuta miili hiyo.
 
Kamanda Mantage pia ametoa rai kwa wavuvi na wananchi wengine wa vijiji vya jirani kutoa taarifa iwapo miili ya watu hao itaonekana ikielea majini.

No comments:

Post a Comment