Na Elizabeth Mayemba
MDHAMINI Mkuu wa Klabu ya Yanga, Yusuf Manji jana alikuwa na wachezaji wa timu hiyo, kupanga mikakati ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara
na michuano ya Kombe la Shirikisho (CAF).
Kikao hicho kiliwahusisha mdhamini huyo na wachezaji pekee, bila ya kuwepo Kocha Mkuu wala viongozi wa klabu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Manji alisema ameamua kukutana na wachezaji pekee, ili kujua matatizo yanayowakabili na nini kifanyike, ili waweze kufanya vizuri katika michuano inayowakabili.
"Siwezi kutibu ugonjwa upande mmoja tu, wachezaji ndiyo wanaocheza hivyo itakuwa vizuri nikijua nini tatizo linalosababisha wasicheze vizuri na nini kiboreshwe, ili wafanye vizuri katika ligi na michuano ya kimataifa na waseme ni safu gani iongezwe makali," alisema Manji.
Alisema huwa anapenda kuzungumza na pande zote, viongozi, makocha na wachezaji na kila mmoja amekuwa akiitwa kivyake, lengo ni kutoa uhuru kwa mtu kuchangia lile analojisikia.
Manji alisema kwa upande wa wachezaji, pia alitaka kujua kama mazoezi wanayoyafanya yanatosha na endapo wanamfurahia kocha, kwani hawezi kutibu ugonjwa upande mmoja.
Mdhamini huyo alisema, anaimani kubwa kikao cha jana kitaweza kuleta mwanga mzuri katika michuano inayowakabili, kwa kuwa atakuwa tayari ameshajua ugonjwa mzima wa timu.
Wakati huo huo, kambi ya wachezaji wa Yanga ilivunjwa jana na kuhurusiwa kurudi makwao.
Msemaji wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema baada wa wachezaji hao kupewa likizo watatakiwa kuripoti tena Novemba 27, mwezi huu kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Shirikisho.
"Wachezaji wote wakishawasili Novemba 27, wale wapya ambao tutakuwa tumewasajili dirisha dogo, tutaanza pia kuwafanyia mazoezi ili kocha aweze kusoma uwezo wao," alisema Sendeu.
No comments:
Post a Comment