Na Addolph Bruno
UONGOZI wa Klabu ya Azam, unatarajia kutangaza kocha mpya wa timu yao keshokutwa baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kuyafanyia kazi majina ya
makocha waliotuma maombi ya kuwania nafasi hiyo.
Azam inatarajia kumtangaza kocha mpya baada ya kukatisha mkataba na aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Mbrazil Itamar Amorin wiki iliyopita.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Idrisa Nassoro alisema awali walipata idadi kubwa ya makocha kutoka sehemu mbalimbali hivyo uongozi wa juu uliamua kupitia sifa zao ambapo wamepitisha majina matatu watakayoyafanyia kazi.
"Kutokana na uwingi wa maombi ambayo tuliyapata, bodi ya wakurugenzi ilikutana juzi na kupitia maombi ya makocha hao na sifa zao na waliamua kupitisha majina matatu, kwa hiyo Jumamosi nadhani tutakuwa tayari kumtangaza kocha," alisema Idrisa.
Hata hivyo Nassoro hakuweza kutaja majina ya makocha waliopitishwa katika kikao hicho akisisitiza kuwa isingekuwa vizuri kufanya hivyo.
Awali baada ya kukatishwa kwa mkataba na Itamar klabu hiyo ilianza kupokea maombi kutoka kwa nchi mbalimbli zikiwemo Uganda, Sweden, Malawi, na Denmark.
Mbali na hilo, Nassoro alisema uwanja mpya wa klabu hiyo ambao unajengwa huko Chamanzi, Mbagala jijini Dar es Salaam upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Alisema kuanzia Desemba 20 wanatarajia kuanza kuweka nyasi bandia katika uwanja huo.
No comments:
Post a Comment