07 November 2010

Meya, madiwani watano waangushwa Shinyanga.

Na Suleiman Abeid,  Shinyanga
 
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga mjini kimepata pigo baada ya wagombea wake sita katika viti vya udiwani akiwemo aliyekuwa
Meya na naibu wake kuangushwa na wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
 
Katika uchaguzi uliomalizika wiki iliyopita wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM katika kata za Kambarage, Kitangili, Ibadakuli, Ngokolo, Ndala na Masekelo waliangushwa vibaya na wagombea wa CHADEMA ambapo kwa mara ya kwanza tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe hapa nchini Manispaa ya Shinyanga itakuwa na madiwani kutoka vyama vya upinzani.
 
Katika kata ya Kambarage aliyekuwa Meya wa Manispaa kwa tiketi ya CCM, Bw. Hassan Mwendapole aliangushwa na mgombea wa CHADEMA, Bw. Nyangaki Shilungushela ambapo pia aliyekuwa Naibu Meya katika Manispaa hiyo, Bi. Moshi Kanji alishindwa na mgombea wa CHADEMA, Bw. George Kitalama.
 
Huko wilayani Meatu katika Kata ya Bukundi aliyekuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya CCM katika kipindi kilichopita Bw. Joseph Masibuka amefanikiwa kutetea nafasi yake hiyo kwa mara nyingine kwa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Bw. Masibuka alijiengua ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) mara baada ya kukamilika kwa zoezi la upigaji kura za maoni ndani ya chama hicho ambapo pamoja na kuibuka
mshindi wa kwanza, lakini vikao vya uteuzi vilikata jina lake na kumteua aliyekuwa mshindi wa tatu.
 
Kufuatia ushindi huo, Bw. Masibuka alisema atahakikisha anatekeleza ahadi zote alizoziahidi kwa wananchi wakati wa kipindi cha kampeni bila ya ubaguzi wa aina yoyote wala kinyongo kwa viongozi wake wa zamani wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

No comments:

Post a Comment