NEWYORK, Marekani
MCHIMBA madini raia wa Chile, ambaye alikwama chini ya mgodi kwa siku kadhaa akisubiri kuokolewa, Edison Pena, amefanikiwa kumaliza mbio za
New York City Marathon.
Mchimba madini huyo, alimaliza mbio hizo juzi huku akiwa anakabiliwa na matatizo ya goti na kumlazimu kumaliza mbio hizo za kilometa 42.4 kwa kutumia muda chini ya saa sita.
Akizungumza muda mfupi, baada ya kumaliza mbio hizo alisema aliamua kushiriki, ili kuwahamasisha wengine hususan watoto kukimbia.
Mchimba madini huyo mwenye umri wa miaka 34, aliokolewa mwezi uliopita pamoja na wachimbaji wenzake 32 kutoka chini ya mgodi, uliobomoka Kaskazini mwa Chile ikiwa ni baada ya kusota chini ya ardhi kwa muda wa siku 69.
Mkiambiaji huyo ambaye alitumia muda wa siku hizo akiwa chini ya ardhi kwa kina cha meta 700, amekuwa akikimbia kwa siku kadhaa akipita kwenye mahandaki.
Akiwa amevaa kofia rasmi ya mbio hizo za New York Marathon, huku akiwa amefunga goti lake kwa bandeji nyeusi, aliendelea na kasi ya kutosha wakati akiwa amezungukwa na mashabiki wake.
Alikatiza mstari wa kumaliza mbio hizo katika eneo la Central Park, muda wa saa 9:30 baada ya kuanza mbio hizo katika eneo la Staten Island saa 3:40.
Mshindi wa mbio hizo za marathon kwa upande wa wanaume, alikuwa ni Gebre Gebremariam wa Ethiopia huku raia mwingine wa nchi hiyo, ambaye alikuwa akishikilia rekodi ya Dunia, Haile Gebrselassie akiamua kujitoa baada ya kukimbia maili 16, kutokana na kuwa majeruhi wa goti.
No comments:
Post a Comment