Na Addolph Bruno
KOCHA Mkuu wa timu ya Majimaji, Peter Mhina amesema baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa matokeo mabaya, anatarajia kusajili wachezaji watano
ili kuimarisha safu ya ushambuliaji atakayoitumia katika mzunguko wa pili wa ligi hiyo.
Majimaji imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa katika nafasi ya 11 kwa kuwa na pointi nane, ambapo ligi hiyo inaongozwa na mabingwa watetezi Simba yenye pointi 24 na inayoshika mkia ni AFC Arusha ambayo ina pointi tano.
Akizungumza na majira kwa simu akiwa Songea, Mhina alisema kikosi chake hakikuweza kufanya vizuri katika mzunguko wa kwanza kutokana na safu yake ya ushambuliaji kuwa butu.
Alisema katika kipindi hiki cha msimu wa dirisha dogo, atahakikisha analiziba pengo hilo ili kikosi chake kiweze kufanya vizuri zaidi katika kupachika mabao kwenye mzunguko wa pili.
Hata hivyo kocha huyo alisema atawafanyia atawaandaa vizuri wachezaji waliopo, ili waweze kusaidiana na atakaowasajili ili kazi ya ufungaji wa mabao iwe nyepesi.
Mhina alisema mbali na safu yake ya ushambuliaji kuwa butu, pia kikosi chake kilishindwa kufanya vizuri kutokana na kusheheni wachezaji wengi wageni.
No comments:
Post a Comment