08 November 2010

Tunataka ahadi zitekelezwe-Wananchi.

Na Eliasa Ally,


WANANCHI wa Mkoa wa Iringa wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza ahadi zake kama alivyoahidi wakati akisaka kura zao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi hao walisema, katika nafasi ya urais Rais Kikwete alitarajiwa kushinda na kuongeza kuwa, anatakiwa kuweka baraza la wachapa kazi.

Bw. Ajelo Mkini Mkazi wa Frelimo B alisema, Rais Kikwete amepita kutokana na kuwa yeye ni kipenzi cha watu walio wengi na kuongeza kuwa, anatakiwa kuwa makini katika kuwachagua mawaziri wake ili wasije wakamwangusha katika siku za usoni.

"Kinachotakiwa ni kuwapima wale mawaziri waliokuwepo kwa miaka mitano iliyopita kama wamefanya kazi ipasavyo na kuwa, endapo wataweza kustahimili misukosuko ya kufanya kazi za maendeleo na kuiwezesha CCM kupita tena uchaguzi ujao," alisema Bw. Mkini.

Alisema kuwa, mafanikio ya uchaguzi ujao juhudi zake zinatakiwa zianze sasa kwa kutekeleza ilani na ahadi ambazo CCM imewaahidi wananchi katika maeneo yote ikiwa ni pamoja na kuwa na watendaji wazuri katika ngazi za chini.

Bi. Diana Sanyagwa Mkazi wa Mwembetogwa alisema, CCM inatakiwa kuwa makini kwani mwaka huu vyama vya upinzani vimetumia  udhaifu wake na kupata mwanya wa kuchaguliwa.

Bi. Sanyagwa aliongeza kuwa, CCM ilijisahau ambapo vyama vya upinzani katika maeneo waliyoshindwa walijipanga kikamilifu na kwamba, kwa kuanza sasa kutasaidia hapo baadaye.

"Katika maeneo ambayo CCM tumeshindwa kwa sasa, tusianze kutafutana nani mchawi ila kinachotakiwa ni tukae chini, turekebishe kasoro tutakazoziona na kuanza mara moja kutekeleza ilani na ahadi ambazo CCM imewaahidi wananchi wake.

"Vinginevyo tukiingiza sumu nyingine tutaendelea kushindwa jimbo mojamoja na baadaye kuruhusu upinzani kutawala nchi nzima," alisema Bi. Sanyagwa.

Wananchi hao wamemshauri Rais Kikwete kukaa na washauri wake wakiwemo wenyeviti wa CCM wa mikoa na makatibu wao, pia wenyeviti wa CCM wa wilaya zote na makatibu wa ngazi zote ili kuunda mshikamano ambao utawezesha kushinda mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment