10 November 2010

Akina Seif waapishwa Zanzibar.

Na Ali Suleiman, Zanzibar

MAKAMU wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi wamekula kiapo cha utii na uaminifu cha kuitumikia Zanzibar
katika serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar.

Makamu wa pili wa rais ndiye atakuwa kiongozi wa shunguli za Baraza la Wawakilishi.

Wa kwanza kuapishwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein ni Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF).

"Mimi Seif Sharif Hamad naapa nitakuwa muaminifu kwa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano na  kuitumikia kwa moyo wangu wote katika kutekeleza majukumu
yangu nikiwa makamo wa kwanza wa rais," alisema Bw. Hamad katika sehemu ya kiapo.

Balozi Seif Ali Iddi alikula kiapo cha kuwa Makamo wa pili wa rais ambaye pia ni kiongozi wa shunguli za serikali.

Sherehe hizo zilizofanyika Ikulu zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu. wakiwemo wakuu wa vikosi vya ulinzi pamoja na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wengine ni viongozi wa vyama vya siasa, akiwemo
Mwenyekiti wa CUF, Professa Ibrahim Lipumba, Makamo Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Machano Khamis pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Bw. Saleh Ramadhan Ferouz pamoja na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Bw.
Pandu Ameir Kificho.

Hatua ya kuteuliwa watendaji hao wakuu ambao ni washauri wa rais Dkt. Shein ni sehemu ya utaratibu wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo inatokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na viongozi hao wakuu.

Dkt. Shein anatazamiwa kulihutubia Baraza la Wawakilishi kesho ikiwa ni ishara ya kulizinduwa tayati kuanza kutekeleza majukumu yake.

Akizungumzia uteuzi huo, Professa Lipumba alisema ni moja ya dalili njema za kuanza utekelezaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na ni uteuzi mzuri wenye hekima na busara kubwa.

Kilichowafurahisha wafuasi wengi wa CUF ni Maalim Seif kuwasili ikulu akiwa na gari moja tu ya chama chake aina ya Nissan Patrol lakini aliondoka akiwa na msafara wa magari yasiyopunguwa sita akiwa na ulinzi kamili.

1 comment:

  1. 'Ali Suleiman' umesoma wapi journalism wewe? Mwandishi aliefunzwa asingeandika 'Akina...', kumaanisha viongozi maarufu nchini kama kwamba ni watu wasio na nafasi katika jamii.

    Na wewe Mhariri unapaswa kuwahamasisha correspondents wako wawe responsible and 'self editing', vyenginevo utumie 'teeth & tools' ulizonazo!

    ReplyDelete