09 November 2010

Ghana yatoa watatu tuzo ya mchezaji bora Afrika.

CAIRO, Misri

WACHEZAJI watatu raia wa Ghana, akiwemo mshambuliaji wa timu ya Sunderland, Asamoah Gyan wametajwa kwenye orodha ya wachezaji
watakaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Mbali na mchezaji huyo, kiungo Andre Ayew ambaye anakipiga nchini Ufaransa na Kevin Prince Boateng wa AC Mlian pia wametajwa katika orodha hiyo.

Wachezaji hao wanatarajia kukutana na upunzani mkali kutoka kwa mshindi wa tuzo hiyo mara tatu, Samuel Eto'o wa  Cameroon na vinara wa Chelsea kutoka Ivory Coast, Didier Drogba na  Salomon Kalou.

Wachezaji wengine waliotajwa katika orodha hiyo ya juzi ni wachezaji nguli kutoka Misri, Mohamed 'Geddo' Nagy na Ahmed Hassan.

Wachezaji hao watatu ndiyo walikuwa nyenzo muhimu kwa timu ya Black Stars, ambayo ndiyo timu pekee ya Afrika iliyofanikiwa kutinga robo fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Juni, mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Gyan na Ayew pia walicheza katika timu ya taifa ya Ghana, iliyokuwa na wachezaji chipukizi ambayo ilifika fainali kwenye michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika zilizofanyika nchini Angola Janurai mwaka huu.

Kwa upande wake Eto'o, ambaye amewahi kunyakua taji hiyo mara tatu kuanzia mwaka 2003 hadi 2005, aliisaidia  Inter Milan kutwaa Kombe la Ligi ya Mabingwa Ulaya Mei, mwaka huu wakati Drogba aliyetwaa medali hiyo mwaka 2006 na 2009 ndiye alikuwa nguzo ya Chelsea, ambayo ilinyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya England Mei mwaka huu.

Orodha kamili ya wachezaji hao na timu wanazochezea na nchi watokako kwenye mabano ni kama ifuatavyo, Andre Ayew (Marseille/Ufaransa, Ghana), Kevin-Prince Boateng (AC Milan/Italia, Ghana), Madjid Bougherra (Rangers/Scotland, Algeria), Didier Drogba (Chelsea/England, Ivory Coast), Samuel Eto'o (Inter Milan/Italia, Cameroon), Asamoah Gyan (Sunderland/England, Ghana), Ahmed Hassan (Al-Ahly/Misri), Salomon Kalou (Chelsea/England, Ivory Coast), Seydou Keita (Barcelona/Hispania, Mali) na Mohamed 'Geddo' Nagy (Al-Ahly/Misri)

Wengine waliomo katika orodha hiyo ya awali ni Oussama Darragi (Esperance/Tusinia), Michael Eneramo (Esperance/Tunisia, Nigeria), Ahmed Hassan (Al-Ahly/Misri) na Dioko Kaluyituka (TP Mazembe/DRC).

No comments:

Post a Comment