Na Addolph Bruno
BODI ya Wakurugenzi ya Azam FC, inatarajia kukutana leo Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali, ambayo yatawawezesha kumpata kocha mpya wa timu hiyo.
Bodi hiyo inakutana kujadili suala hilo, baada ya klabu hiyo kukatisha mkataba na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazil Itamar Amorin wiki iliyopita kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kwa maslahi ya klabu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo Idrisa Nassoro, alisema bodi hiyo inakutana kujadili suala hilo baada ya kuona wanaendelea kupata maombi mengi wanaomba kuchukua mikoba ya ya Amourin.
"Kwa kuwa suala hili ni kubwa na linahitaji utulivu hasa kutokana na uzito wake, Bodi ya juu ya ukurugenzi ya klabu imeona ikutane kesho (leo), ili kulifanyia kazi kwa makini apatikane kocha ambaye ataifikisha mbali zaidi Azam FC," alisema Nassoro
Nassoro alisema tayari wamepokea maombi ya makocha kutoka zaidi ya nchi nane na bado wanaendelea kupokea kutoka kwa wengine waliowahi kufundisha sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Alisema wanamatumaini makubwa ya kumpata kocha, muda mfupi kuanzia sasa na hadi watakapoanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, kocha mpya ataanza kazi ya kuinoa timu hiyo.
Nassoro alizitaja baadhi ya nchi walizopata maombi kuwa ni Uganda, Kenya, Sweden, Zimbabwe, Tanzania na kuongeza kuwa bado wanaendelea kupokea maombi ya makocha wanaowania nafasi hiyo.
No comments:
Post a Comment