Kampuni na taasisi
mbalimbali nchini zimeshauriwa kujua hali ya afya za wafanyakazi kwa sababu
itasaidia pia kuongeza mchango wao uzalishaji katika sehemu zao za kazi, anaripoti
Mwandishi Wetu.
Kauli hii ilitolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Katibu
Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam
(RAS),Teresia Mbando wakati wa maadhimisho ya Siku ya UkimwiDuniani katika
makao makuu ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Bi.Mbando alisema huku suala la maambukuzi ya VVU / Ukimwi yakiwa
yanaongezeka, ni muhimu kwa kampuni na taasisi kuchukua hatua ya kujua hali ya
afya za wafanyakazi wake akisema kuwa kwa kufanya hivyo itakuwa ni kutekeleza
harakati na mpango wa serikali wa mapambano dhidi ya Ukimwi.
Alisema Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutokomeza ugonjwa
huo na kusema kuwa kwa 'kauli mbiu ya mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya
Ukimwi ya " kufikia asilimia sifuri katika maambukizi mapya,unyanyapaa na
idadi ya vifo vinavyotokana na Ukimwi, inaonyesha kwamba juhudi zaidi zimeelekezwa
kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Mbando aliipongeza TBL kwa kuweka mbele suala la afya ya
wafanyakazi wake na kutoa wito kwa kampuni na taasisi nyingine kuiga mfano huo,
kwani kwa kufanya hivyo kutapunguza kwa kiasi kiwango kikubwa cha maambukizi
mapya.
Kwa upande wake, Meneja Rasilimali wa TBL, David Magesa alisema
tokea mwaka 1990, kampuni hiyo ilikuwa na mpango ambao unawawezesha kupata
huduma ya upimaji wa hiari na Ushauri nasaha.
Magesa alisema pia hadi sasa asilimia 80 ya wafanyakazi wa TBL
wanajua hali ya afya zao, akibainisha kuwa mpango huu unafanyika kutokana na
kuungwa mkono na utawala wa kampuni hiyo.
"Mbali na upimaji wa hiari na Ushauri nasaha, kampuni kupitia
kliniki yake ambayo imejitosheleza inatoa bure dawa za kurefusha maisha (ARVs)
na mpango huo pia unashirikisha zaidi ya asilimia 40 ya wanafamilia wa
wafanyakazi," alisema.
Aidha, Magesa alisema kupitia programu hiyo wameweza kupunguza
idadi ya vifo kwa asilimia 99.9 pamoja na kupunguza kesi za maambukizi ya
magonjwa ya zinaa (STDs) na kuongezea kuwa programu hiyo imekuwa ya manufaa
makubwa si tu klwa wafanyakazi bali hata wasio wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Mbali na hayo alisema kuwa kampuni hiyo
hadi sasa ina waelimishaji rika 116 ambao wanashiriki katika kutoa ushauri kwa wafanyakazi
wenzao ili kuwafanya wawe na ufahamu katika kutambua umuhimu wa kujua hali ya
afya zao.
thanks for sharing article
ReplyDelete