- SASA KUIVAA BURUNDI KESHO
Na Mwandishi Wetu, Nairobi
Kocha Mkuu wa
timu ya Taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Kim Poulsen amesema kwamba
kuwasili katika kikosi chake kwa wachezaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta
kutaongeza nguvu katika kikosi hicho hasa katika mchezo wao wa kesho wa Kombe
la Challenji dhidi ya Burundi
Samatta na
Ulimwengu waliwasili jijini Nairobi wakitokea
kuichezea timu yao, TP Mazembe ya DRC katika
Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo walifungwa jumla ya mabao 3-2 na
timu ya CS Sfaxien ya Tunisia
na hivyo kukosa kombe.
Akizungumza jijini Nairobi
jana, Kim alisema ujio wa wachezaji hao ni ahueni katika kikosi chake ambacho
bado kinakabiliwa na mechi ngumu dhidi ya Burundi kwani aliiona timu hiyo na
anaimani italeta upinzani mkali.
"Wachezaji nilionao ni wazuri
lakini kuongezeka kwa Samatta na Ulimwengu pia kumeongeza nguvu zaidi katika
kikosi changu, hivyo nategemea mechi ya Jumatano itakuwa nzuri zaidi,"
alisema kocha huyo.
Alisema timu zote zinazoshiriki
michuano hiyo hakuna timu kibonde, hivyo hata wakivuka robo fainali bado
watakuwa na kazi ngumu katika kuhakikisha wanatwaa kombe hilo
na kurudi nalo Tanzania.
Kim alisema anaendelea na mazoezi
katika kuboresha kikosi chake, kwani kuna mapungufu ambayo aliyagundua walipocheza
na Somalia, hivyo anatakiwa
kuyafanyia kazi haraka kabla ya mechi yao
ya kesho.
Stars imeambulia
pointi nne na mabao mawili baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Zambia katika mchezo wa kwanza na ushindi wa 1-0
dhidi ya timu dhaifu, Somalia
juzi.
No comments:
Post a Comment