26 November 2013

ZITTO, MKUMBO WAIBUA MAZITO Na Goodluck Hongo
Viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wametakiwa kutumia busara katika maamuzi yao juu ya tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bw. Zitto Kabwe na wenzake ili kulinda masilahi ya chama ambacho msingi wake mkubwa ni watu.

Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Magharibi inayoundwa na mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora, Bw. Mohamed Mambo, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na Majira kwa njia ya simu juu ya uamuzi wa Kamati Kuu, uliomvua madaraka Bw. Kabwe na wenzake.
Wengine waliovuliwa madaraka ya uongozi ni Dkt. Kitila Mkumbo aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanazuoni wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Bw. Samson Mwigamba, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi.
Bw. Mambo alisema ni muhimu viongozi wakuu wa CHADEMA, waangalie jamii inataka nini, kwa wakati gani ambapo Kamati Kuu ya chama hicho ni kikundi cha watu wachache kinachotoa maamuzi ya wanachama wote hivyo maamuzi hayo yaangaliwe vizuri.
“Umakini unahitajika katika jambo hili kwa masilahi ya chama chetu...kamati kuu inaweza kutoa maamuzi yanayoweza kukigawa chama, wanachama wapo tayari kufanya lolote juu ya maamuzi ambayo yatatolewa.
“Nimepokea simu nyingi kutoka mikoa mbalimbali ambayo wanapinga Bw. Kabwe kuvuliwa nyadhifa zake za uongozi katika chama...maeneo mengi kadi za CHADEMA zimerudishwa, wengine walikuwa wanasubiri maamuzi ya Zitto,” alisema Bw. Mambo.
Aliongeza kuwa, kwa kuwa Bw. Kabwe amesema ataendelea kubaki ndani ya chama, wanachama waliorudisha kadi nao wamesema wataendelea kubaki na kudai wapo pamoja naye na wapo tayari kumfuata popote ambako atakwenda.
Bw. Kabwe na wenzake wanadaiwa kukihujumu chama hicho kwa kuandaa waraka unaosema: ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’, hivyo Kamati Kuu iliwapa barua za kujieleza ndani ya siku 14 kwanini wasifukuzwe uanachama kutokana na kosa hilo.
Hata hivyo, Bw. Kabwe juzi alizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa, waraka uliotajwa si sababu ya yeye kuvuliwa nyadhifa za uongozi na Kikao cha Kamati Kuu.
Alisema pamoja na kuvuliwa nyadhifa hizo, hatoki CHADEMA na wanaotaka atoke, wamtoe wao na kwamba atakuwa wa mwisho kutoka na ana imani kubwa na chama chake kuwa ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
Aliongeza kuwa, misukosuko inayoendelea ndani ya chama hicho ni mapambano ya kukuza demokrasia si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment