26 November 2013

CHADEMA KUJIBU UTETEZI



Na Goodluck Hongo
  Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo kitatoa ufafanuzi juu ya hali halisi ya kisiasa nchini pamoja na kutolea ufafanuzi kauli walizodai ni za upotoshaji zilizotolewa na viongozi waliovuliwa vyeo vyao ndani ya chama baada ya kubainika kukisaliti chama hicho.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa chama hicho, Bw. Tumaini Makene, alisema watu wengi wanataka chama hicho kitoe ufafanuzi juu ya utetezi wa viongozi hao, hivyo ukweli wa madai yao utawekwa hadharani.
Alisema hivi sasa kuna mambo mengi yanayoelezwa juu ya chama hicho hasa baada ya Kamati Kuu ya CHADEMA kuwavua nyadhifa za uongozi Bw. Zitto Kabwe aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu Dkt. Kitila Mkumbo.
“ K e s h o ( l e o ) CHADEMA tutazungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama Kinondoni, tutazungumzia hali ya kisiasa nchini pia tutatoa ufafanuzi wa kauli za uongo na upotoshaji ambazo zimetolewa na viongozi waliovuliwa vyeo vyao na Kamati Kuu baada ya kufanya mkutano wao na waandishi juzi,” alisema.
Awali, Kamati Kuu ya chama hicho iliwavua vyeo vyote Bw. Kabwe, Dkt. Mkumbo na Bw. Samson Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa sasa amesimamishwa uongozi wakidaiwa kukisaliti chama hicho na kutaka kukiangamiza.
Katika mtandao huo, Bw. Kabwe anafahamika kama ‘MM’ kwa maaana ya mhusika mkuu, Dkt. Mkumbo M1 (mhusika namba moja), Bw. Mwigamba M2 (mhusika namba mbili).


No comments:

Post a Comment