13 November 2013

WAIGOMEA KAMPUNI YA STRABAG DAR Penina Malundo na Maua Mashu
  Wafanyakazi wakiwemo vibarua zaidi ya 200 wa Kampuni ya STRABAG inayojenga barabara ya mabasi yaendayo kasi jijini Dar es Salaam wamegoma.

Mgomo huo ulianza jana jijini humo kwa madai ya kutaka kulipwa stahiki zao za zamani kabla ya kampuni hiyo kuingia mkataba na kampuni nyingine.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana na waandishi wa habari, wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema kuwa, wameingia katika kampuni hiyo kwa sheria zote na wengi wao wameweza kufanya kazi zaidi ya mwaka mmoja, hivyo wanapaswa kulipwa madai yao kabla ya kuvunja mkataba na Kampuni ya STRABAG.
Walisema kuwa, mgogoro mkubwa uliibuka kati ya vibarua hao na kampuni iliyoingia mkataba na Strabag ijulikanayo kama Laba Constractors juu ya malipo watakayolipwa kuwa madogo tofauti na malipo ya Kampuni ya Strabag.
"Jumamosi tulikaa kikao na viongozi wa Laba Constractors wakatueleza kuwa kuanzia siku ya Jumatatu (juzi), malipo yetu yatakuwa chini yao, kwani wameingia mkataba na Kampuni ya Strabag kwa ajili ya kulipa wafanyakazi wake na vibarua, jambo la kushangaza sisi hatujapata taarifa yoyote kutoka kwa Strabag juu ya mkataba huo walioingia na Kampuni ya Laba Constractors," alisema mmoja wa vibarua hao ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Alisema kuwa, Kampuni ya Strabag ingefanya utaratibu maalumu wa kumaliza madai yote ya msingi kwa vibarua wake na hapo ndipo wangeweza kuanza kuingia mkataba na kampuni nyingine.
"Mpaka sasa hatujui hatma yetu, sisi tumekaa hapa toka saa 12 asubuhi na tutaendelea kukaa mpaka kieleweke hadi tupatiwe haki yetu, malipo yetu tupewe ndiyo kampuni nyingine ianze upya na sisi, kwani tumeshakaa zaidi ya mwaka mmoja, kisheria sisi tayari ni wafanyakazi halali," alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika Kampuni ya STRABAG (TAMICO), Abdullah Rukusa alisema kuwa, Kampuni ya Strabag ilikuwa inawalipa vibarua hao malipo ya sh. 12,500 kwa siku huku malipo ya posho yakiwa sh. 4,800 kwa saa za ziada.
Alisema kuwa, Kampuni ya Laba Contractors inataka kuwalipa vibarua hao kiasi cha sh.10,000 kwa siku hali itakayofanya kampuni hiyo kuwanyonya wafanyakazi hao pindi wanapoanza kazi saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Laba Contractors, Emanuel Mshana alisema kuwa, mkataba kati yao na Kampuni ya Strabag ulisainiwa Jumamosi iliyopita na kazi rasmi ilianza kufanyika juzi huku tayari akidai wamekutana na wafanyakazi hao kwa mazungumzo.
Alisema kuwa, vibarua 95 waliopewa na Kampuni ya Strabag kati yao 45 ndio walioanza kufanya kazi nao juzi na kampuni yao kuongeza vibarua 28 kwa siku, kwa ajili ya kufanya kazi.
Juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Kampuni ya Strabag ziligonga mwamba baada ya kugoma kuzungumza na waandishi wa habari huku geti likizuiliwa na mawe makubwa ya barabaran

No comments:

Post a Comment