13 November 2013

MGAWO CHENJI YA RADA KUONESHWA



 Frank Monyo na Daniel Samson
  Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zuberi Samatabe, amewahimiza walimu wa shule za msingi kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kujisomea vitabu ili kuongeza uelewa katika masomo yao.

Aliyasema hayo katika uzinduzi wa tovuti ya kufuatilia mgawo wa vitabu vya chenji ya Rada uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Lengo la tovuti hiyo ya www. pesptz.org ni kutoa taarifa kwa wadau wa elimu pamoja na wanafunzi juu ya vitabu vinavyosambazwa katika shule za msingi kwa kutumia chenji hiyo.
Alisema, Serikali ya Uingereza iliamuru fedha zilizotumika vibaya katika manunuzi ya Rada zirudishwe kwa Watanzania na zitumike katika manunuzi ya vitabu na madawati kwa shule za msingi.
"Fedha za chenji ya Rada sh. bilioni 72 zilizorudishwa ziliingizwa katika mpango wa manunuzi ya vitabu na madawati katika shule za msingi na asilimia 75 zimetumika katika manunuzi ya vitabu vya wanafunzi na vya mwongozo wa walimu kufundishia," alisema Samatabe.
  Kwa upande wake Meneja Takwimu wa Kampuni ya Data vision International, William Kihula alisema Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Uingereza (DFID) iliwapa jukumu la kutengeneza tovuti kufuatilia mgao wa vitabu vya chenji ya Rada, ili kuwezesha ushirikishwaji wa wadau wa elimu na wananchi katika kufuatilia usambazaji wa vitabu shuleni.
  Alisema hatua hii itawezesha serikali kuendelea kutembelea katika maeneo yake na kuwa na uendeshaji wa uwazi ndio maana wamejenga mfumo huu katika namna ambayo itaweza kutumika na wizara hata baada ya mradi huo wa mgawo wa vitabu vya chenji ya rada kuisha.
"Tovuti hiyo ndio pekee inayoweka mtandaoni majina yote ya shule za hapa nchini wilaya na mikoa iliyopo hii itatoa mwanga wa kuanzia katika ufuatiliaji wa maendeleo ya mwanafunzi mmoja mmoja," alisema Kihula.
  Aliongeza kuwa, kuwepo kwa jitihada za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanza kutumia mfumo mpya wa kupima ufaulu wa wanafunzi kwa kuhusisha "Continous Assessment" kwa kuanza na shule za sekondari.
  "Katika hili Datavision tupo kwenye hatua za mwisho za kutengeneza mfumo wa teknolojia itakayowezesha kupatikana na kutunza taarifa za maendeleo ya mwanafunzi shuleni kwa wakati," alisema Kihula.

No comments:

Post a Comment