Na Fatuma Rashid
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board), imefungia
viwanja saba vilivyokuwa vikitumiwa na timu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na
Ligi Daraja la Kwanza (FDL), hadi vitakapofanyiwa marekebisho ili kukidhi mahitaji
ya mechi za mpira wa miguu.
Akizungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema uamuzi huo umefikiwa na TPL Board
katika kikao chake cha kwanza kilichofanyika juzi ambapo pamoja na mambo
mengine, kilipitia ripoti za mechi za VPL na FDL katika mzunguko wa kwanza.
Alisema viwanja vilivyofungiwa na marekebisho yanayotakiwa kufanyika
kwanza, ili viruhusiwe kutumika tena ni Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba
(majukwaa yake yamechakaa, hivyo kuhatarisha usalama wa watazamaji) na Uwanja
wa CCM Mkwakwani jijini Tanga (vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo (dressing
rooms) havina hadhi.
Wambura alisema Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya (sehemu ya kuchezea-pitch
ni mbovu), Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha (sehemu ya kuchezea ni
mbovu), Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi (vyumba vya kubadilishia kutumika kwa ajili
ya shule ya awali), Uwanja wa Majimaji mjini Songea (pitch ni mbovu) na Uwanja
wa Jamhuri mjini Morogoro (pitch ni mbovu).
Wambura ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, alisema klabu ambazo timu
zake zinatumia viwanja hivyo zimeshataarifiwa rasmi juu ya uamuzi huo, ambapo
ama vinatakiwa kuwasiliana na wamiliki wa viwanja hivyo, ili wafanye
marekebisho au kutafuta viwanja vingine vya kuchezea mechi zao.
Wakati huo huo, timu za Taifa za Future Taifa Stars na Taifa
Stars zinacheza leo. Mechi hiyo ya kirafiki itafanyika Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam kuanzia saa
10 kamili jioni.
Mechi hiyo ni maalumu kwa Benchi la Ufundi la Taifa Stars linaloongozwa
na Kim Poulsen, kuangalia wachezaji kumi kutoka Future Taifa Stars
watakaoongezwa katika Taifa Stars, tayari kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa
itakayochezwa Novemba 19, mwaka huu jijini Arusha.
Watazamaji 300 tu wataruhusiwa kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha
sh. 5,000. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeingia
kambini jana. Miongoni mwa wachezaji wanaotarajia kuripoti ni kipa Ivo Mapunda
wa Gor Mahia.
No comments:
Post a Comment